ISSN 0865-6941 | Toleo Na. 307 | Machi 2016 | |
Maoni ya MhaririMpendwa msomaji wetu wa RUMULI, Tumsifu Yesu Kristo! Kheri ya Pasaka! Pasaka hii iwe ya baraka kwako, Kristo Mfufuka aendelee kukunyanyua na kukujalia uzima, furaha, amani, upendo, na huruma yake. Tunazidi kuwashukuru sana wanahabari wetu na waandishi wa makala mbali mbali katika gazeti letu. Mungu azidi kuwabariki na kuwalinda. Tunazidi kuwakaribisha na wengine na makala mbalimbali ili tuzidi kuielimisha jamii kwa kulitumia jukwaa hili la gazeti Rumuli. Tuzidi kuichangamkia fursa hii: tuongee kwa njia ya kalamu kupitia Rumuli. Ndugu msomaji tunapenda kukufahamisha kwamba kuanzia toleo hili tumeanza kuwa na makala endelevu (ya mwendelezo) yatakayokuwa yanatoka kila toleo. Tayari waandishi wetu mahiri wamejitokeza na kuanza mara moja kuandika makala hizi (endelevu). Kwa nafasi hii tunawashukuru sana Maaskofu wetu : Mhashamu Baba Askofu Desiderius M. Rwoma anayetulisha neno lake la kichungaji kila mara kupitia gazeti lake hili la Rumuli, na sasa katika toleo hili ametualika tuwe wapya – tupyaishwe na Ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo, huku akimulika mwanga katika nyanja za mafundisho ya imani, maadili, misingi imara ya uongozi, haki, huruma, nk kama njia pekee ya kuzuia kuota kwa majipu; na Mhashamu Baba Askofu Methodius Kilaini kwa kutulisha neno lake la kibaba kupitia gazeti hili sauti ya Jimbo. Ndugu msomaji, katika toleo hili Baba Askofu Kilaini amependa kukujuza historia ya Kagera na watu wake; ni machimbuko makini na yanayovutia sana, bila shaka utaipenda makala yake hii endelevu. Mababa tunawashukuru sana kwa kuielimisha jamii. Katika mwendelezo huu wa shukurani kwa makala endelevu, tunamshukuru Mzee Enock L. Kamuzora, mwandishi aliyebobea, kwa utayari wake wa kuandika makala endelevu. Yeye kama mwandishi makini ameonelea aongelee juu ya umoja wa Marafiki wa Bukoba (FoB) ili aendelee kuwavuta wana Kagera walioko nje na ndani ya Kagera kupaendeleza nyumbani kama shukurani kwa Mungu na jamii nzima ya Kagera kwa kuwawezesha na kuchangia kwa namna moja au nyingine kuwafanya jinsi walivyo. Ndugu msomaji endelea kujipatia nakala za Rumuli kila mwezi na wahamasishe wengine kupata nakala zetu ili usipitwe na elimu hii.<>
Tunamshukuru pia Mhe. Pd. Faustin Kamugisha (Kanyanya) kwa kujitolea kuwa mwandishi wa makala endelevu, akiangaza katika Mwaka wa Huruma. Baba tunasema ahsante sana. Tunazidi kuwakaribisha wengine wengi kuandika makala za kawaida na makala endelevu zitakazokuwa zinatolewa kila mwezi. Pia tunahimiza utafiti uendelee kufanyika katika jamii yetu ili kile kinachoongelewa kiakisi uhalisia wa jamii yenyewe na hivyo kuibadilisha ili ijifananishe na Kristo zaidi na zaidi, na tuufikie wakati ambapo kila mmoja wetu atajiambia haya: "Kusudi la maisha yangu ni kumwabudu Mungu kwa moyo wangu wote, kumtumikia kwa umbo langu, nishiriki na jamii yake, nikue katika mfano wake kitabia, na kutimiza utume wake duniani ili Yeye apokee utukufu"; na kama Sulemani Mfalme asemavyo, "kwa kuwa utaona furaha ukiyatunza moyoni, na kuyapata tayari midomoni pako daima" (Mith 22:18). |