Babu yake Yohana Maria Muzeeyi aliitwa Mianda wa ukoo wa nyati (abazirambogo). Mianda alikuwa na ndugu yake aitwaye Binagwa. Wote wawili walihama kutoka Bunyoro, Kaskazini Magharibi mwa Uganda na kulekea Karagwe. Walipofika Karagwe, mtemi wa eneo hili aliwaruhusu kumiliki kijiji cha Buimba katika wilaya ya sasa ya Karagwe. Hadi leo kijiji hiki kinamilikiwa na wingi wa wanaukoo wa nyati walioachwa na Mianda na nduguye.
Hawakukaa sana katika kijiji hiki; walihama tena kuelekea Kiziba. Walipofika Omuibuga (maeneo ya Kitengule), Binagwa alienda Kiziba. Mtawala wa Kiziba wakati ule alimruhusu kuishi katika kijiji cha Busheza huko Ruzinga. Mianda naye alivuka mto Kagera kwenye sehemu iitwayo Nyamilima hadi Lwakalisa na kusogea hadi Minziro kwenye kilima cha Kabare. Wakati huo Minziro palikuwa patupu bila mkazi yeyote. Ikumbukwe kuwa, kwa watu wa zamani, kuhama hama lilikuwa jambo la kawaida. Sababu zilizowafanya wahame ni pamoja na kukimbia mapigano ya kivita, kutafuta sehemu zenye rutuba kwa ajili ya kilimo na kutafuta jamaa zao waliosambaratika kwa sababu ya njaa na vita. Haijulikani ni ipi kati ya sababu hizi tatu iliwafanya Mianda na Binagwa wahame hame.
Akiwa Kishomberwa, Mianda alizaa watoto wanne: Lusunga lwa Kabale (alimwita hivyo ili kuenzi makazi yake ya kwanza kwenye kilima cha Kabale), Wandyaka, Bunyaga na Kitasimbwa. Baadaye Bunyaga (mtoto wa watutu wa Mianda) alioa msichana kwa jina la Mukatunzi wa ukoo wa nyani (abazirankende) kutoka kijiji jirani cha Kilaiya. Mukatunzi alijulikana pia kwa majina ya Kashwa, Nnamalayo na Kabbejja (binti mfalme). Alipooa, baba yake alimpatia shamba lililoko katika kijiji cha Kishomberwa chini ya kilima cha Kabale. Inasemekana kuwa Bunyaga alikuwa na wake wengi pamoja na idadi kubwa ya watoto. Mukatunzi alipopata mimba alirudi kwao Kilaiya kama ilivyokuwa desturi. Siku zake za kuzaa zilipokaribia, wazazi wake walimwamuru arudi kwa mumewe Kishomberwa ili azalie huko. Walifanya hivyo kwa kuepa usumbufu wa kutimiza mila na desturi endapo angezaa mapacha. Mukatunzi alirudi kwa mumewe Kishomberwa na baada ya siku chache akamzaa mtoto wa kiume ambaye ndiye Yohana Maria Muzeeyi. Ilikuwa kati ya mwaka 1852 na 1857. Muzeyi alipozaliwa alipewa jina la ukoo Kiwanuka, lakaini wazazi wake walizoea kumwita jina la utani la Musoke, maana yake upinde wa mvua. Baadaye Bunyaga alihama na familia yake kutoka Kishomberwa hadi Kakuuto katika wilaya ya sasa ya Masaka. Wakati huo Yohana Maria Muzeyi alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili. Baada ya kukaa Kakuuto kwa miaka kadhaa, Mtemi wa eneo hilo alimteua Bunyaga kwenda kutoa huduma katika Ikulu ya Kabaka kwa kuzingatia desturi za utawala wa wakati ule. Alipoondoka, aliambatana na mwanae Muzeeyi ili amsaidie katika shughuli za nyumani wakati yeye atakapokuwa anahudumu ndani ya Ikulu. Zamu yake ya utumishi ilipomalizika, alitaka kurudi na mtoto wake Muzeyi. Lakini habari za Muzeeyi kuhusu tabia na mwenendo wake mzuri zilishamfikia Kabaka. Hivyo Kabaka Mutesa I aliamuru Yohana Maria Muzeeyi abaki ili asaidie katika utumishi ndani ya Ikulu pamoja na vijana wengine. Bunyaga aliafiki kwa moyo radhi maadamu ilikuwa heshima kwake kuona mwanae anafanya kazi katika mazingira ya Ikulu. Huo ndio ulikuwa mwanzo wa Yohana maria Muzeeyi kuishi katika Ikulu ya Kabaka.
