Header

Bishop Methodius Kilaini: BURIANI BABA YANGU

Rugambwa_Kilaini

Askofu Kilaini na Kardinali Rugambwa

Utangulizi

(Makala hii iliandikwa na Padre Method Kilaini kwa magazeti mbali mbali mara baada ya kifo cha Mwadhama Kardinali Rugambwa, 12 Desemba 1997. Padre Kilaini wakati huo alikuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Kilaini alitumwa Roma na Mwadhama mwaka 1968 kusomea Upadre. Hata baadaye alikuwa karibu sana naye kiasi kwamba ndiye alyemwachia kuwa msimamizi wa mirathi yake).


Rugambwa Mwana wa Mfalme wa Kanisa(Prince of the Church)

Rugambwa

Mwaka 1968 tukiwa Roma Kardinali Rugambwa alikuja kikazi Roma. Nilipata bahati ya kumsindikiza mjini Roma na Vatikani. Kwa mara ya kwanza nilielewa ukubwa wa kardinali na nilipolinganisha na jinsi alivyotendewa hapa kwetu ndipo nilitambua unyenyekevu wake. Huko nyumbani Bukoba na Tanzania kwa ujumla watu hawakujua wamwiteje ndipo wakatengeneza maneno ya 'Nyakutununta' kwa kihaya na Mwadhama kwa kiswahili.

Kardinali katika Kanisa Katoliki lenye waumini zaidi ya bilioni moja, ni mmoja wa watu bawaba au wa msingi 130 katika kanisa hilo. Kikanisa yeye yuko juu ya maaskofu, maaskofu wakuu, balozi wa Baba mtakatifu na wengine. Kidiplomatia hupokelewa kama Mwana Mfalme. Yeye hushiriki katika uchaguzi wa Baba Mtakatifu, (Rugambwa ameshiriki kuwachagua Baba Watakatifu watatu). Nakumbuka mwaka 1992, Baba Mtakatifu Yohana Paulo II akiwapokea maaskofu wa Tanzania alimwita mwana wa kwanza wa kanisa la Afrika. Aliwaambia maaskofu kwamba anamheshimu sana kwa sababu alimtangulia kama Kardinali. Rugambwa alikuwa mjumbe katika kamati na tume mabali mbali huko Vatikani ikiwemo ile ya Liturugia na ile ya Uenezaji Injili.

Kama Kardinali alipewa kanisa lake la kudumu Roma, kanisa la zamani sana la Mtakatifu Fransisco wa Ripa. Mwaka 1992 akisherehekea miaka 40 ya Uaskofu aliweza kuwaalika maaskofu wa Tanzania katika kanisa ambako walipokelewa vizuri na waumini wake. Waumini hao walimpenda na kujivunia kuwa na kardinali wa kwanza wa Afrika kama kardinali wao wa pekee.


RUGAMBWA HESHIMA YA WATU WEUSI

Baada ya kuteuliwa kuwa kardinali alipotembelea nchi za Ulaya na Marekani alipokelewa vizuri sana na heshima zote za kiserikali. Ikumbukwe kwamba wakati huu ulikuwa bado wakati wa ukoloni katika nchi karibu zote za Afrika. Kupitia kwake mtu mweusi aliheshimiwa na kukubalika kwa wote. Ulaya hasa Italia, Ugerumani, Uholanzi, Ubelgigi na Austria alipokelewa na viongozi wa juu wa serikali. Ugerumani alionana na Raisi, Waziri Mkuu na kuiongelea Bundestag ambalo ndilo bunge la Ugerumani. Hii ilikuwa heshima kubwa sana ambayo hawapewi hata wakuu wa serikali.

Huko Marekani alihutubia katika vyuo vikuu vingi vilivyomtunuku shahada za juu za udaktari wa heshima. Alikutana na vingozi wa wamerikani weusi ambao walijionea sifa sana kwake. Katika yeye walijivuna kuwa weusi na kukumbuka kwamba wao ni watoto wa Afrika. Kwa mara ya kwanza wamarekani weusi walimwona mwafrika aliyepata cheo kikubwa kama hicho, hata na wazungu wa marekani ingawa waliwadharau watu weusi walimheshimu sana. Makardinali weupe wa Marekeni kama Kardinali Cushing, walimkaribisha majimboni kwao kwa heshima kubwa. Hivyo wote walimwona kama ishara ya uwezo wa mtu mweusi katika harakati zao za kupigania usawa huko marekani. Walianza kujihusisha na kanisa la Afrika.

