Header
rumuli

ISSN 0865-6941

Toleo Na. 307

Machi 2016

Kuviringisha Jiwe ni Tendo la Huruma


Na Pd. Faustin Kamugisha

Ni nani atakayevingirisha lile jiwe? Ni swali tunalojiuliza kila mara katika maisha yetu. Barabara ya maisha ambayo haina mawe ya kuviringisha haiendi popote. Ni nani atakayevingirisha lile jiwe? Mungu ana jibu. Tunasoma hivi katika Injili ya Marko: "Wakasemezana wao kwa wao. Ni nani atakayevingirisha lile jiwe mlangoni pa kaburi? Hata walipotazama, waliona ya kuwa lile jiwe limekwisha kuviringishwa; nalo lilikuwa kubwa mno" (Marko 16: 3-4).

Kuna mtoto wa miaka saba aliyejaribu kunyanyua jiwe akashindwa. Baba yake alikuwa amemtazama anavyohangaika kunyanyua jiwe. Alimwambia, "Tumia nguvu zako zote." Mtoto alijibu, "Baba nimetumia nguvu zangu zote." Baba alirudia kusema, "Tumia nguvu zako zote." Mtoto alijibu, ""Baba nimetumia nguvu zangu zote, nimeshindwa kulinyanyua." Baba alimwambia, "Hujatumia nguvu zako zote kwa vile hujaomba nikusaidie kunyanyua." Mungu anaweza kukusaidia kuviringisha jiwe.

Katika maisha yetu Mungu Baba mwenye huruma anatuma malaika wa kuviringisha mawe makubwa katika maisha yetu. Alimtuma malaika wa ufufuko kuviringisha jiwe kutoka kaburini. Peter Marshall (1902-1949) mhubiri wa kiamerika alisema, "Jiwe liliondolewa kutoka mlango wa kaburi, si kumruhusu Yesu atoke bali kuwawezesha mitume waweze kuingia." Tunasoma hivi: "Akainama na kuchungulia akaviona vitambaa vya sanda vimelala; lakini hakuingia. Basi akaja na Simoni Petro akimfuata, akaingia ndani ya kaburi; akavitazama vitambaa vilivyolala; na ile leso iliyokuwako kichwani pake" (Yohane 20: 5-7). Mtume Yohane aliweza kuchungulia ndani kwa vile jiwe lilikuwa limeviringishwa. Mtume Petro aliweza kuingia ndani kwa vile jiwe lilikuwa limeviringishwa.

Tunasoma katika Injili ya Luka kuwa "Wakalikuta lile jiwe limeviringishwa mbali na kaburi" (Luka 24:2). Hao walikuwa ni Maria Magdalene na Yoana na Maria mamaye Yakobo. Malaika wa ufufuko aliviringisha jiwe. "Na tazama, palikuwa na tetemeko kubwa la nchi; kwa sababu malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akaja akaliviringisha lile jiwe akalikalia" (Mathayo 28:2). "Jiwe liliviringishwa baada ya ufufuko kwa ajili ya wanawake, ili waweze kuamini kuwa Bwana amefufuka, kwa kuona kaburi bila mwili," alisema Mtakatifu Yohane Kyrisostomu

JIWE LA KIFO LIMEVIRINGISHWA
Kwa kuondoa jiwe kaburi la Yesu lilibaki mlango wazi kuonesha kuwa kaburi si gereza tena kuna kufufuka. Kifo si nukta bali ni alama ya mkato. Meli ikianza safari yake toka Kisumu hadi Mwanza Tanzania wale walioko Kisumu wanasema meli imeenda. Wale walioko Tanzania wanaoiona kwa mbali wanasema meli imekuja. Mtu akiaga dunia tunasema "Ameenda." Walioko mbinguni au toharani wanasema, "Amekuja." Hivyo kifo sio kituo bali ni koma. Kwa vile jiwe la kifo limeviringishwa KWETU KIFO SIO UKUTA NI MLANGO. Kwetu kifo sio kizuizi bali ni daraja.

Mbio za sakafuni huishia ukingoni. Mbio zetu haziishii ukutani bali tunapitia zinafika mlangoni na tunapita. Hadithi ikiwa nzuri sana kwenye gazeti inakatizwa na chini yake yanaandikwa maneno itaendelea toleo lijalo. Toleo Lijalo ni, mbinguni, toharani au motoni.Kuna refa aliyeaga dunia akaenda motoni. Huko alikuta uwanja mzuri sana na watu wamejipanga kucheza mpira alifurahi sana. Timu mbili ziliingia yeye akashika kipenga. Wachezaji wakasalimiana na kushika nafasi zao. Yeye refa akaulizia mpira wapi. Aliambiwa huku ndio maana kunaitwa motoni. "The hell of it" ni kwamba hakuna mpira. Huna hamu ya chakula na hauwezi ukala. Kuna kitu kinakosekana.