Yohana Maria Muzeeyi alizaliwa katika familia ya kipaganai na kulelewa katika mazingira hayo hayo. Aliyapokea vema mapokeo ya mababu zake. Alipoingizwa katika mazingira ya Ikulu ya Kabaka, alikutana na waislamu. Aliyafuata mafundisho ya waislamu na kuingizwa katika uislamu. Alipewa jina la Jamali, yaani mtu mwema na mwenye baraka. Walimwona kuwa ni 'mtu mwenye bahati njema.' Jamali alipewa pia jina la Muzeeyi yaani MZEE, kwa sababu ingawa alikuwa kijana mbichi, alionekana kama mzee mwenye busara kwa mawazo, maongezi na matendo yake. Aliweza kutoa ushauri hata kwa watu wazima. Kamwe hakusita kutumia hekima yake. Ajiunga na Uprotestanti
Wamisionari wa Kiprotestanti walipowasiri nchini Uganda na kuanza kuhubiri Injili, Yohana Maria alivutwa na mahubiri yao. Alipenda sana kusikiliza maneno ya Yesu Kristo. Huo ulikuwa mwaka wa 1881. Ingawa aliyafuata mafundisho hayo, Yohana Maria Muzeeyi hakuwahi kubatizwa na waprotestanti. Wakati huo Muzeeyi alikuwa anaishi Mutundwe mbali kidogo na Ikulu. Hatimaye Ajiunga na Ukatoliki
Tarehe 17.2.1879, Wamisionari wa Kikatoliki waliwasili Uganda na kuanza kueneza Injili. Basi Yohana Maria Muzeeyi alipotoka Mutundwe na kurejea katika Ikulu, wenzake akina Yozefu Mukasa Balikuddembe, Mathias Mulumba Kalemba, Matayo Kirevu na wengine alikuta kwamba waliisha anza kujifunza dini ya mapadre wa Kikatoliki. Naye alifurahi pia alionesha moyo wa kuvutiwa na mafundisho hayo. Ndipo alipoomba kufuatana nao watakapokwenda kwa mapadre.
Yosefu Mukasa Balikuddembe alimpeleka Yohana Maria Muzeeyi na kumtambulisha kwa mapadre. Mara Yohana Maria Muzeeyi akaamua kuyafuata mafundisho ya mapadre wakatoliki. Alianza kujifunza sala za kawaida. Katika muda wa siku tatu tu, aliisha kuzikariri sala za asubuhi na Jioni. Wenzake na mapadre wao walimshangaa sana. Pia aliweza kuikariri katekisimu nzima katika muda wa siku kumi na nne tu! Lakini pamoja na kuikariri katekisimu haraka hivyo, mapadre walisita kumbatiza mapema. Hii ilisababishwa na kuhama hama kwake kutoka dini hii hadi nyingine. Walitaka kumchunguza vizuri kabla ya kumbatiza na kuhakikisha kama kweli ana moyo wa kuwa mkatoliki. Wakati huo Yohana Maria Muzeeyi alikuwa na umri karibu miaka ishirini na mitano. Mapadre walipokimbilia Bukumbi-Tanganyika, Yohana Maria Muzeeyi alikuwa hajabatizwa bado. Huo ulikuwa ni mwaka wa 1882. Hata hivyo hakukata tamaa. Aliendelea na moyo wa kujifunza dini na kuwafundisha watumishi wenzake. Hakuwa mchoyo katika kuwamegea rafiki zake imani aliyokuwa nayo. Yosefu Mukasa Balikuddembe alipopewa uongozi wa watumishi wenzake katika Ikulu, aliwakusanya wanafunzi wa dini na kuwaajiri. Baadhi ya vijana aliwapa kazi katika Ikulu na wengine katika Bulaage, yaani Mahakama Kuu ya Kabaka. Tendo hilo liliwapa mwanya mzuri wa kuchukua mafundisho ya dini kwa pamoja.
Baada ya kifo cha Kabaka Mutesa I, vijana wote watumishi katika Ikulu walifukuzwa na kuamriwa kwenda kuishi Kasubi-Bugashani yaani nafasi ya makaburi ya Makabaka. Kazi yao ilikuwa ni kukoka moto na kuyatunza makaburi ya Makabaka. Yohana Maria Muzeeyi hakukaa huko kwa muda mrefu. Matayo Kirevu alimshauri kuwa si halali kwake yeye aliye mfuasi wa Kristo kukaa Bugashani na kutimiza ibada za kishenzi pale makaburini. Alimsihi ahamie nyumbani kwake. Yohana Maria alikubali na akahamia katika nyumba ya Kirevu. Kirevu alikuwa ni chifu wa Bbuye. Wakati Yohana Maria Muzeeyi alipokuwa akikaa Bbuye, aliwasiliana sana na watumishi wapya katika Ikulu. Pia aliwatembelea mara kwa mara. Kabaka Mwanga alipotawala, aliwaita vijana wote waliotumikia Ikulu wakati wa utawala wa baba yake, Mutesa I warudi katika Ikulu. Lakini Yohana Maria Muzeeyi aliendelea kukaa Bbuye. Yozefu Mukasa Balikuddembe, Yohana Maria Muzeeyi na Kajane walijadiliana pamoja jinsi watakavyomwomba Mwanga ili awaruhusu mapadre warudi Buganda kutoka uhamishoni Bukumbi- Tanganyika. Kijane ndiye aliyekuwa wa kwanza kutoa habari za majadilianno hayo kwa Kabaka Mwanga. Mwanga alipokea ombi hilio kwa moyo radhi na kutoa ruhusa kwa wamisionari wakatoliki kurudi Uganda. Mapadre waliporudi Uganda walimkuta Yohana Maria Muzeeyi akiishi kwenye nyumba ya Matayo Kirevu. Alikuwa akishughulika kama Katekista.