RUGAMBWA KIUNGO NA MPATANISHI WA WOTE


Kiongozi wa Maaskofu wa Afrika

AMECEA

Rugambwa alikuwa askofu wa tatu mwafrika na kardinali wa kwanza wa bara la Afrika. Maaskofu wa Afrika walimtambua na kumkubali kama kiongozi wao. Wakati wa Mtaguso Mkuu wa Vatikano II (1962-65) uliohudhuliwa na maaskofu zaidi ya 3,000 yeye alikuwa askofu mwafrika pekee aliyepewa fursa ya kuhutubia maaskofu wote kwa pamoja katika ukumbi mkuu katika miaka yote mitatu ya mkutano huo. Hata wazungu ni wachache sana waliopewa fursa hiyo.

Wakati wa mtaguso huo aliwaita pamoja maaskofu wote kutoka Afrika (wengi wao wakiwa wamisionari wazungu) na yeye akiwa mwenyekiti wao zilianza harakati za kuundwa umoja wa maaskofu wa Afrika, (SECAM).Vivyo hivyo Rugambwa alikuwa kiuongo cha kusaidia kuunda umoja wa maaskofu wa Afrika ya Mashariki, zikiwemo nchi za Eritrea, Ethiopia, Somalia, Sudan, Kenya, Uganda, Tanzania, Malawi na Zambia, (AMECEA). Mpaka alipofariki alikuwa bado baba mlezi wa umoja huo. Kwa sababu hiyo alikuwa mjumbe wa kudumu wa kamati tendaji, pamoja na kuwa vile vile baba mlezi wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika ya Mashariki.


Rugambwa na Baraza la Maaskofu Tanzania

Rugambwa ni mmoja wa waasisi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania pamoja na Askofu Mkuu Marantha akiwa askofu mwafrika pekee katika baraza hilo mwaka 1956. Yeye ndiye aliyewakaribisha maaskofu wengine waafrika katika baraza hilo na kuwaelekeza. Baada ya kuwa kardinali mwaka 1960 wengi wao aliwapa uaskofu au aliwasimika katika viti vyao vya uaskofu. Alijiona kama kiungo chao. Hakutaka hata mara moja kukosa vikao vya baraza hili ikijulikana kwamba kwa heshima alikuwa mwanachama wa kudumu katika kamati tendaji mpaka alipostaafu. Askofu Mathias Joseph Isuja akitoa rambi rambi zake alisema 'Rugambwa alikuwa nguzo yetu nakiungo chetu. Kule kuwako kwake kulimfanya mtu kushika adabu. Kama mtu hakushika adabu alimwita na kumwambia neno moja tu na lilitosha.' Vile vile kama alivyoeleza askofu huyo hakuzungumza sana katika vikao vya baraza lakini ilipofika wakati akaona kwamba maaskofu kidogo hawakubaliani alisema maneno machache na ndio ulikuwa mwisho wa mabishano. Alipenda sana umoja wa maaskofu na alitaka wawe kitu kimoja.

Mwaka 1967 alikuwa msitari wa mbele katika kuunganisha seminari kuu za Tanzania ili kuleta umoja. Yeye aliitoa Seminari yake ya Ntungamo iwe kwa ajili ya Baraza zima.

Maaskofu walimpenda na kumheshimu sana. Yeye vile vile aliwapenda sana. Mfano mmoja ni mwaka jana alipoona Askofu Castor Sekwa wa Shinyanga ameugua sana na ukawa muda mrefu bila kumwona, alifunga safari mpaka Shinyanga kumtia nguvu na kumpa moyo licha ya barabara mbaya ingawa yeye tayari alikuwa anakuwa mnyonge kiafya. Alibaki naye zaidi ya wiki moja wakati wa pasaka.


Ad Limina

Mwezi wa saba akiwa kitandani baada ya kutembelewa na maaskofu aliniambia 'Mwanangu najisikia vizuri nikiwaona maaskofu' Kwa kawaida Mwadhama hataniani sana lakini alipokuwa na maaskofu hasa kama Askofu Isuja wa Dodoma, Marehemu Askofu Sekwa wa Shinyanga, Amedeus wa Moshi, hata na maaskofu vijana kama Askofu Paul Ruzoka wa Kigoma na Justin Samba wa Musoma na wengine alitaniana nao sana hata unasahau kama ni yeye ambaye kikawaida ni mtu mtulivu mwenye maneno machache. Alitafuta namna ya kuwafanya wacheke na kujisikia vizuri naye.

