Header

Masista Batereza Bukoba: Alivyowakirimu

Batereza

Shirika la Masista wa Mtakatifu Teresa wa Mtoto Yesu - Bukoba (Batereza)

Kardinali Rugambwa alituonyesha upendo wa baba, akituonya kwa uwazi na upendo, akituasa tujitahidi kulinda heshima yetu Bathereza .
Na Sr. Caritas Kokuteta; Mama Mkuu Batereza, Bukoba

Mwadhama alikuwa kweli Mwana - Kanisa aliyejitoa kwa moyo wake wote kwa ajili ya kumtumikia Kristu bila ya kujitafuta. Upendo wake kwa Kristu na Kanisa lake ulimsukuma kufanya yale aliyoweza kufanya kwa ajili ya maendeleo ya watu kiroho na kimwili.


Maisha ya Kiroho

Alikuwa mtu wa kumtegemea Mungu katika maisha yake, mwenye imani dhabiti. Alikuwa mtu wa sala, hivyo katika ratiba zake sala alizipa kipaumbele. Alisali kwa ibada, aliamka saa 11.00 alfajiri kwa ajili ya kusali Breviari, Rozari, Meditasio na Misa Takatifu. Kila siku kuanzia saa 11.00 jioni ulikuwa muda uliotengwa rasmi kwa ajili ya tafakari yake ya jioni, kusali Breviari, Rozari, na Maonano. Ilikuwa siyo rahisi kumtembelea muda huo wa saa za jioni labda kama mtu alikuwa na shida maalum na amemuomba kufika kwa muda huo.

Kila alipo ingia ofisini alianza kusali, kumkaribisha Roho Mtakatifu amwongoze katika majukumu yake ya kulichunga taifa la Mungu. Alikuwa na upendo mkubwa kwa Bikira Maria, alitumainia sana ulinzi wake. Ofisini mwake alikuwa amesimika sanamu ya Bikira Maria, mara kwa mara aliomba ulinzi na ushauri wake – Mama wa Shauri Jema. Alikuwa na Goroto Ndogo ya Bikira Maria kwenye uwanja wa nyumba yake alikuwa anaenda pale kusali rozari. Ibada ya Bikira Maria ilimsukuma kutoa ruhusa ya kusali Rozari ya mateso katika jumuiya za Waumuni na pia kuanzishwa Chama cha Bikira Maria wa Mateso. Alipokuwa Askofu wa Jimbo la Rutabo alianzisha kituo cha mahujaji hapo Nyakijoga, Mugana, iwe ndiyo Ludi ya Africa. Mpaka leo waumini humiminika kila mwaka kwa kuhiji kwa Mama yetu Bikira Maria hapo Nyakijoga. Imani kwa Mama wa Mungu imeimarishwa kati ya watu.

Alikuwa na kipaji cha kuongoza Ibada Takatifu vizuri sana na kuwavutia watu wengi kusali. Alipenda vifaa vya ibada viwe safi, kanisa na mazingira yake na nguo za kanisani. Alikuwa msafi kwa ujumla na alipenda mazingira yawe safi, nje na ndani. Maua ya kupamba kanisani aliyapa kipaumbele, alipokuwa safari kama angeona ua zuri aliliomba kulileta kwa Masista ili walipande kwenye bustani baadaye liweze kuwa linapambwa kanisani. Kamwe hakuruhusu maua ya bandia yapambwe kanisani, alikuwa akiyaona aliomba yatolewe haraka. Alikuwa mnyenyekevu na kujiweka kama mtu wa kawaida.


Utume

Katika kazi zake alizingatia na kuheshimu muda uliopangwa kwa kuwahi Ofisini, kurudi nyumbani, kwenda Parokiani katika shughuli za kichungaji au popote alipokuwa na wajibu wa kutoa huduma au kuhudhuria mikutano. Mfano alikuwa anaondoka Oysterbay saa 12.45 ili aweze kufika St. Joseph saa 1.00 asubuhi na kuondoka saa 5.30 kurudi nyumbani. Muda huo ulizingatiwa labda kama kulitotea shida fulani. Alipomwita mtu kwake alisisitiza kuwahi kwa muda aliompangia, iwapo alichelewa kidogo alikuta ameishaondoka na kwenda kanisani kwa sala za binafsi.