Yohana Maria Muzeeyi alibatizwa na Padre Lourdel Mapeera tarehe 1 Novemba 1885. Alipewa jina la kikristu la JEAN MARIE – matamshi yake kwa lugha ya Kifaransa yanafanana na jina la JAMALI alilokuwa amepewa na waislamu. Siku hiyo ilikuwa ni siku ya furaha kuu, siyo kwa Yohana Maria Muzeeyi tu na wenzake bali kwa mapadre pia. Tunasoma katika kumbukumbu za kila siku za Padre Mapeera: "Leo katika Sikukuu ya Watakatifu Wote tumebatiza wakatekumeni ishirini na wawili. Tazama, padre anapombatiza mtu kwa maji ya ubatizo, mbatizwa hutakatifuzwa na kuwekwa wakfu. Huwekwa huru kutoka katika minyororo ya dhambi na ya shetani. Leo kwa hakika tunaweza kuwaomba watakatifu, waombezi wetu wa mbinguni, kuiombea nchi ya Uganda. Tunahisi kuwa nchi ya Uganda itapata matatizo mengi. Hadi kufika sikukuu nyingine ya Watakatifu Wote, baadhi ya wakrito wapya watakuwa wamekwisha mwaga damu yao kwa ajili ya dini yao. Ndio mashahidi wa mbinguni watakaopokelewa huko mara moja na watakuwa ni waombezi wetu. Damu yao itamwagwa juu ya ardhi hii iweze kuzaa wakristo wengi sana. Yesu Kristo atashinda na shetani atashindwa. Watu wengi sana wataokolewa." Jambo walilolibashiri wamisionari halikukawia kutimia. Kabaka Mwanga alikorofika na kuanza kuwabughudhi mapadre na wakristo sawia. Mwisho baadhi yao iliwabidi kumwaga damu yao kwa ajili ya imani yao. Dhabihu ya Namugongo ya tarehe 3 Juni 1886 ndicho kilikuwa kilele cha mateso kwa wakristo.
Baada ya ubatizo wake, Yohana Maria Muzeeyi aliendelea kujifunza zaidi na zaidi mintarafu imani yake. Mara nyingi alienda kwa mapadre kufundishwa na kuwaulizia juu ya mambo yahusuyo dini ambayo alikuwa hajafahamu bado. Kwa sababu ya wepesi wa kuyakariri mafundisho ya dini, mapadre hawakusita kumfahamisha mafundisho ya msingi ya imani ya kikristo. Baadaye yeye Yohana Maria alienda na kuwafundisha wenzake. Padre Mapera alikuwa na haya ya kusema juu ya Yohana Maria Muzeeyi: "Kila wakati Yohana Maria Muzeeyi anafikiria juu ya kuwafundisha wenzake dini na kuwafafanulia Katekisimu. Anasuluhusisha matatizo ya wakatekumeni. Kila jambo linalowatinga wakatemumeni wanamwendea Yohana Maria Muzeeyi kwa ushauri na ufafanuzi. Anawasuluhisha wagomvi bila upendeleo. Yohana Maria Muzeyi ni mtu mwadilifu na mwenye huruma. Ni kijana mpevu lakini hata watoto wanampenda" Padre Lourdel anaendelea kumweleza Yohana Maria Muzeeyi kuwa: "...ni mmojawapo wa wakristu wetu wema. Ni mcheshi na mstahimilivu. Ingawa ni kijana, yu tayari daima kuwasaidia wenzake na kuwaongoza. Katika Uganda nzima, ni mtu pekee mwenye heshima kwa mapadre. Wakati wenzake wanapoangua vicheko, yeye hutabasamu tu. Huwasaidia wenzake bila kujali maslahi binafsi. Mtu hamwombi kitu akanyimwa. Asipompa, basi hana aombwacho."