Askofu Mkuu Pengo akitoa buriani kwa aliyemwita, Baba yetu Rugambwa, aliongelea juu ya uwezo wake wa kuwa juu ya makabila na vikundi. Akiongelea juu ya kazi yake Dar es Salaam alisema aliweza kuwafanya waumini wa jiji wajisikie wenye kanisa la Dar es Salaam bila kujali walitoka wapi. Aliwapata mapadre wa Dar es Salaam, masista wa Dar es Salaam na waumini wa Dar es Salaam. Kardinali kwao ni Bukoba na Bukoba aliipenda lakini hakupenda ukabila hata kidogo. Akiwa askofu wa Bukoba baada ya kumaliza nyumba yake ya kiaskofu, aliwaalika masista wa Kilimanjaro waje kumtunza na kuhudumia katika nyumba yake. Hivyo watawa waliokuwa karibu naye kumhudumia kwa miaka 34 ya uongozi wake wengi walikuwa ni wachagga. Ni hao vile vile aliowaleta katika seminari kuu ya Ntungamo na siyo shirika lake la Bukoba. Alifanya juu chini kutuma wasichana katika shirika hilo la Kilimanjaro ili wapate upeo wa kitaifa. Kwa moyo huo alipokuja Dar es Salaam alikaribisha mashirika mbali mbali ya watawa kutoka sehemu zote za Tanzania na kuwaweka katika parokia mbali mbali ili kuwafanya watanzania wote wajisike nyumbani jijini.


Rugambwa na Umoja wa Wakristu na Uelewano na Waislamu

Askofu Elinaza Sendoro wa kanisa la Kiluteli Tanzania akitoa rambi rambi zake alimtaja Kardinari Rugambwa kama baba wa umoja wa makanisa Dar es Salaam. Pamoja na Askofu Sambano wa kanisa la Kianglikana walimkumbuka kama mwanzilishi wa umoja huo na mwenyekiti wake kwa miaka 8. Alihimiza ujenzi wa makanisa ya pamoja kama lile la hospitali ya Muhimbili. Wakati wa kuifungua aliomba waibariki kwa pamoja. Huu ni moyo alioukuza katika uongozi wake wote.


Rugambwa

Kamachumu alikozaliwa Mwadhama Laureani Kardinali Rugambwa palikuwepo madhehebu matatu yaliyoshindana. Wakatoliki wakiwa na makao yao katika kilima cha Rutabo, Waluteli wakiwa Ndolage na Waislamu wakiwa wafanyabiashara tajiri Kamachumu mjini. Kwanza alijitahidi kuelewana na kutoa ugomvi kati ya wakristo na Waislamu. Aliwaonyesha upendo wake kwa kuwafanya watambue kwamba analeta maendeleo, elimu na huduma kwa wote bila ubaguzi. Kwa hilo alifanikiwa kiasi kwamba Waislamu wenye siasa kali walimwita Sheik Mkuu wa Bukoba mkristo asiyebatizwa lakini yeye hakujali. Uelewano wake na Waislamu aliueleza vizuri sana Mhashamu Askofu Mkuu Polycarp Pengo aliposema kwamba Waislamu wenye siasa kali Dar es Salaam waliwatukana maaskofu wengine wa madhehebu ya Kikristo kama yeye Askofu Pengo na Sendoro wa Kiluteli lakini siyo kardinali Rugambwa. Siku moja walipojaribu kumgusa, kwa pamoja wakristo kwa Waislamu walikuwa tayari kuwapiga mawe. Hii inatokana na uwezo wake wa kuleta upendo na uelewano.

Kama baba wa Mtaguso Mkuu wa Vatikano II aliamini katika umoja wa wakristo. Alilelewa katika moyo wa Papa Yohana XXIII aliyesema kila wakati 'tafuteni kile kinachowaunganisha na si kile kinachowatenga' Katibu Mkuu wa Chama cha Biblia Tanzania, Mchungaji Albert Mongi akituma rambi rambi za chama alikumbuka maneno ya Kardinali Rugambwa ' Jambo hili (maanake la kueneza pamoja Biblia kati ya wakatoliki na waprotestanti) halihitaji ushawishi. Ikiwa tutashindwa kushirikiana katika huduma ya kuwapa watu Biblia, basi tutakuwa hatuna la kutuunganisha'.

