Mwanzoni mwa mwaka 1960 niliambiwa na mhudumu wa wakapuchini waholanzi nijitayarishe kwenda Tanganyika kuwa mmisionari wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam.
Mwaka ule ule Askofu Laurian Rugambwa alichaguliwa kuwa Kardinali. Katika kundi lake alikuwa pia Kardinali Alfrink wa Uholanzi. Nakumbuka kwamba TV ya nchi yangu (Uholanzi) ilionyesha ibada nzima ya kupewa Kofia ya Kikardinali. Walau Baba Mtakatifu Yohane wa XXIII alipoweka Kofia juu ya kichwa cha Kardinali Rugambwa watu katika Kanisa la Mtakatifu Petro walimshangilia sana kwa sababu alikuwa Kardinali wa kwanza kutoka Afrika. Wakati ule sikuweza kujua kwamba ningelikuja kukaa pamoja na Karidinali Rugambwa siku za mbeleni na kufanya kazi naye kwa muda mrefu.
Nilipokuwa katika parokia ya Mtakatifu Joseph tangu mwaka 1972 tulionana karibu kila siku kwa sababu ofisi yake ilikuwa katika gorofa ya pili ya nyumba yetu. Wakati ule tulikuwa huko Mtakatifu Joseph Wakapuchini wawili, Padre Novatus na mimi. Padre Novatus alipohamia Mbagala, nilibaki peke yangu kama padre Mkapuchini. Wakuu wangu walianza kusema ni vizuri zaidi nikae katika nyumba ya watawa na walijaribu kunihamisha kutoka Mtakatifu Joseph lakini Kardinali Rugambwa alipendekeza nibaki katika Kanisa Kuu Ia Mtakatifu Joseph. Kwa upande wangu nilifurahi. Kardinali Rugambwa alishirikiana vizuri na parokia yetu. Tulipojenga Kanisa dogo huko Keko Mwanga. Kardinali alikuwa tayari kubariki na watu walifurahi sana.
Wakati Kamati ya Walei ilipoweka ukumbusho wa Hayati Askofu Mkuu Edger Maranta katika Kanisa Kuu Ia Mtakatifu Joseph, Kardinali alisaidia kufanya ibada ya kumwombea Askofu Edger Maranta ambaye alikuwa mtangulizi wake katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Mara nyingi tulikuwa na ibada katika Kanisa Kuu ambazo ziliongozwa na Kardinali na alifurahi sana ikiwa mliweza kupiga picha na kuzikabidhi kwake kama ukumbusho ya kazi yake.
Nimeandika hapo juu kuhusu Kardinali Alfrink, ambaye alichaguliwa kuwa Kardinali wakati ule ule pamoja na Kardinali Rugambwa. Huyu Kardinali Alfrink alipokuwa padre kijana alikuwa paroko msaidizi katika parokia ya nyumhani, kijijini kwangu. Kwa hiyo aliifahamu familia yangu na kama mtoto niliwahi kutumikia misa alizoadhimisha katika kanisa la nyumbani. Kumbe wakati wa Conclave ya kumchagua Baba Mtakatifu Yohana Paulo II Kardinali Rugambwa alikaa pamoja na Kardinali Alfrink. lnaonekania waliongelea juu ya wamisionari wa Kiholanzi Tanzania, nami ni kiwa miongoni mwao. Basi Kardinali Alfrink aliandika barua fupi ya kunisalimia na alimkabidhi Kardinali Rugambwa, ambayo aliporudi kutoka Roma alinipatia. Nilifurahi sana kwa alama ya mapendo ya Makardinali hawa wawili.