Yohana Maria Muzeyi alikuwa akiwasaidia sana wagonjwa na wenye shida. Hata kabla ya kubatizwa kwake alishirikiana sana na Matayo Kasule katika kuwahudumia wagonjwa. Aliwabatiza wakatekumeni wengi katika hatari ya kufa. Kwa kufanya hivyo, aliwahudumia wagonjwa kimwili na kiroho. Hata Kabaka Mutesa I alipokuwa kufani, tunaambiwa kuwa aliwachagua vijana wawili ili wamuuguze, nao ni: Josefu Mukasa Balikuddembe na Yohana Maria Muzeeyi. Wote kwa pamoja walimtunza vizuri hadi alipoaga dunia. Inasemekana kuwa walimwongelea juu ya ubatizo na dini kwa ujumla, lakini hakuna ushahidi kuonesha kuwa alikubali kubatizwa au la. Watu wengine walivumisha kuwa alikubali kubatizwa alipokuwa kufani na kwamba Yozefu Mukasa Balikuddembe ndiye aliyembatiza. Tauni ilipozuka katika Ikulu ya Kabaka mwaka 1881 Yohana Maria Muzeeyi alionesha moyo wa pekee katika kuwahudumia waathirika. Wakati watu wengine waliwakimbia wagonjwa hao kwa hofu ya kuambukizwa, yeye hakuchelea katu kuambukizwa ugonjwa huo. Kilichowaogofya zaidi ni kwamba ugonjwa huo haukuwa na tiba wala kinga. Wakati huo huo Yohana Maria Muzeeyi aliomba likizo bila malipo ili apate nafasi tele ya kutoa huduma kwa wagonjwa. Kabaka alimpa ruhusa mara moja. Naye alienda kuishi katika kijiji cha Mutundwe ambacho kilikuwa kimeathiriwa sana na ugonjwa huo. Pamoja na kuwapa huduma za kimwili wagonjwa hao, aliwafundisha dini. Mkombozi wa Watumwa Nyakati za Yohana Maria Muzeeyi, biashara ya watumwa ilikuwa imeshamiri sana katika Uganda. Yohana Maria Muzeeyi alikitumia kipato chake kuwakomboa watumwa. Pindi alipoishiwa aliwaomba wenzake wachange hela ya kuwakomboea watumwa. Mara nyingi alifanikiwa kupata misaada hiyo. Wale aliowakomboa utumwani aliwafundisha dini na kwa njia hiyo aliwaweka huru kimwili na kiroho. Siku moja alikuwa amekwenda kuwatembelea mapadre. Alipofika kwa mapadre alipata habari kuwa ipo haja ya kumkomboa mtumwa ambaye pia ni mkatekumeni. Mara moja alienda kwa bwana wa mtumwa yule na kumwomba amwachilie huru. Lakini yule bwana hakuwa tayari. Ndipo Yohana Maria Muzeyi alipojitoa kumnunua. Yule bwana kabla ya kumwuuza mtumwa wake, alimpeleka kwanza kwa waislamu wakamtahiri. Baadaye akamwuuza kwa Yohana Maria Muzeeyi. Naye mara moja alimpeleka kwa Mapadre. Mapadre walifurahi sana. Yohana Maria Muzeeyi alipoulizwa kiasi cha fedha alichotumia kumkombolea mtumwa yule ili wapate kumfidia, alikataa na kusema, "Fedha hizo ambazo mgenifidia, zitumie kwa kumkombolea mtumwa mwingine!"
Ingawa Yohana Maria Muzeeyi alikuwa amekwisha fikia umri wa kuoa, na alikuwa na uwezo wa kuoa, hakufanya hivyo. Matayo Kirevu aliyekaa naye kwa muda mrefu anasema kuwa Yohana Maria Muzeeyi hakuoa wala hakuwa na mpango huo. Siku moja wakristu wenzake walimwambia kuwa Padre Livinhac anarejea Uganda akiwa tayari askofu na ameagiza kuwa hapendi kumkuta mkristu wa makamo hajaoa bado. Hata mapadre walirudia tena na tena kulisema jambo hilo. Nao wakristu walimwuliza Yohana Maria Muzeyi, "Mbona hushughulikii kuoa? Hujayasikia maneno ya Padre Lourdel?" Lakini yeye aliwajibu kwa utulivu, "Askofu atakapowasili Uganda na kuniamuru kuoa nitaoa, bila amri sitaoa!" Tangu wakati huo Yohana Maria Muzeeyi hakuongea tena juu ya kuoa. Askofu Livinhac alipowasili Uganda hakutoa amri ya wakristo wote wazima kuoa. Ndipo Yohana Maria Muzeeyi alipoowaambia rafiki zake, "Kwa hilo la kuoa nalo nimelipona." Katika nyumba ya Matayo Kisule, alikuwamo mjakazi mwenye sura mbaya, na ndiye huyo ambaye Yohana Maria Muzeeyi alikuwa awe mke wake iwapo Askofu angelimshurutisha kuoa. Alikaa kapera maisha yake yote. Mara kwa mara aliwambia watu kuwa mapadre wangalikubali angalaijiunga na mabruda wao. Inasemekana kuwa hata mapadre walipomshawishi aoe aliwajibu, "Ninyi mkioa nami pia nitaoa." Tangu hapo hawakumsumbua tena na wazo hilo. Baada ya kifodini cha Yohana Maria Muzeeyi, Padre Lourdel alikuwa na haya ya kusema: "Yohana Maria Muzeeyi alikuwa ni mtu mwema sana. Ingawa alikuwa na umri wa kutosha na nafasi nzuri ya kuoa na kuzaa watoto alichagua kutooa maisha yake yote. Hii ni neema ya Mungu Mwenyezi. Mwenyezi Mungu ana uwezo wa kupanda ua zuri mahali popote hata pawe pakame namna gani. Katika maisha ya Yohana Maria Muzeeyi, Mwenyezi Mungu anamfariji Padre anayeishi kati ya watu waliooa."