Rugambwa alitumia uwezo wake wote kuleta ushirikiano. Akiwa Bukoba alishirikiana kwa karibu na Askofu wa Kiluteli, Josias Kibira. Kibira alipochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kiluteli ulimwenguni, Kardinali alifanya mpango wakaenda pamoja kumsalimu Papa Paulo VI huko Roma. Picha ya Kardinali Rugambwa na Askofu huyu wa Kiluteli, Kibira, ilipochapishwa katika gazeti na kalenda ya gazeti la jimbo la Rumuli, mmoja akiwa mkono wa kulia na mwingine wa kushoto wa Baba Mtakatifu Paulo VI, iliamsha uelewano na ushirikiano mkubwa kati ya madhehebu haya makubwa ya kikristo Bukoba. Huu moyo wa ushirikiano uliendelea vizuri hivyo hata wakati wa sinodi ya Afrika, Roma 1994, ni mrithi wa Askofu Kibira, Askofu Mushemba aliyealikwa na Baba Mtakatifu Yohana Paulo II kuwakilisha kanisa la Kiluteli Afrika katika sinodi hiyo.

Hata baada ya kustaafu kama wakristu walikuwa na kitu chenye utata au walitaka kumwona Raisi wa Tanzania kwa pamoja kutatua tatizo fulani walimwomba awe kiongozi wao. Yeye alikuwa juu ya tofauti za kidhehebu au kikabila.


MTU MWENYE UPEO MKU


Rugambwa katika Kuelimisha Watu

Jioni baada ya mapokezi makubwa ya Mwili wa marehemu Rugambwa Mwanza, nilipata fursa ya kuongea kwa faragha na Mhashamu Askofu Gervase Nkalanga, Askofu mstaafu wa Bukoba ambaye sasa yuko katika monastri ya wabenediktini wa Hanga. Nkalanga alikuwa parokia moja na Rugambwa alipotangazwa kuwa askofu, baada ya hapo alitumikia chini yake miaka 11, miaka sita kama katibu wa jimbo wa elimu na miaka mitano kama Askofu Msaidizi. Nilimwuliza swali moja 'Ulimwonaje Mwadhama' Hapo uso wa Askofu Nkalanga ulingara kwa tabasamu na alisema: 'Mwadhama alikuwa na upeo mkubwa ajabu, hakukata tamaa katika shida'. Muda wote hasa baada ya kupewa jimbo jipya la Rutabo, lilikiwa fukara, mwadhama alimwambia kwamba kuna ufunguo mmoja tu kwa shida hizi zote, tuwape watu elimu na matatizo mengine watatua wao wenyewe. Askofu Nkalanga anasema katika miaka kumi na moja aliyotumikia chini ya Mwadhama, ingawa jimbo lilikuwa fukara hakuna hata siku moja alikwendea kumwomba fedha kwa ajili ya elimu akamnyima. Nkalanga akasema kwamba hata mapadre wengine wakamchukia wakiuliza kwa nini alipata fedha kwa ajili ya shule na wengine hawakupata kwa ajili ya shughuli nyingine muhimu.


Rugambwa

Upeo wake wa elimu ulikuwa ni wa kumwelimisha mtu mzima, kijamii, kifamilia, na kitaifa. Kutimiza hilo alianza umoja wa 'St. Augustine Social Guild' katika umoja huu aliwaweka pamoja vijana na watu wazima wenye uwezo na kuwaendeleza kwa pamoja. Wale waliokuwa na akili aliwatuma sehemu mbali mbali kwa masomo ya juu hata Ulaya na Marekani. Wengi waliporudi walichukuliwa na serikali lakini aliendelea kuelimisha tu. Kwa watu wa kawaida kijijini aliona kwamba hawawezi kuendelea kama hawajifunzi kuweka pesa zao na kupanga maendeleo yao. Akitumia Marehemu Padre Robert Rweyemamu ambaye baadaaye alikuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu, na Padre Peter Mutashobya, sasa ni mhasibu wa jimbo la Bukoba, alianzisha chama cha kukopa, (Credit union) Kilipofanikiwa katika parokia moja ya Mwemage waliieneza katika jimbo zima na baadaye wakajaribu kulieneza kitaifa. Watu wengi waliinuka kwa huduma hii.

