ISSN 0865-6941 | Toleo Na. 307 | Machi 2016 | |
Ujue Umoja wa Marafiki wa Bukoba (Friends of Bukoba, FoB)Na Enock L. Kamuzora Rais wa BUDEFO, Dar es Salaam Ndugu Wasomaji,Bila shaka baadhi yenu mmewahi kusikia hadithi ya kijiji kimoja kilichokumbwa na njaa kali iliyohatarisha maisha ya watu. Hata Mwalimu Nyerere katika hotuba zake alipenda kusimulia hadithi hii, akitazamia kuwa watu watajifunza kitu kutokana nayo, na hasa vijana kutoka familia masikini walisomeshwa na wazazi wao kwa shida kubwa na baadaye wakaamua kuishi maisha ya kutowajali. Katika kijiji hicho wazee walikaa na kutafakari janga hilo na kuamua kuchukua hatua za haraka kunusuru maisha ya wanakijiji. Kulikuwa na taarifa za kuaminika kuwa nchi moja ya mbali ilikuwa na chakula kingi ambacho wangeweza kukinunua kama wangepata namna ya kufika huko. Hivyo wakaamua kuchagua vijana wanaowaamini na kuwatuma huko na fedha ili wanunue chakula na kukileta haraka iwezekanavyo. Pamoja na umasikini wao, wanakijiji walichanga fedha za kununulia chakula na kugharimia safari ya vijana hao. Vijana waliondoka kuelekea nchi ya neema. Walipofika huko wakakuta chakula kipo kwa wingi, lakini pia wakakuta anasa za kila aina. Badala ya kununua chakula wakaanza kuponda maisha, mpaka fedha zote zikaishia kwenye anasa. Huko nyuma wanakijiji wenzao wakawa wanasubiri kila kukicha bila kuwaona, na wengi wakafariki kwa njaa. Kwa lugha nyepesi vijana hawa walikuwa wasaliti. Kwa lugha ngumu walikuwa wauaji. Walijifikiria wenyewe badala ya kuwafikiria wanakijiji wenzao waliowaamini na kuwapa kile kidogo walichokuwa nacho ili waweze kuwaletea chakula. Dhamiri zao zilizimika, wakawa na tabia ya kinyama. Hadithi hii inatufundisha kuwa sisi tuliobahatika kusoma tunao wajibu wa kuwarudishia ndugu zetu angalau sehemu ndogo ya faida ya usomi wetu, tukizingatia kuwa ndugu zetu hao walijinyima ili sisi tupate na waliishi maisha duni ili tuwe na maisha bora. Tunapowasahau baada ya kusoma na kupata maisha mazuri, tunafanya dhambi mbele ya Mwenyezi Mungu. Kwa kuzingatia haya, wazawa wa mkoa wetu wa Kagera, waliomo ndani ya nchi na waishio ughaibuni, waliamua hivi karibuni kuanzisha umoja wao utakaowawezesha kujipanga kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika mkoa. Walianza kwa kutengeneza jukwaa la mawasiliano ya kielektroniki la kubadilishana mawazo kuhusu maendeleo ya mkoa. Jukwaa hili linaitwa Friends of Bukoba (Marafiki wa Bukoba). Nina furaha kuwajulisha kuwa, mpaka sasa, watu takriban 800 kutoka kila pembe ya dunia, wakiwemo baadhi ya viongozi wetu wa kisiasa na wale wa kidini, tayari ni washiriki wa jukwaa hili. Hatua ya pili ilikuwa ni kuanzisha taasisi zisizo za kiserikali zitakazobuni na kutekeleza miradi na programu za maendeleo. Hivyo mwaka jana zilianzishwa taasisi mbili, yaani Bukoba Development Foundation (BUDEFO) na Bukoba Investment Group (BIG), ambazo tayari zimesajiliwa serikalini. Kwa zote mbili, na kwa jukwaa letu, tumetumia jina Bukoba kwa kuwa ndiyo makao makuu ya mkoa wetu, na ni jina linalojulikana kihistoria kuliko Kagera. Katika makala itakayofuata nitafafanua zaidi kazi za taasisi hizi na jinsi wananchi wa mkoa wetu wanavyoweza kushiriki katika kupanga malengo yake na kuyafanikisha. Mafanikio ya jitihada zetu hizi yatatokana na watu kuona umuhimu wa kuunganisha nguvu zetu kama wazawa wa Kagera. Kama wahenga walivyosema, umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Itaendelea toleo lijalo |