JIWE LILILOVIRINGISHWA LINA UJUMBE WA HURUMA
Kwa kawaida mawe ya kaburini (tombstones) huwa na ujumbe. Ujumbe wa jiwe hili baada ya ufufuko ni kwa wafu ni huu: "Mlivyo ndivyo nilivyokuwa. Nilivyo ndivyo mtakavyokuwa." Ni ujumbe wa matumaini ya kufufuka. Ni ujumbe wa huruma. Ni matumaini yasiyo na mwisho. Ijumaa Kuu ujumbe huu kwa walio hai ulikuwa, "Mlivyo ndivyo nilivyokuwa. Nilivyo ndivyo mtakavyokuwa," ulikuwa ni mwisho wa matumaini. Katika tamaduni za kiafrika mtu akiwa anaomboleza anamwambia marehemu amsalimie jamaa zake walioaga dunia. Anasema: Nisalimie babu yangu, nisalimie nyanya yangu. Nisalimie mjomba wangu. Nisalimie mama mdogo. Mfano wa majina: immortality of name: mjukuu anapewa jina la babu. Mtoto wa kike anapewa jina la nyanya yake. Tunataka jina la mtu liendelee kutajwa. Immortality of fame: Tunataka sifa ya mtu iishi milele. Tunajenga sanamu za ukumbusho. Kuna immortality of influence: Jina la baba linawapa watoto ushawishi. Immortality of power: Tunataka mamlaka yaendelee kwa kuanzisha mashirika ya kutoa msaada mfano Nyerere Foundation au mfano wa aliyeanzisha zawadi ya Nobel Prize.

JIWE LILILOVIRINGISHWA NA KUKALIWA NA MALAIKA LINATOA UJUMBE WA KUPUMZIKA.
"Na tazama, palikuwa na tetemeko kubwa la nchi; kwa sababu malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akaja akaliviringisha lile jiwe akalikalia" (Mathayo 28:2). Kukaa ni kupumzika. Kukaa kwake kunaongea kuwa kazi imemalizika. Ni siku ya Bwana. Ni siku ya kupumzika. Lakini si kupumzika katika kutenda matendo ya huruma. Kuhubiri ni kutenda tendo la huruma. Malaika huyu ingawa alipumzika alihubiri. "Malaika akajibu akawaambia wale wanawake, Msiogope ninyi; kwa maana najua ya kuwa mnamtafuta Yesu aliyesulubiwa. Hayupo hapa; kwani amefufuka kama alivyosema. Hayupo hapa; kwani amefufuka kama alivyosema. Njoni mpatazame mahali alipolazwa. Nanyi ndeni upesi, mkawaambie wanafunzi wake, Amefufuka katika wafu" (Mathayo 28: 5-7). Wanawake wanahubiriwa na kualikwa kuamini, kushirikisha wengine na kufurahi. Kupumzika Jumapili hakuna maana tunapumzika katika kutenda matendo ya huruma. Ni Jumapili hiyo elimu dini inafundishwa kwa watoto kwenye Sunday School.

YESU ANAVIRINGISHA JIWE LA DHAMBI
Yesu ataliviringisha hilo jiwe. "Mtu yeyote asiomboleze kuwa ameanguka tena na tena; kwa vile msamaha umefufuka kutoka kaburini – Mt. Yohane Chrysostom. Yesu anaondoa jiwe la dhambi.

Hitimisho
Katika maisha ya kila siku tufanye utume wa malaika wa ufufuko wa kuondoa mawe: mawe ya shukrani ya punda, mawe ya kukata tamaa, mawe ya chuki, mawe ya kujilinganisha na wengine, mawe ya kukufuru, mawe ya kutosamehe, mawe ya nia mbaya, mawe ya roho ya tuharibikiwe sote, mawe ya kukatisha tamaa, mawe ya msongo wa mawazo kutaja machache.

Itaendelea toleo lijalo

Jipatie Nakala Yako
Anuani:
Rumuli Printing Press
P. O. Box Private Bag, Bukoba
Cell:+255784-440 159 au +255768 - 761 270
Fax:2222113
E-mail: rumulipaper@hotmail.com

Contact Information
Bishop's House Ntungamo,
P.O.Box Private Bag,
Bukoba, Tanzania.
Tel. & Fax. 028 - 2220746
Office: Tel. 028 - 2220194
E-mail: b.officebk@yahoo.com
Website: www.bukobadiocese.co.tz
© Bukoba Catholic Diocese 2023
Find us on
Facebook: Bukoba Catholic Diocese
Twitter:  @bcdcatholic