Alipenda kuwaelimisha viongozi akianzia na mapadre, watawa na walei. Ni kweli ni wengi katika makundi hayo matatu aliowaelimisha wanaosaidia taifa katika nyadhifa mbali mbali. Nilipomhoji Sista Caritas Kokuteta ambaye mpaka mwaka huu alikuwa Mama Mkuu wa shirika la masista wa Mtoto Yesu Bukoba juu ya Kardinali, alisema kitu kikubwa alichowafanyia ni kwamba aliwaelimisha. Aliendelea kusema sasa wanaweza kujiendeleza wenyewe na kutatua matatizo wanayoyapata kwa sababu aliwapa elimu.

Askofu Nkalanga anasema kwamba mara nyingi ilikuwa vigumu kuelewa malengo yake kwa sababu yalionekana magumu na ya juu mno yasiyoweza kutekelezwa. Lakini mwadhama alisema kila mara kwamba itawezekana tu, na kama kwa mwujiza iliwezekana. Mwishoni wale aliofanyakazi nao walipata imani kubwa kwake na walitimiza kama Yesu alipowaambia wafuasi wake wawagawie umati wa watu elfu tano vipande vitano vya mikate na wakafanya. Uhusiano wake na serikali ulikuwa mzuri kwa sababu yeye alichotaka kwao ni kwamba wampe fursa ya kufanya mema, kujenga hospitali, mashule na kupewa fursa za kutoa huduma kwa watu. Askofu Nkalanga anasema kwamba serikali ilipoanza kuzungumzia juu ya kutaifisha shule za kanisa alimwuliza Kardinali kama aendelee kujenga au aache, na kardinali alimjibu, 'endelea kujenga ili wapate cha kutaifisha, si shule zitaendelea kuelimisha watu' Kutaifisha haikuwa shida ya Kardinali mradi bado zinaendelea kulea watoto na vijana. Hii ndiyo sababu hata baada ya kutaifisha mashule bado aliendelea kuwa karibu a shule zilizotaifishwa.

UJENZI WA SEMINARI

Mwadhama Kardinali Rugambwa aliamini kwamba uchungaji hauwezi kufanikiwa kama hakuna wachungaji wenye akili, ucha Mungu na elimu ya kutosha. Hivyo nguvu zake za kwanza zilikuwa kuwapata mapadre waliotayarishwa vizuri.


Seminari Ndogo ya Rutabo

Alipoteuliwa kuliongoza jimbo changa la Kagera ya Chini ambalo baadaye liliitwa Rutabo alikuwa na mapadre 17 tu wote wa jimbo. Wakat huo kulikuwepo seminari ndogo ya Bunena na seminari ya sekondari ya Rubya kwa ajili ya jimbo la Bukoba. Mara alipewa idadi ya watoto ambao angeliweza kupeleka katika seminari hizo. Mara moja akaona umuhimu wa kufungua seminari yake walau ile ndogo. Mwaka 1958 alifungua seminari ndogo ya Rutabo iliyowapokea vijana kwa ajili ya darasa la tano. Seminari hiyo ipo hadi leo na imekwisha elimisha vijana na kutoa mapadre wengi.


Seminari Kuu ya Ntungamo

Baada ya kuwa askofu wa Bukoba aliona umuhimu wa kuwa na Seminari Kuu badala ya kuwatuma mafrateli Uganda.

Ntungamo

Aliomba msaada na kujenga seminari Kuu ya Mtakatifu Antoni wa Padua pale Ntungamo nje kidogo ya Bukoba mjini. Seminari hii ilipokea mafrateli wa kwanza wa jimbo la Bukoba na Rulenge mwaka 1964. Mwaka 1967 maaskofu wa tanzania walipomuomba iwe sehemu ya seminari ya taifa alikubali na hadi leo ni Seminari Kuu ya Falsafa.


Seminari Kuu ya Segerea

Mwadhama Laureani Kardinali Rugambwa alipohamishiwa jimbo Kuu la dar es Salaam mwaka 1969, jambo la kwanza alilotambua ni kuona changamoto za jiji ambazo zilihitaji mapadre ambao wamezoea kusuguana nazo. Aliona vile vile kwamba kuwa na seminari Kuu jijini kutaongeza chachu siyo tu kwa ajili ya jimbo Kuu la Dar es salaam bali kama kitovu cha nchi kutachangia katika kutatua changamoto za kitaifa. Aliomba pesa na kujenga seminari Kuu ya Segerea ambayo ni sehemu ya mfumo wa taifa ikiwa kwa ajili ya Tauhidi (Teologia). Sasa inaendelea kutoa matunda yake.