Alipenda kufanya kazi kwa uhusiano mwema na wadau wake. Alidumisha uhusiano mwema na serikali na watu wa madhehebu mengine. Kila mmoja alimpa nafasi yake kama alivyostahili. Hakupenda mabishano na malumbano, uamzi wake ulikuwa wazi na wenye busara. Mwadhama Kardinal Laurian Rugambwa alikuwa na upendo kwa watu wote hasa wenye shida mbali mbali. Aliwafariji wafiwa na wagonjwa kwa maneno yake na misaada aliyoweza kuwatolea. Alikuwa Baba anayependa jumuiya ya wale alioishi nao, yaani masista waliokuwa wanamuhudumia. Aliwashauri na kuwaelekeza kwa upendo yale aliyotaka yatekelezwe.

Alikuwa na upendo kwa watu, aliwakaribisha wamtembelee nyumbani kwake na aliwapokea kwa moyo mkunjufu. Hakukosa kuwa na kahawa au senene za kuwapa wageni waliofika kumtembelea, alikuwa mkarimu. Alikuwa mcheshi akipiga soga na watu wa rika mbali mbali na vyeo. Alikuwa tayari kuuliza au kupokea ushauri kwa yeyote aliyekuwa na imani naye. Alikuwa wazi na mtiifu. Katika utume wake alipenda maendeleo ya Mapadre na Walei kielimu, amewatafutia wengi wao misaada ya kwenda kwenye vyuo mbali mbali ili Elimu yao iweze kusaidia katika kulitegemeza Kanisa. Hii pia ilimsukuma kuanzisha mashule kwa manufaa ya jamii yetu.

Alihimiza Mapadre na Watawa kuvaa kwa heshima kulinda hadhi yao. Alipotembelea Parokia na Konventi za watawa, alikuwa na nia ya kujionea hali halisi ya mazingira na kushauri lipi lifanyike. Alikaribisha mashirika mbali mbali ya Kiume na Kike, ili kufanya kazi katika jimbo lake. Alitaka wasaidiane katika kuimarisha imani ya waamini, na kutoa huduma katika nyanja mbali mbali kufuatana na karama za mashirika hayo, kwa kadri ya mahitaji ya nyakati hizo. Mwadhama Kardinali Laurean Rugambwa alikuwa mtendaji kazi hodari na alijipa nafasi ya kufanya mazoezi ya viungo, hivyo aliendesha gari lake mwenyewe mpaka hapo alipoishiwa na nguvu, njiani watu walimheshimu na mara nyingi walimpisha ili apite kwanza.


Uhusiano wa Kardinali Rugambwa na Shirika la Batereza

Mwadhama Kardinali Laurean Rugabwa akiwa ni mzawa wa Jimbo la Bukoba amekuwa na uhusiano wa karibu tangu akiwa Frater mpaka kuwekwa wakfu kwa Sakrament ya Daraja la Upadre – Uaskofu na Ukardinali. Ameishi na kufanya kazi mahali ambapo Masista Bathereza wamekuwa wanatoa huduma yao kwa kazi za kitume. Tangu mwanzo ametegemezana nao katika wito na utume katika kanisa.

Batereza

Alipoteuliwa kuwa Askofu wa Jimbo la Bukoba na kusimamia Shirika la Bathereza lenye hadhi ya Kijimbo, alilishughulikia ili lijitawale. Mlezi Mkuu wa Shirika alikuwa ametoka kwenye shirika la Masista Wamisionari wa Bikira Maria wa Afrika ( White Sisters ) na Chaplain akiwa ni kutoka Wamissionari wa Africa ( White fathers ). Aliwaagiza kuandaa Masista ili waweze kufanya Mkutano wa Mkuu wa Kwanza. Tarehe 28/10/1961 Shirika lilichagua Mama Mkuu wa kwanza na Washauri wake, yeye akiwa Mwenyekiti wa Mkutano huo . Hali ya uchumi wa Shirika ilikuwa duni hivyo alijitahidi kuwasaidia viongozi kutafuta njia za kulitegemeza shirika. Aliwaombea Masista nafasi za masomo katika vyuo mbali mbali na kuwatuma nje ya nchi kwa ajili ya kuwaelimisha waweze kukabiliana na changamoto za nyakati. Alitushughulikia tupate vitendea kazi, mfano gari la kwanza la Shirika alilitoa kwa ajili ya Mama Mkuu.

Alishauri shirika tuanzishe Shule ya Msingi kwa ajili ya Makandidati ili kuchochea miito. Ni katika kipindi hiki Shirika la Bathereza tumepata watawa wengi ambao sasa ni nguzo katika shirika. Wakati huo Postulant na Novisiati vilikuwa sehemu moja kwa hiyo alituombea msaada wa fedha kuweza kujenga Novisiati. Alifanya upanuzi wa kanisa letu hapo Nyumba Mama Nyaigando kuwa la kisasa. Kwake tulikuwa wana ambao alitutakia maendeleo ya kiroho na kimwili. Alitukazania kuwa watu wa sala kwa kujali ratiba za sala na kusali kwa ibada. Kuwa na nidhamu ya kitawa, wenye kujibandua na mambo ya kiulimwengu. Maisha yake yote amekuwa karibu sana nasi akituonya kwa uwazi na upendo yale ambayo aliyaona hayaendi sawa au aliyoyasikia juu yetu. Nasi tulimpokea kama baba na mwana.

