Ni Kwaresima
"Tuongoke, Tutubu na Kufanya Kazi. Kuweni na Huruma kama Baba yenu wa Mbinguni alivyo na Huruma"
Mwaka huu tunaadhimisha Kwaresma katika Mwaka wa jubilei ya 'Huruma ya Mungu". Hivyo tunaalikwa kupokea huruma ya Mungu ambaye yuko anatungoja kama baba angojavyo mwanaye arudi. Turudi kwa Baba yetu aliye mbinguni.
Tutambue kwamba sisi ni wadhambi na hapo hapo tuombe msamaha kwa Bwana tukiahidi kweli kwamba hatutatenda dhambi tena. Tuongoke tuwe watu wapya. Baba Mtakatifu katika kutangaza mwaka wa Jubilei ya Huruma ya Mungu alisema: "Kanisa ni nyumba ya huruma ya Mungu inayowapokea na kuwakumbatia wote; watakatifu na wadhambi wanaotambua mapungufu yao na wako tayari kukimbilia huruma na upendo wa Mungu. kwa njia ya upendo, Yesu anaponya na kukanya mioyo iliyopondeka na kuvunjika kutokana na dhambi". Kwa maneno hayo Kanisa limejipanga kusaidia kila mtu kutubu, kupata rehema na kurudi kwa Bwana. Kwa hiyo hasa katika kipindi cha Kwaresma tunategemewa kufanya yafuatayo:
- Baada ya kutubu twende kuungama ili tuondolewe dhambi zetu na Bwana Mungu ambaye si mwepesi wa hasira bali mwingi wa huruma atutakase tuwe wapya.
- Tudumu katika sala, sala binafsi, tusali katika familia zetu, katika Jumuiya Ndogo Ndogo na makanisani. Tuwe watu wa sala.
- Kama tuna vikwazo katika maisha yetu yawe ni ndoa, uchumba sugu na mengine twende kwa padre atupe ushauri namna ya kutatua tatizo letu.
- Kwaresma ni wakati wa kujitoa sadaka, kufunga na kujinyima. Kufunga na kujinyimani kunyenyekesha miili yetu ili iwe imara katika kushinda vishawishi. Tunajinyima ili kile tunachojinyima kisaidie maskini na wenye shida.Huu ni wakati wa kushinda desturi mbaya kama ulevi, ulafi, na anasa mbali mbali. Wakati wa Kwaresma ni wakati wa saumu ya Bwana.
- Tupatapo fursa twende hija katika sehemu mbali mbali zilizopangwa jimboni hata nje ya jimbo. Kila dekania ina kanisa la hija, kuna vituo vya hija kijimbo kama Nyakijoga, Kishomberwa na kituo cha msalaba wa jubilei Bunena. Tukiwa tumejitayarisha katika hija tunapata rehema kamili.
- Kushiriki mahubiri mbali mbali katika parokia, vyama vya kitume na jumuiya ndogo ndogo.
- Tusaidie kueneza habari njema ya Neno la Mungu kila mmoja kwa namna anayoweza, kwenda wewe mwenyewe kuhubiri Neno la Mungu, au kusaidia kwa hali na mali na kuwatia moyo wale wote wanaofanya kazi hiyo.
- Kufanya matendo mema siyo tu kutoa fedha na vitu lakini kutoa muda wako kutembelea wazee, wagonjwa, maskini, wasiojiweza, yatima na wajane. Vile vile kuwasaidia kadiri unavyoweza kwa hali na mali. Bwana anasema nilikuwa na njaa ukanilisha, mgonjwa ukaja kunitazama.
- Mtakatifu Paulo anatuambia kwamba asiyefanya kazi asile hivyo katika kipindi cha Kwaresma tufanye kazi zaidi kama sehemu ya kutimiza wajibu wetu.
Nawatakia Kwaresma njema katika mwaka huu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu, tupate neema zitakazotuimarisha sisi, familia na jumuiya zetu.
+Method Kilaini (Askofu Msaidizi Jimbo la Bukoba)
|