Seminari ya Visiga

Juhudi za mwisho katika kuanzisha seminari zilikuwa Dar es Salaam. Kwa miaka mingi alituma waseminari katika seminari ya Mtakatifu Petro, Morogoro lakini alivyosema hakupata mapadre wengi.

Visiga

Hapo aliazimia kuanza seminari ndogo ya Jimbo Kuu la Dar es Salaam ambapo angewafundisha vijana katika mazingira watakayofanyia kazi. Alijenga seminari hiyo Visiga, nje ya mji wa Dar es Salaam mkoa wa Pwani. Ilifunguliwa mwaka 1990 na alipostaafu mwaka 1992 vijana walikuwa katika kidato cha pili. Kilichomfurahisha sana ni pale Umoja wa Wanawake Wakatoliki wa Dar es Salaam ulipoipokea na kuikumbatia shule hiyo.

Kabla hajafariki alipata habari kwamba imekuwa shule ya nne kitaifa katika mitihani ya kidato cha nne, hii ilikuwa ni faraja kubwa. Katika majimbo yote matatu aliyoyaongoza, alitayarisha walimu wa seminari kwa kuwatuma mapadre kujifunza katika vyuo vikuu mbali mbali ndani na nje ya nchi.


MWADHAMA RUGAMBWA NA MAENDELEO YA ELIMU YA WANAWAKE

Askofu Nkalanga anasema kwamba akiwa katibu wa jimbo wa elimu mwadhama alimwambia kwamba asielimishe wavulana tu bali hasa wasichana. Kwani wanawake ndio walimu wa binadamu. Alipopokea jimbo la Rutabo, wamisionari wote wa Afrika waume kwa wake waliondoka akabaki na mapadre na watawa Wafrika. Mpaka wakati huo watawa waafrika wa Mtakatifu Tereza wa Mtoto Yesu walikuwa hawajapata elimu ya kutosha kuendeleza elimu ya wanawake. Hapo ndipo alikwenda kuwatafuta masista wa Kanosa mwaka 1956 waje kusadia. Walipofika Mugana aliwapa jukumu moja nalo ni kuendeleza wanawake katika njia yote. Chini ya mama yao Riveta waligawana kazi. Sr. Josephina aliona watoto wana nguo zimechanika akaanza shule ya akina mama 300 akiwafundisha kushona kwa kutumia sindano, kitu kidogo lakini kilileta tofauti sana katika maisha ya watu, na baadaaye akaanza mambo mengine ya maendeleo ya akina mama, na mwishowe shule ya maarifa ya nyumbani ya kwanza Bukoba, na baadaye wakaanza vile vile shule ya kati ya wasichana. Sr. Carolina akaanza na Sr. Victoria kliniki za akina mama ambayo sasa imekua na kuwa hospitali kubwa ya Mugana, shule ya wakunga wasaidizi na fani nyingine.

Alivyofanya hapo Mugana ndivyo alivyoendelea kutafuta watawa wenye moyo na ujuzi hasa kuwasaidia akina mama katika elimu, afya na maendeleo hadi alipostaaafu Dar es Salaam. Aliwatafuta masista wa Breda Uholanzi kufungua hospitali ya Rubya, sasa ni hospitali teule ya wilaya, Masista wa Familia takatifu kutoka Uholanzi kuanza shule ya msingi ya pekee Rumuli na shule ya kati Mwemage, Masista wa Mtakatifu Paulo kushika duka la vitabu la Mtakatifu Joseph Dar, wakamelitane - Changombe, Waivrea - Kawe, nk. Nakumbuka nilimsindikiza kwa masista wa Kamelitane na Waivrea alipokuwa anaomba, kila mara aliweza kujieleza vizuri sana na kuonyesha ulazima wa wao kuja kusaidia wanawake.

Katika kupigania elimu ya wanawake labda ya kukumbukwa kuliko zote ni ujenzi wa shule ya sekondari ya wasichana ya Rugambwa. Wakati huo hata kiulimwengu haja ya kuwasaidia wanawake ilikuwa bado haijapata msisitizo. Hapa Askofu Nkalanga anasema aliponiambia kwamba tujenge shule ya wasichana hadi kidato cha sita baada ya kuteuliwa kuwa kardinali, sikuamini masikio yangu kwa sababu hatukuwa na chochote. Akasema yeye nilikuwa namwona kama nabii kwa sababu aliposema tutafanya kilifanyika hivyo niliamnini tu. Kwanza kupata ardhi ilikuwa shida lakini hapo Mwadhama hakuogopa mtu awe nani hata wakubwa wengine wa serikali walipoweka vipingamizi alipigana tu. Hapa alitumia hadhi yake kwa watu ambao walimwunga mkono.