Fr. Mansuetus OFM Cap
Mwadhama Rugambwa na Changamoto ya Miito ya Kichungaji Jimboni
Siku moja nikiwa katika Seminari Kuu ya Kipalapala nilibahatika kuyasikia mazungumzo kati ya askofu mmoja na mseminari mmoja. Muulizaji alikuwa marehemu Askofu Mkuu Mario Mgulunde, ebu tuyafuatilie mazungumzo yao: Wewe ni mseminari toka jimbo gani? Mimi ni mseminari wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Umekulia Dar es Salaam au ni mkimbizi tu? Hapana, nimezaliwa na kukulia Dar es Salaam. Ni kweli unachosema! Muuliza maswali usoni mwake kukukajawa na butwaa la kutoamini alichosikia! Mshangao huu wa watu mbalimbali juu ya uwezo wa vijana walikulia Dar es Salaam kuwa mapadri na watawa miaka ya nyuma ulikuwa na nguvu sana. Lakini taratibu kama samli katika jua la kiangazi ukaanza kuyeyuka.
Waseminari wazawa na wakulia wa Dar es Salaam, idadi yao siku kwa siku ilipokuwa ikiongozeka, na kuufikia upadri, na wasichana kuwa watawa ukweli mpya ulijifunua, kwamba jiji la Mzizima linauwezo wa kuwapata mapadri na watawa wake wenyewe. Jua hili la kiangazi liliyoyeyusha mshangao wa watu kuwa kweli kijana wa jijini anaweza kuwa padri ni Hayati Kardinali Rugambwa. Jimbo la Dar es Salaam kwa muda mrefu lilikuwa likitegemea wachungaji wamisionari toka nje ya nchi. Mapadri wazalendo waliokuwepo walikuwa walioanzimwa toka majimbo mengine, baadhi yao ni kama Pd. Alex Kiwori toka Moshi, Pd. C. Luoga, F. Nyoni, J. Mbunga na N. Maseko kutoka Songea, Pd F. Rweikiza, Sadoth Rweyemamu, W. Mutashambara, H. Kobukare kutoka Bukoba. Ukweli huu pia ulisadifu kwa watawa wa kike. Hali hii ilikuwa na mapungufu yake mengi. Mazingira ya Dar es Salaam yana upekee wake, hasa ukizingatia kwamba sehemu kubwa ya jimbo ni jiji. Watu ni wengi toka kona zote za nchi. Kuingia na kutoka kwa watu ni kukubwa sana kama vile maji katika Bwawa la Mtera. Changamoto za kichungaji za waamini na jirani zao ni tofauti sana na za majimbo mengine. Nakumbuka katika utafiti uliofanyika hivi karibuni kwa watoto wa Kipaimara, wao suala la ushirikina lilikuwa la mwisho, likipitwa na masuala mengine mfano UKIMWI, ujambazi, ukosefu wa shule za sekondari na amani katika kaya. Jimbo lina wingi wa madhhebu ya Kikristo, bila kusahau uwepo mkubwa wa Waislamu. Vyombo vya habari ni vingi na vuguvugu la mambo ya kisiasa ni kubwa. Utafutaji fedha ni jambo linalowakimbiza watu huku na kule kama mchwa! Hizi ni baadhi tu ya changamoto ambazo waamini wa jimbo letu wanakabiliana nazo, ambazo zinahitaji uzoefu wa kichungaji wa aina ya pekee. Jimbo lenye changamoto hizi zote za kichungaji, kwa miaka mingi likawa katika uhaba wa mapadri wenyeji. Ukiangalia takwimu za upadrisho ni sawa na uzazi wa majira wa kusikitisha sana: 1969 alipadrishwa Pd. C. Nyambo, 1972 Pd. J. Muba na Pd. D. Mbiku, L. Mdenkeri, 1981 Pd. C. Luambano na 1982 marehemu Pd. M. Gutambi na Pd. V. Tegete. Kwa miaka kumi na tatu mapadri saba tu, wakati mwaka 1994 na 1995 Kardinali Rugambwa alipadrisha mapadri wapya wanane. Mwono wa Kardinali Rugambwa toka aingie katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam, ni kuweza kujitegemea kichungaji. Jambo hili alilitekeleza kwa namna mbalimbali:
Kwa namna ya pekee aliimalisha ofisi ya mkurugenzi wa miito, mfano mzuri ni pale alipomteua Pd. Alex Kiwori na Pd. Joseph McCabe kuendesha shughuli za ofisi hiyo. Pd. Mara kwa mara alikuwa akipata nafasi ya kukaa pamoja na mafrateri na kuzungumza nao kama baba na wana wake. Andrea Mwekibindu, anakumbuka vizuri, jinsi gani wakati wa likizo Mwadhama Laurian alivyowakutanisha kwa semina mafrateli wote, hasa kwenye Kituo cha Kiroho Mbagala.