Miezi ya Novemba1885 hadi Machi 1886 ilikuwa ya wasiwasi mwingi kwa wakristo. Mwanga alipania kuwafutilia mbali wakristo na ukristo wao. Ndipo mapadre walipowashauri wakristo waingie mafichoni, huku wakimnukulu Bwana wetu Yesu Kristo: "Watu wakiwadhulumu niyi katika mji mmoja, kimbilieni mji mwingine" (Mt 10:23). Walifundishwa kuwa kujificha kwa namna hiyo siyo kukana dini, lakini atakayekamatwa kamwe asiikane dini yake. Yohana Maria Muzeeyi aliendelea kufundisha dini huko huko mafichoni. Alikuwa akishirikiana na akina Matayo Kirevu, Yozefu Kaddu na Sepiria Kamya katika shughuli hiyo ya ufundishaji dini. Walikuwa kwa pamoja wakitoa mafundisho ya dini hasa nyakati za usiku. Wakristo waliposikia kuwa Askofu Livinhac amewasili Uganda katika misioni ya Lubaga, wote kwa pamoja walitoka mafichoni, wakaenda kumsalimu. Askofu Livinhac aliwashauri wakristo waendelee kukaa mafichoni. Wakristo wale ambao bado walikuwa hawajapewa Sakramenti ya Kipaimara walipewa ratiba ya maandalizi. Baada ya muda walipewa Kipaimara. Yohana Maria Muzeeyi alipewa Kipaimara tarehe 4 Juni 1886, siku moja baada ya dhabihu ya Namugongo. Katika kipindi hicho cha wasiwasi, waamini tisini na saba walipewa Sakramenti ya Kipaimara.
Askofu Livinhac alishangazwa na ujasiri wa wakristo wachanga jinsi walivyokuwa tayari kukabili madhulumu, mateso na hata kifo. Kwa wakati huo, mapadre waliwashauri wakristo waliokuwa na jamaa zao mbali na Ikulu wahamie huko. Yohana Maria Muzeeyi alihamia katika kijiji cha Kyaddondo kwa jamaa yake aliyeitwa Ssebowa. Aliambatana na rafiki yake kwa jina la Mugwanya. Walikaa humo kwa kitambo. Baadaye wakawa wanahama hama kutoka nyumba hii kwenda nyumba nyingine wakiwazungukia wakristo na kuwaimarisha. Hatimaye Yohana Maria Muzeeyi aliposikia kuwa Matayo Kirevu ameachiwa huru, alikwenda kukaa kwake. Kabaka alikuwa amemkamata na kumweka gerezani lakini baaadye alimsamehe. Toka kwa Matayo Kirevu, Yohana Maria Muzeeyi alikuwa akienda kwa siri kuonana na mapadre pale misioni. Dhumuni kuu lilikuwa ni kwenda kuhudhuria Misa na kupokea Sakramenti ya Ekaristi. Basi ikawa kwa moyo mmoja, Yohana Maria Muzeeyi aliendelea kufundisha dini kama Katekista.
Mwishoni mwa mwaka 1886, ugonjwa wa kipindupindu ulizuka nchini Uganda. Watu wengi sana walikufa. Kabaka Mwanga aliwatangazia watu wote kuwa ugonjwa huo umesababishwa na wakristo. Kwamba hiyo ilikuwa ni laana kwa wakristo, na wakristo wote watakufa – hatabaki hata mmoja! Aliendelea kuwaeleza watu kuwa hayo yalikuwa ni matokeo ya sala yake kwa miungu, kwa maana alikuwa ameomba ati wakristo wote wafe. Lakini alipoona kuwa ugonjwa huo umeenea hata katika Ikulu yake aliogopa sana. Alihama Ikulu na kukimbilia kwenye Ikulu ndogo ya Munyonyo. Yohana Maria Muzeeyi alijifunga kibwebwe na kuwahudumia wagonjwa hao kwa moyo na nguvu zake zote. Wengi wa wagonjwa aliowaahudumia walibatizwa kufani. Mmoja wa hao waliobatizwa ni Simoni Kibuka ambaye tarehe yake ya ubatizo ni 22 Januari 1887. Kadiri watu walivyoedelea kufa kwa wingi ndivyo woga wa Kabaka ulivyozidi. Aliogopa sana na kusema kuwa Mungu wa wakristu amekasirika na sasa analipiza kisasi. Vilevile washauri wake walimgombeza na kumshauri aache tabia yake ya kuwaua waumini. Mama yake pia alimwonya aache kuwaua watu wa Mungu. Mwanga aliona kwamba sasa mambo yamemtinga pande zote, alikiri na kuapa kuwa hatawatesa wakristo tena.