Kwa ajili ya ujenzi alikwenda Ujerumani; akisaidiwa na Misereor, alionana na bunge zima la nchi hiyo akiwemo, Raisi na viongozi wengine ambao wote aliwahubiri juu ya ulazima wa kumwelimisha msichana mama na mwalimu wa kesho. Kote huko hakuomba kitu kingine ila hicho tu. Walimwamini na kumpa fedha za kujenga shule nzuri sana yenye kupendeza. Ilipokuwa tayari serikali ilisema haina pesa za kuanza wakati huo kuiendesha, lakini akisaidiana na wananchi hasa wakulima wa kahawa wa Bukoba walikubali kukatwa hela kuendesha shule, aliifungua mwaka 1964. Kusimamia na kufundisha katika shule hiyo aliwapata masista mashuhuri kwa kuendesha shule za wasichana, Masista wa Maryknol. Hawa tayari waliendesha shule za wasichana za Marian Morogoro na Rosary college Mwanza. Hapa siyo tu alijenga shule bali kwa kuwahusisha wananchi kuchangia uendeshaji wa shule hiyo, aliifanya shule ya watu wanaothamini elimu ya wasichana.

Katika maisha yake alipenda kuendeleza elimu hasa ya wasichana kama chaguo la kwanza. Hata mwishoni mwa utawala wake Dar es Salaam alitumainia bado kujenga shule ya sekondari ya wasichana ya bweni aliyotaka kuita 'Omushumba' maanake mchugaji. Kwa hilo alimaanisha kazi yake ya uchungaji ni hasa kuelimisha wasichana kama namna ya pekee ya kuelimisha jamii.


Shirika la Dada wadogo wa Mtakatifu Fransisko wa Asizi

Katika uzee wake kitu kimoja alichojivunia lilikuwa ni shirika hili la watawa wa Dar es Salaam. Alisumbuka sana kulianzisha hasa kuwapata walezi wazuri na kuwapa mwongozo. Tulicheka kwa sababu kila ulipokwenda kumtembelea alikuonyesha picha hizo bila kutambua kwamba alisha kuonyesha picha hizo mara nyingi.

Masista

Alipokwenda Ulaya alikwenda na picha hizo za wajukuu wake kama tulivyowaita kwa utani. Kila mara alitoa picha hizo mkobani na kukueleza jinsi anavyotaka dada hao wadogo wawe watawa wa Jiji wenye kujiamini, elimu na mbinu mpya za uchungaji. Aliwashika kama mboni ya jicho lake.

Kadiri siku za kustaafu kwake zilivyokaribia ndivyo alivyozidi kupata homa juu ya wajukuu wake hao. Aliogopa kuwaacha yatima. Alipostaafu kwa wema wao hakuwaingilia ili wampokee askofu mkuu mpya na waweze kuedelea bila yeye. Hata hivyo kila mara aliulizia kwa mbali jinsi wanavyoendelea. Alifurahi kuona wanakua vizuri na kushika kasi nzuri chini ya uongozi wa Sr. Paulin Bommer na shirika la 'Divine Providence' la Balddeg Uswizi aliokuwa amewakabidhi.

Hospitali ya Ukonga

Ukonga

Mradi mwingine wa mwisho ilikuwa hospitali ya Ukonga. Aliweka nguvu nyingi sana katika mradi huu, kuipata ardhi ilikuwa na mlolongo mrefu sana lakini hakukata tamaa. Kwa sababu aliamini kwamba anataka kuwasaidia watu wa sehemu hiyo ambayo ilikuwa mbali na huduma za afya alitumia nguvu zote za wadhifa wake kuleta ufanisi. Kazi nyingine ilikuwa kuwapata wafadhili.