Alianzisha shirika la watawa wa kike la jimbo mwaka 1983, watawa wa kwanza waliweka nadhiri zao za kwanza 1987. Shirika hili lijulikalo kama Wadada Wadogo wa Mtakatifu Fransisko lilizinduliwa rasmi mwaka 1999 na Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo. Leo hii watawa hawa wanahudumia waamini katika parokia za Mbagala, Mt. Yosefu, Mt. Petro, parokia ya Roho Mtakatifu Segerea, Don Bosko Kibaha, Vikindu na katika asasi kadhaa za jimbo, ikiwa pamoja na ofisi za jimbo, shule ya Msingi ya Mt. Yosefu na Sekondari ya Mt. Anthoni Mbagala, shule ya sekondari High school) ya Mtakatifu Yosefu, bila kusahau wengi wao wanaohudmia wagonjwa na kutoa mafunzo ya katekesi. Huu ndio uchanuo wa ndoto za mwadhama ya kutaka jimbo lijitegemea kwa wachungaji wake.
Machipukizi huitaji maangalizi ya pekee katika siku zake za mwanzo. Ndio maana chini ya uongozi wake jimbo lilianzisha Seminari Ndogo ya Visiga mwaka 1990. Seminari hii imewekwa chini ya ulinzi wa Mama Bikira Maria, kama kitalu cha miito ya upadri kwa jimbo letu, ipo umbali wa km 50 toka katikati ya jiji, katika bararaba ya Morogoro.
Alianzisha Seminari Kuu ya Segerea jimboni. Iwe kama changamoto kwa wazazi na vijana wa jimbo, kwani wahenga walisema penye miti mingi hapana wajenzi. Changamoto kwetu ilikuwa sasa kwa kupitia seminari hii, tuwe na ujenzi wa maisha ya vijana wetu yatakayowasaidia kuweza kwenda kujifunza hapo.
Frendinand Mazuni, anakumbuka vizuri alipokuwa kidato cha kwanza katika Seminari ya Maria Visiga, jinsi gani Kardinali Rugambwa alivyokuwa akiwatia moyo. Alimithilisha wito wa upadri na ugumu uliokuwepo katika kuanzisha seminari hiyo, aidha huzuni iliyoikumba jimbo kwa kifo cha wanafunzi seminari hiyo. Kwa vijana waliomsikia akisema maneno haya, kwao waliona himizo la kibaba, kuwa wavumilivu, wenye jitihada na udumufu katika wito wao. Tunu hizi alizokuwa akizisisitiza Kardinali Rugambwa ndizo zilizoanza kuchanuza maua na leo tuna mapadri saba tayari waliopitia kitalu cha Visiga. Hakuna kumbukumbu nzuri tunayoweza kumfanyia Kardinali Rugambwa, isipokuwa kuendeleza kila mmoja wetu anachangamoto ya kukukuza miito ya kichungaji jimboni. Mimi kama mzazi, sisi kama jumuiya, mimi kama kijana wa kike na kiume, tunaalikwa tujiunge na miito ya kichungaji. Wahenga walisema haba na haba ujaza kibaba! Hatua moja baada ya nyingine iliyopigwa na Hayati Mwadhama Laurian Kardinali Rugambwa, tumeanza kuona matunda yake. Shukrani tunayaoweza kumpa Mungu, tunapoadhimisha miaka kumi ya kifo chake: kwa wote waliohitikia rai yake ya kuwa wachungaji wadumu katika wito huo, nasi sote tuendeleze moyo wa kujitoa kwa Kanisa, na hasa Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Pd. Stefano Kaombe