Alituamini katika utendaji wa kazi za kitume hata alipohamia Jimbo Kuu la Dar es Salaam alikaribisha shirika letu kufanya kazi huko, hapo Msimbazi Centre katika vitengo vyake vyote. Lilikuwa ni shirika la pili kwa Watawa wa Kike kuingia Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Mpaka hivi leo huduma hizo bado Bathereza tunaziendeleza na zinazidi kupanuka.

Batereza

Alipoanza kazi ya kuchukua Kiti cha Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Makatibu wake mahususi walikuwa Bathereza ambao ameendelea kufanya kazi nao mpaka Mungu alipomwita kwake. Alituamini kuweza kutuaminisha siri za Jimbo na kuzisetiri. Alituonyesha upendo wa baba akituasa tujitahidi kulinda heshima yetu Bathereza na heshima ya Jimbo la Bukoba. Alipenda huduma zetu zipanuke na kuwafikia watu wa nyanja zote kufuatana na mahitaji ya nyakati. Utume wetu tuliuendeleza kwa kutoa huduma ya Afya pale Ukonga. Mwanzoni ilikuwa Zahanati leo hii imefikia hatua ya kuwa Hospitali ijulikanayo kama Kardinali Rugabwa Hospital.

Alipenda shirika letu na kulitetea kwa kila hali, kwa mfano pale shirika lilipokumbwa na msukosuko wa kiuongozi (ulioitwa Kongamano la mwaka 1985), Mwadhama Kardinali Laurean Rugabwa, alikemea, alishauri, hakutulia mpaka hapo mambo yaliposawazishwa na kukawa shwari. Uchaguzi Mkuu ukaendelea kama ulivyopangwa, amani ikarudi shirikani. Katika afya yake alipenda Masista Bathereza wawe karibu naye. Afya yake ilipoanza kubadirika, aliomba Sista aliye Muuguzi kumsindikiza katika safari zake ili aweze kumhudumia. Sista Muuguzi Mthereza amekuwa karibu naye mpaka alipoitwa na Mwenyezi Mungu.

Daima katika maisha yake amejivunia shirika la Bathereza – msemo wake ulikuwa "Mtoto wa kwanza ni wa kwanza" huona mengi, hupendwa na kupokea mengi.

Baba yetu apumzuke kwa Amani
Sr. M. Caritas Kokuteta Mama MkuuBaba yetu Mwadhama Kardinali Rugambwa

Nilivyomfahamu: Alipenda Watawa wa Mashirika mbali mbali Wawe na Umoja.
Na Sr. Rita Ishengoma

Mapendo yake kwa Shirika Ia Mt. Theresia wa Mtoto Yesu

Batereza

Tukiwa Shirika Ia jimbo, Mwadhama alikuwa kwetu Baba. Alitupenda, alilipenda shirika letu; alituita "Bana-bange" (maanake watoto wangu). Mapendo yake yamesaidia shirika kujiamini katika kufanya kazi ya Umisionari nje ya jimbo letu. Alitupa moyo kila mara akisema "Mnaweza", "Hakuna anayewashinda"


Tabia yake nilivyomfahamu


Afya yake haikuwa nzuri, lakini hakupenda kusema. Alikuwa mtu wa kujitesa na mvumilivu. Kwa mtu asiyefahamu, ingekuwa vigumu kuishi naye. Utakosana naye upesi kwa sababu ingawa kitabia alikuwa mcheshi wa kutania lakini pia alijali sana muda na vitu kufanywa vizuri. Zawadi kwetu kama Shirika tulipata fursa ya kumuhudumia wakati wa saa zake za mwisho. Masista wetu Sr. Hilaria Mumusime, na Sr. Francis Borgia amefia mikononi mwao.

Apumzike kwa Amani- AMINA
Sr. Rita Ishengoma
Contact Information
Bishop's House Ntungamo,
P.O.Box Private Bag,
Bukoba, Tanzania.
Tel. & Fax. 028 - 2220746
Office: Tel. 028 - 2220194
E-mail: b.officebk@yahoo.com
Website: www.bukobadiocese.co.tz
© Bukoba Catholic Diocese 2023
Find us on
Facebook: Bukoba Catholic Diocese
Twitter:  @bcdcatholic