Katika hayo yote alifanikiwa na kuanzisha kituo cha afya cha Ukonga kikiwa na lengo la kuwa hospitali kamili. Aliwaomba masista wa shirika la Mtakatifu Therezia wa Mtoto Yesu wa Bukoba wamsaidie kuiendesha. Misingi aliyoiweka ilifanikisha kituo hicho ambacho sasa ni hospilati. Tunashukuru uongozi wa jimbo Kuu la Dar es salaam ambao walitambua juhudi hizo na kuiita jina lake. Pamoja na Ukonga aliyaalika mashirika mengine kufungua zahanati katika sehemu mbali mbali za jiji ikiwemo, Tegeta, Kawe na Kibiti.


SIRI YA UFANISI WA RUGAMBWA


Baada ya ibada ya Misa ya kumwombea marehemu Rugambwa nilimwendea Padre Jovin Bakekera na kumwuliza aniambie siri ya mafanikio ya Kardinali Rugambwa. Padre Jovin alikuwa katibu wake katika miaka tisa ya mwisho. Alifanya kazi naye katika ofisi na aliishi naye nyumbani hadi alipokata roho. Baada ya kufikiri kidogo Bakekera alisema 'sitaki mimi nimwite mtakatifu lakini katika uamuzi wa kibinadamu alikuwa mkamilifu.' Hii ilikuwa hoja kubwa; hivyo, nikamwomba maelezo. Alisema kufuatana na cheo chake, heshima yake ya kifalme na unyamavu wake watu wengi walimwogopa, lakini nakwambia ukweli nilikaa naye miaka hii yote kwa sababu ana moyo mzuri ajabu, ingawa alikuwa na misimamo thabiti lakini hakupenda kumwudhi au kumwonea mtu. Kama alifanya kitu na akaona amekuudhi hata ukiwa mdogo uliona alifanya juu chini mwenyewe kukuonyesha kwamba anasikitika na anakuwa wa kwanza kuja kwako.

Niliuliza swala hilo hilo Askofu Nkalanga, alinijibu kwa kiingreza 'He had a golden heart' alikuwa na moyo wa dhahabu. Akasema watu wameongelea sana juu ya unyenyekevu wake lakini nadhani zaidi ya unyenyekevu yeye alikuwa na upendo mkubwa kwa watu. Yeye alijinyima vitu vingi hata kukuta nguo zake nyingine zimechakaa lakini kila alichopata alitaka kiende kwa watu wenye shida. Na mimi vile vile nilimjua kwa miaka 30. Hasa katika miaka ya 80 alipoanza kuugua alikuja Roma kwa matibabu nikiwa mwanafunzi, kitu kikubwa ambacho wote walijua ni kwamba hakutaka hata mara moja kusumbua watu hata kama aliumwa, alitaka watu wafanye mambo yao wamalize kabla ya kumhudumia.

Siri yake nyingine ni kwamba alijua kutumia vipaji vya watu. Alipokuwa na kazi alimpa mtu aliyeamini ataifanya vizuri lakini vile vile alifuatilia na alitaka ripoti kamili za mara kwa mara. Mwadhama alijali sana uwezo katika kutoa kazi au madaraka, mtu akifnya vibaya awe nani atamnyang'anya kazi au madaraka. Alichukia kama kitu kilifanywa vibaya. Watu wengine walimchukia kwa sababu alitaka ripoti. Lakini jambo hilo liliwafurahisha wafadhili kwa sababu alikuwa mkali sana katika matumizi ya fedha na kutoa ripoti. Kwa sababu hiyo wafadhili wengi walimsaidia wakijua kwamba fedha zitatumika vizuri kama zilivyokusudiwa.


PUMZIKA KWA AMANI RUGAMBWA

Kilaini

Apumzike kwa amani Rugambwa kwa kazi yake kubwa aliyoifanya. Alivyotaniwa kila wakati na Askofu Isuja wa Dodoma, yeye alikuwa namba one, katika upadre kijijini mwake, katika uaskofu Tanzania, Ukardinali Afrika, na Askofu Mkuu wa kwanza Mtanzania Dar es Salaam. Sasa yuko kwa Mungu kama Mwobezi wetu. Mungu amweke mahala pema mbinguni na sisi tufuate katika nyayo zake. AMINA.




Contact Information
Bishop's House Ntungamo,
P.O.Box Private Bag,
Bukoba, Tanzania.
Tel. & Fax. 028 - 2220746
Office: Tel. 028 - 2220194
E-mail: b.officebk@yahoo.com
Website: www.bukobadiocese.co.tz
© Bukoba Catholic Diocese 2023
Find us on
Facebook: Bukoba Catholic Diocese
Twitter:  @bcdcatholic