Baada ya uamuzi wake huo wa kutoendelea kuwatesa wakristo, Mwanga alikuwa bado na kinyongo na Yohana Maria Muzeeyi, Yozefu Kaddu na Sepria Kamya. Hawa walikuwa ni mashujaa wa kufundisha dini. Hivyo tangu mwanzo wa kuwatesa wakristo majina yao yalikuwa miongoni mwa wale waliokuwa wakitafutwa na maaskari wa Kabaka Mwanga ingawa mpaka wakati huo walikuwa hawajakamatwa bado. Walikuwa wakiwakwepa maaskari na kujificha. Kabaka Mwanga alikuwa ametoa amri ya kuwatafuta kwa kila hali. Iliposhindakana kuwakamata, Mwanga alishauriana na katikiro wake jinsi ya kuwanasa. Mbinu waliyoipanga ilikuwa kwamba itangazwe katika utawala mzima wa Kabaka Mwanga kwamba watumishi wote waliotumikia katika Ikulu tangu enzi za Kabaka Mutesa I watatuzwa. Ilikuwa ni kama kuwapa kiinua mgogo au malipo ya uzeeni. Pia kwamba wakristo nao wamesamehewa, hivyo nao waje kupokea tuzo zao. Mwanga aliahidi kwamba atawapa mashamba na kutoa uhuru wa dini. Ujumbe huo ulitangazwa katika himaya nzima ya Kabaka Mwanga. Basi tangu hapo waamini wakaanza kujifunza dini kwa nguvu, ingawa bado walikuwa na wasiwasi juu ya tangazo la Kabaka. Yohana Maria Muzeeyi aliposikia habari hizi alifurahi sana. Kwa wakati huo alikuwa ameishachoshwa na hali ya kuhamahama na kujificha. Hata hivyo alionya kuwa ujumbe wa Kabaka Mwanga ni mbinu ya kuwanasa wakristo ili awaue. Mwishowe alijipa moyo na kusema: "Nitaenda kwa kabaka Mwanga. Ikiwa atanipa shamba, basi waamini watapata nafasi ya kukutanikia. Nitalifanya kuwa kituo cha kufundishia dini. Toka hapo nitawapeleka wakristo na kuwatambulisha kwa Kabaka Mwanga. Iwapo ataniua, waamini waendelee kujificha. Naamini kuwa hii ni hila ya Kabaka Mwanga. Mbona hajawaachia wafungwa wa dini?"
Rafiki zake walijitahidi kumshauri asiende Ikulu lakini yeye alikataa. Baadaye alikwenda kutafuta ushauri kutoka kwa mapadre. Nao mapadre walimshauri afuate uamuzi wake mwenyewe; kwenda Ikulu kuonana na Kabaka ana kwa ana au la. Ili aweze kumanasa vizuri, Kabaka Mwanga alimtuma Kalungi aliyekuwa Mweka Hazina Mkuu wa Ikulu apeleke ujumbe huo binafsi kwa Yohana Maria Muzeeyi. Kalungi alipeleleza na kujua alipokuwa Yohana Maria Muzeeyi. Wakati huo Yohana Maria Muzeeyi alikuwa amejificha katika nyumba ya Stanislaus Mugwanya ambaye alikuwa mkatoliki shupavu. Ingawa Kalungi alijulikana na kusifiwa kwa werevu wake wa kung'amua mambo, siku hiyo alihadaika na kuupeleka ujumbe wa Kabaka Mwanga kwa Yohana Maria Muzeeyi. Rafiki zake Yohana Maria Muzeeyi walizidi kumsihi aendelee kujificha kwa kuwa waliamini kuwa Kabaka Mwanga anataka kumwuua tu. Naye aliwajibu kwa utulivu: "Nitakimbiakimbia na kujificha mpaka lini? Nitakimbilia wapi? Nchi nzima ya Uganda ni himaya yake Kabaka Mwanga! Liwalo na liwe, nitaenda kwake. Akitaka kuniua basi na aniue. Sina neno lolote baya na Kabaka Mwanga. Akiniua najua kwa yakini kuwa nakufa kwa ajili ya dini yangu." Siku hiyo Yohana Maria Muzeeyi alichukua uamuzi wa kishujaa. Mara moja akafunga safari na kwenda kuonana na Kabaka Mwanga. Kabla ya kuondoka aliwaambia rafiki zake kuwa ameitwa Ikulu na anaenda sasa moja kwa moja. Matayo Kirevu alimsihi na kumwambia, "Kweli unaenda kufa na kuniachia kazi ya kufundisha dini peke yangu? Kazi hii ni nzuri sana. Usiende." Naye alimjibu, "Ni heri kufa na kuingia katika uzima wa milele."
Ndipo Yohana Maria Muzeeyi alipoanza safari ya kwenda Ikulu. Njiani alitua kwa Matayo Kisule na kulala humo. Matayo Kisule naye alimsihi Muzeeyi asiende Ikulu lakini alikataa. Kisule alimtuma Kirevu aje kwake ili kwa pamoja wamsihi Yohana Maria Muzeeyi asiende Ikulu. Lakini yeye aliwauliza kwa majonzi makubwa: "Je, mnataka kunizuia nisiende mbinguni?" Kisha akawaaga akaendelea na safari kuelekea Ikulu. Wote wawili waliinuka na kumsindikiza. Maongezi yao wakiwa njiani yalihusu dini na maendeleo yake. Walipitia kusini mwa Lubaga, wakashika njia ipitayo katikakati mwa Lubaga na Mengo. Yohana Maria Muzeeyi alipoelekea katika nyumba ya Kalungi, wao wakarudi nyumbani. Hiyo ndiyo ilikuwa mara ya mwisho ya kuonana na Yohana Maria Muzeeyi akiwa hai.
