Header
rumuli

ISSN 0865-6941

Toleo Na. 307

Machi 2016

Njia nzuri ya kujikinga na Radi


Na Prof. Kamazima Lwiza Profesa wa Fizikia ya Anga, New York, Marekani
Mwanachama wa FOB na BUDEFO


Mtaalamu wetu juu ya Fizikia ya Anga hapa anatujuza na huku akitutahadharisha kuhusu namna nzuri ya kuchukua tahadhari wakati hali ya hewa inapotubadilikia na kuwa ni mawingu, mvua na radi.

Ni busara kwa wanafunzi na hata watu wengine kuyazingatia mawaidha haya ya kisayansi na ambayo kamwe hayazingatii mambo ya imani za watu juu ya RADI na mtikisiko wake.

Pigo moja la radi linakadiriwa kuwa na Volt 125,000,000 za umeme. Kwa sasa hakuna njia kamili ya kujikinga na maafa ya radi isipokuwa kuna njia za kupunguza maafa kama ifuatavyo:

Ukiwa ndani ya nyumba ukaanza kuona dalili za mvua ya radi usitoke nje. Wala usiharakishe kutoka nje baada ya dhoruba – subiri ipite nusu saa baada ya ngurumo ya mwisho. Vifo vingi vya radi hutokea dakika chache baada ya dhoruba kupita.

Ukiwa nje ukaanza kuona dalili za mvua ya radi usingoje mvua ianze kunyesha – tafuta sehemu mahali hususani jengo lenye kuta na paa (k.m. nyumba, kanisa, msikiti, duka, n.k.). lakini siyo kioski, au veranda. Kama hakuna jengo ingia kwenye gari au basi lakini hakikisha hugusi sehemu yoyote yenye chuma.

Usijikinge mvua chini ya mti au karibu na maji (ziwa au bwawa). Miti na maji hupitisha (conduct) umeme wa radi kwa urahisi. Sehemu nyingine za hatari ni nyika na viwanja vya michezo, kilele cha mlima, au mgongo wa mlima, mbele ya pango.

Kama ukikumbwa na dhoruba na huna pa kukimbilia itabidi uchuchumae miguu yako ikutanishe pamoja (kwa sababu umeme wa radi huwa unaingilia mguu mmoja na kutokea kwenye mwingine – huongeza athari), na pia inamisha kichwa kwenye magoti. Kamwe usilale chini kwenye ardhi, kwa sababu radi ikiisha piga huwa inasambaa kupitia ardhini na kama umelala chini umeme utapita mwilini mwako.

Ukiwa ndani ya nyumba usitumie simu ya waya – tumia ya mkononi. Usiguse mabomba ya jikoni wala bafuni. Chomoa TV (kuzima switch peke yake haitoshi na vifaa vingine kama air conditioner, kompyuta, n.k.).

Kama una mwenzako akipigwa na radi, na huduma ya ambulance ipo wapigie simu mara moja, au tafuta njia nyingine ya kumfikisha hospitalini. Na unaweza kumshika anakuwa hana umeme ila ni vyema kumtafutia msaada wa kumpeleka hospitali haraka iwezekanavyo.

Radi ikikukuta ziwani mambo sio mazuri. Ni vema kupiga makasia haraka sana kurudi ufukweni na kutafuta mahali pa kujikinga. Kama uko mbali na huwezi kufika pwani kama ni mtumbwi una sehemu ya kujisetiri ingia haraka bila hivyo kama ni ngalawa ya kawaida chuchumaa chini (usilale chini) na hakikisha hugusi maji.

Kanuni ya thelathini – kwa – thelathini:
Ukiona miali ya radi anza kuhesabu sekunde mpaka utakaposikia ngurumo. Muda ukiwa chini ya sekunde 30 basi ujue dhoruba iko karibu sana nawe. Ina maana huna muda wa kutafuta mahali pa kujisetiri – chuchumaa na kutanisha miguu yako.

Hadithi za uongo – na – kweli (nyingi sio za kweli)

  1. Vitu virefu vilivyochongoka vinapigwa na radi kwa urahisi – kweli. Watu wawili wakiwa wamesimama karibu na kuna radi, aliyebeba mwavuli hata kama ni wa plastiki atapigwa na radi kabla ya mwenzie.

  2. Ukiwa umebeba chuma ni rahisi kupigwa na radi – Uongo ilimradi chuma hicho kisikuzidi urefu kichwani hakivuti radi.

  3. Viatu vya mpira au plastiki na koti la mvua vinaweza kukulinda na radi – Uongo

  4. Nguo nyekundu inavuta radi – Uongo

  5. Mtu akipigwa na radi lazima afe – Uongo

  6. Miti mirefu inaweza kukusetiri na radi – Uongo Kama inabidi uwe karibu na mti kwa sababu uko nyikani au msituni basi hakikisha unachuchumaa zaidi ya mita 2 kutoka kwenye mti.

  7. Kwenye jengo, mnara au mti mrefu kuna eneo la nyuzi 45 kutoka kwenye ncha ya juu ambayo unaweza kujisetiri – Kweli Lakini mti, au jengo linapozidi mita 30 hiyo kanuni haifanyi kazi.

Jipatie Nakala Yako
Anuani:
Rumuli Printing Press
P. O. Box Private Bag, Bukoba
Cell:+255784-440 159 au +255768 - 761 270
Fax:2222113
E-mail: rumulipaper@hotmail.com

Contact Information
Bishop's House Ntungamo,
P.O.Box Private Bag,
Bukoba, Tanzania.
Tel. & Fax. 028 - 2220746
Office: Tel. 028 - 2220194
E-mail: b.officebk@yahoo.com
Website: www.bukobadiocese.co.tz
© Bukoba Catholic Diocese 2023
Find us on
Facebook: Bukoba Catholic Diocese
Twitter:  @bcdcatholic