Header
rumuli

ISSN 0865-6941

Toleo Na. 307

Machi 2016

Historia ya Kegera na Watu wake


Wapendwa,
Katika makala hii ambayo tutaendelea nayo kwa vipindi kadhaa tutajaribu kuongelea juu ya mkoa wa Kagera, kwa kuona ni nchi ya aina gani, asili ya watu wake, historia yao, historia ya ukoloni, mila na desturi zao, dini zao za jadi na mwishoni kwa kinaganaga zaidi historia ya uinjilishaji.

Dhumuni la makala hii kwanza ni kujuza hasa vijana juu ya historia ya nchi yao. Kuna wengi ambao chimbuko lao ni Kagera lakini wanapasikia tu au wanakuja kwa msimu lakini wangelipenda kujua baba na babu zao walitoka wapi, utamaduni wao, historia yao na imani zao. Kuna wengine wako mbali na wanaulizwa juu ya chimbuko lao na hawajui wapate wapi habari hizo.

Dhumuni la pili ni kuamsha mjadala kati yetu juu ya historia na nchi yetu. Ninakaribisha mawazo na kujaza pale ambapo mtu ana ujuzi zaidi au ana chimbuko zuri juu ya baba zetu na historia yao. Tusipoandika sasa yote yatasahaulika. Hivyo nawakaribisha nyote tusaidiane kuacha kumbukumbu kwa watoto na wajukuu zetu.

Jiografia ya Kagera
Kagera iko Kaskazini Magharibi mwa Tanzania kati ya uzi 1 na 2.5 Kusini mwa Ikweta kwa latitudi; na kwa longitudo uko katika nyuzi 30.25 na 32.40 Mashariki mwa 'Greenwich'. Mipaka yake ni Ziwa Viktoria Nyanza mashariki na mto Kagera Kaskazini na Magharibi. Kuna sehemu ya Missenyi, yenye eneo la kilomita mraba 1,800, kaskazini mwa mto Kagera ambayo zamani ilikuwa sehemu ya himaya ya Buganda, jimbo la Buddu.

Sehemu hii ilifanywa sehemu ya Tanzania baada ya makubaliano kati ya Wajerumani na Waingereza tarehe 1 Julai 1890 (makubaliano ya Hegoland) yaliyoweka mpaka uzi mmoja kusini mwa ikweta kati ya koloni la Waingereza na lile la Wajerumani. Kagera ina eneo la kilometa mraba 39,168 na kati ya hizo kilometa mraba 10,655 ni eneo la maji.

Ingawa sehemu kubwa ya Kagera ilikuwa na umoja wa kitamaduni, haikuwahi kuwa na umoja wa kiutawala kabla ya wakoloni. Kila utemi ulikuwa unajitegemea. Kagera iliwahi kuitwa majina mbali mbali, iliitwa Kiziba na Waganda kufuatia jina la utemi uliokuwa mpakani mwao na Wamisionari wa kwanza waliotoka Buganda wakatumia jina hilo.

Wakoloni walijenga kituo chao katika ardhi ya ukoo wa Bakoba walioishi mwaloni mwa ziwa Viktoria na kituo kikaitwa Bukoba, jina ambalo mwanzoni liliwakilisha sehemu yote ya Kagera. Mwaka 1959 Kagera ilikatwa kama mkoa na kuitwa Mkoa (kanda) wa Ziwa Magharibi na mwishowe vita vya Iddi Amini vya mwaka 1978-79 vilivyopiganiwa kwenye eneo la mto Kagera, kama kumbukumbu mkoa uliitwa Kagera.

Kagera ni nchi ya milima, ikianzia Ziwa Viktoria Nyanza ambalo liko mita 1300 juu ya bahari, nchi inainuka na inashuka tena kuingia bonde la mto Ngono, inainuka tena kwenye nyanda za juu za Kihanja na Ihangiro sehemu yenye rutuba nyingi, na kushuka tena katika bonde la mto Mwisa. Mito hii miwili, Ngono na Mwisa yenye tingatinga kubwa inamwaga maji yake mtoni Kagera kaskazini. Kutoka bonde la Mwisa nchi inainuka tena katika nyanda za juu za Karagwe mpaka kufikia mita 1750 juu ya bahari. Kusini mwa Kagera toka ziwa Burigi kuna nyanda za chini za Rusubi na Busubi. Mpakani na Burundi kati ya mto Kagera na tawi lake la mto Ruvuvu kuna Bugufi sehemu yenye rutuba na wakazi wengi.

Licha ya mito mikubwa ya Kagera, Mwisa, Ngono na Ruvuvu kuna vijito vingi hasa sehemu ya kaskazini ya Kagera. Vile vile Kagera ina mwambao wa zaidi ya kilomita 150. Kuna maziwa madogo kama Rwanjana, Ikimba, Burigi na Mujungwizi. Karagwe kuna kijito cha maji moto yanayochemka cha "Mutagata". Kijito hiki kinaaminika kuponyesha magonjwa kadhaa hasa ya mifupa na misuri. Hata mvumbuzi wa kizungu Stanley aliyepitia huko mwaka 1876 alijaribu uponyaji huo.

Hali ya hewa ya mkoa wa Kagera kwa ujumla ni ya joto la wastani wa 26.02 sentigredi. Katika sehemu za nyanda za juu za Ihangiro na Karagwe mara nyingine kiwango cha chini hufikia sentigredi 10. Mvua zinanyesha kwa wastani wa milimita 800 nyanda za chini za kusini sehemu za Rusubi hadi milimita 2,000 ukingoni mwa ziwa Viktoria. Mvua hunyesha hasa kipindi cha vuli kati ya mwezi Septemba na Januari na kipindi cha masika kati ya mwezi Machi na Mei. Mvua hizi ndizo zinazowezesha kuwepo kwa uoto wa asili wa kuvutia na hasa zao la ndizi katika maeneo mengi ya mkoa. Mvumbuzi Grant akipitia sehemu ya Karagwe mwaka 1861 akitafuta chanzo cha mto Nile alielezea hivi nchi aliyoiona:

"Hii ni nchi nzuri sana hata wapagazi (kutoka uzaramo) wanaitazama kwa mshangao na kusifia. Bonde moja linalopitiwa na mto unaoelekea ziwa Viktoria Nyanza una miti mizuri ya kila aina pamoja na utajiri wa mimea mbali mbali. Kati ya miti kuna mianzi bila kutaja mashamba makubwa ya ndizi, vile vile nyanda za majani katika milima ya Karagwe na Kishaka na sehemu kubwa imelimwa. Penye misitu na vichaka kuna wanyama wa porini kama viboko na vifaru na wanyama wengine. Kuna maziwa madogo na mito inayotelemka kuelekea mabondeni".

Kagera ni nchi nzuri sana yenye mandhari na historia ya kuvutia sana. Katika toleo lijalo tutaongea juu ya wakazi wa Kagera na chimbuko lao.

Itaendelea toleo lijalo

Jipatie Nakala Yako
Anuani:
Rumuli Printing Press
P. O. Box Private Bag, Bukoba
Cell:+255784-440 159 au +255768 - 761 270
Fax:2222113
E-mail: rumulipaper@hotmail.com

Contact Information
Bishop's House Ntungamo,
P.O.Box Private Bag,
Bukoba, Tanzania.
Tel. & Fax. 028 - 2220746
Office: Tel. 028 - 2220194
E-mail: b.officebk@yahoo.com
Website: www.bukobadiocese.co.tz
© Bukoba Catholic Diocese 2023
Find us on
Facebook: Bukoba Catholic Diocese
Twitter:  @bcdcatholic