Yohana Maria Muzeeyi alipoingia ndani ya nyumba ya Kalungi, mara moja Kalungi alimpeleka katika Ikulu ya Kabaka. Kabaka Mwanga alipomwona Yohana Maria Muzeeyi alijifanya kufurahi kweli; lakini ilikuwa ni furaha ya kinafiki. Walipoagana, Kabaka Mwanga aliamuru Yohana Maria Muzeeyi apelekwe kwa Katikiro eti ampe shamba pamoja na vijakazi wawili wa kumtunzia shamba hilo. Mwanga alimshauri Yohana Maria Muzeeyi awalete rafiki zake wengine ili nao wapewe mashamba pamoja na vijakazi. Yohana Maria Muzeeyi alipofika katika uwanda wa Mukasa (Katikiro wa Kabaka Mwanga), Mukasa alirudia ahadi zile zile kama za Kabaka. Alimshauri Yohana Maria arudi kesho yake pamoja na rafiki zake wote waweze kugawiwa mashamba pamoja na kupewa vijakazi. Kati ya hao, waliotajwa kwa majina ni Sepria Kamyuka, Yozefu Kaddu, Matayo Kisule na Matayo Kirevu. Yohana Maria Muzeeyi alipokuwa njiani kutoka kwa Katikiro, alitafakari sana juu ya ahadi za Kabaka Mwanga zilizorudiwa na Mukasa, Katikiro wake. Mara aling'amua kuwa hizo zilikuwa ni mbinu za kuwanasa wakristo shupavu. Akaamua kurudi peke yake bila kuambatana na wale waliotajwa na Katikiro. Basi Yohana Maria Muzeeyi alienda kwa wakristo wenzake na kulala huko. Kesho yake alirudi kwa Katikiro. Katikiro alipomwona yu peke yake, alishangaa na kumfokea kwa ukali, "Rafiki zako niliokuagiza uje nao wako wapi? Hutaki nao wapewe mashamba na vijakazi? Rudi sasa hivi uwatafute na kesho uje nao!" Yohana Maria Muzeeyi alirudi kule kule alikolala jana yake, wala hakujisumbua na kuwatafuta rafiki zake maana alishazitambua hila za Kabaka Mwanga na Mukasa katikiro wake.
Kesho yake, kabla ya kwenda kwa Katikiro, Yohana Maria Muzeeyi alienda kanisani kuhudhuria Misa pamoja na kupokea Ekaristi Takatifu. Kwa nguvu hiyo alifunga safari kwenda kwa katikiro. Hakurudi tena. Alipofika kwa katikiro aliuawa. Baada ya kumwua walikitupa kiwiliwili chake kwenye bwawa lililokuwa ndani ya ugo wa Katikiro. Bawa hilo lilikuwa katika tingatinga liitwalo Jjugula, katikati ya Mengo na Namilembe. Yohana Maria Muzeeyi aliuawa akiwa shahidi wa mwisho tarehe 27 Januari 1887.
Habari za kuuawa kwake hazijulikani kwa uhakika. Hakuna aliyeshuhudia kuuawa kwake. Ilisimuliwa tu na wale waliokuwa wakitumikia katika mji wa katikiro Mukasa. Waliomsimulia Padre Mapeera walimwambia kuwa kabla ya kuuawa kwake, Yohana Maria Muzeeyi aliteswa sana. Walimpiga kwa fimbo hatimaye wakamnyonga hadi kufa. Halafu mwili wake waliutupa katika Bwawa. Wengine walimwambia kuwa Yohana Maria Muzeeyi alitupwa bwawani akiwa hai, hivyo alikufa maji. Mathia Kasi, yeye anasimulia kwamba, watumishi wa Katikiro walimweleza kuwa Yohana Maria Muzeeyi kwanza alikatwa kichwa na kiwiliwili chake kikatupwa katika Bwawa. Ludovick Masimbi anaeleza kuwa siku tatu baada ya kifo cha Yohana Maria Muzeeyi, kijakazi aliyekuwa akikaa katika nyumba ya katikiro Mukasa (ambaye zamani alikuwa mke wake Kabaka Mutesa I na alimfahamau Yohana Maria Muzeeyi) alimwambia kuwa rafiki yenu wamemkata kichwa na kukitupa kiwiliwili chake kwenye bwawa. Baadhi ya watumishi wa katikiro walisimulia kuwa walipoenda kuchota maji katika mto Jjugula walisikia harufu kali. Walipowauliza vijakazi walielezwa kuwa kule chini kuna maiti. Ndipo Simeo Nssubuga pamoja na wakristo wengine walipoenda kuiangalia maiti na kutambua kuwa ni mwili wa Yohana Maria Muzeeyi. Naye Padre Lourdel katika kumbukumbu zake za kila siku, tarehe 22 Februari 1887 ameandika: "Wanasimulia kuwa Yohana Maria Muzeeyi ameuawa. Aliyemwua ni Waswa Katembe. Lakini sina uhakika. Pengine ameuawa mtu mwigine na akadhaniwa kuwa ni Yohana Maria Muzeeyi." Kwa vyovyote vile Yohana Maria Muzeeyi alikufa shahidi. Ndiyo maana hata Kanisa Katoliki la Roma limemweka katika orodha ya watakatifu Mashahidi waliouawa kwa ajili ya dini huko Uganda. Baada ya kifo cha Yohana Maria Muzeeyi Padre Lourdel alipeleka tasbihi yake na kuitundika ukutani karibu na sanamu ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Basi siku moja, tarehe 12 Julai 1887, Kabaka Mwanga alikwenda kuwajulia hali mapadre na kuona hiyo tasbihi. Ndipo alipoigusa na kumwambia Kawuta aliyekuwa amefuatana naye, "Angalia hirizi za wazungu!" naye Kawuta akamjibu, "Ndiyo naziona." Kabaka Mwanga alikuwa anaenda kwa mapadre, mara kwa mara hasa baada kumwua Muzeeyi. Kila alipokuwa anaiona tasbihi hiyo alikuwa akijawa na wasiwasi mwingi sana. atifu
Mnamo mwezi Mei 1912, Baba Mtakatifu Pio X aliwatangaza vijana ishirini na wawili waliiofia dini yao huko Uganda kuwa watumishi wa Mungu, Venerabilis. Naye Papa Benedikto XV aliwatangaza wenye heri, Beati, tarehe 6 Juni 1920. Na tarehe 18 Oktoba 1964, katika mji wa Roma kwenye ibada maalum ya Jumapili ya Kueneza Injili, Baba Mtakatifu, Paulo VI, alitoa tamko rasmi na kusema: "Kwa heshima ya Utatu Mtakatifu, kwa kukomaza Imani Katoliki na kuimarisha ukristo kwa ujumla; kwa uwezo na mamlaka ya Bwana wetu Yesu Kristo, ya Mitume Petro na Paulo na yetu sisi, baada ya uchunguzi unaofaa na maombi mbalimblai kwa uongozi wa Aliye Juu, pamoja na ushauri katika utume: Makardinali, Mapatriarki, Maaskofu Wakuu na Maaskofu wa Kanisa Katoliki, tunawatangaza rasmi pamoja na kuwaandika katika Orodha ya Watakatifu: Mtakatifu Kalori Lwanga, Mathias Mulumba Kalemba na wenzao ishirini, kuwa ni watakatifu wa Mungu. Kwa hiyo tunaamuru kuwa Kanisa zima liwaheshimu kwa ibada maalum kila mwaka tarehe 3 Juni. Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Amina." Kati ya majina ishirini na mbili ya Watakatifu Mashahidi wa Uganda, limo pia jina la Yohana Maria Muzeeyi.
Mtakatifu Yohana Maria Muzeyi anatupa mfano wa kutafuta ukweli katika imani na kumpa Mungu heshima anayostahili. Kila wakati alitafuta njia itakayomuunganisha na Mungu zaidi na zaidi. Ndiyo maana alianza na dini ya jadi ya wazazi wake; baadaye Uislamu na kisha Uprotestanti. Lakini zote hizi hazikukidhi haja yake. Hatimaye alijiunga na Ukatoliki na humo alidumu na kutulia hata akautoa uahai wake kwa ajili ya kutetea heshima ya Mungu aliyemtumaini. Aliieneza na kuikomaza dini katoliki kwa njia ya mafundisho ya katekisimu ambayo yeye alifanikiwa kuyafahamu haraka kwa mang'amuzi ya ajabu. Aliamua kuishi maisha ya useja ili amtukimie Mungu kwa moyo usiogawanyika. Alitumia kipato chake kuwakomboa watumwa kiroho na kimwili, kwa njia ya ubatizo, huku akiwaweka huru. Hakusita kutumia mshahara wake kwa ajili ya wagonjwa aliokuwa akiwahudumia. Hakuwa na tamaa ya kujilimbikizia mali. Alizingatia sana fadhila ya utii. Hakufanya jambo lolote mahsusi bila kuomba kibali na kupata ushauri wa mapadre. Hata kabla ya kwenda kwa katikiro kukabili kifo-dini, kwanza alienda kuomba ruhusa ya Mapadre. Inasemekana alikufa akiwa shahidi wa mwisho kwa sababu mara nyingi mapadre walikuwa wamemshauri ajaribu kukwepa kwepa zile nafasi ambazo zingeweza kuhatarisha maisha yake. Alikazia sana maisha ya sakramenti. Wakati mapadre wakiwa uhamishoni Mwanza, aliwabatiza wakatekumeni wengi katika hatari ya kufa - japo kuwa yeye alikuwa bado mkatekumeni kwani alibatizwa baada ya mapadre kutoka Mwanza. Alifanya mipango pamoja na viongozi wenzake kuwapeleka waamini Mwanza ili waweze kupokea Sakamenti kama vile Kitubio, Komunyo, Kipaimara na Ndoa. Yeye binafsi kabla ya kwenda kwa Katikiro kukabili kifo, alihudhuria Misa na kupokea Ekaristi Takatifu. Muungano huo pamoja na Yesu wa Ekaristi, ulimpa nguvu ya kukabili kifo na mateso na hatimaye kuungana na Bwana wetu Yesu Kristu katika maisha ya mbinguni. Kwa kuzingatia karama zake, Baraza la Maaskofu wa Uganda limemfanya kuwa msimamizi wa: Watawa, Madaktari, Wauguzi, Hospitali na wanafunzi. Ni muhimu kwetu kuomba usimamizi na msaada wake.
Na Pd. Thomas R. KagumisaFor more information contact: The Parish Priest, Minziro Parish Cell: +255 787 157 393 E-mail: revoijumba@yahoo.com