Header

Maaskofu Walivyomfahamu Mwadhama Rugambwa

Rugambwa_Maaskofu

MPENDWA MWADHAMA RUGAMBWA

Na Mha. Nobert Mtega, Askofu Mkuu wa Songea

Desemba 1985 nilipata fursa ya kwanza kukutana naye ana kwa ana katika ofisi ya nyumbani kwake. Ni siku chache tu baada ya kuteuliwa kwangu kuwa Askofu wa Iringa, nikiwa safarini kwenda Roma kwa ajili ya kupewa daraja la Uaskofu. Kwa mara ya kwanza nilitambua kwamba Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa alikuwa mwenye upendo wa kibaba, ingawa kwa nje haukuonyeshwa waziwazi. Aliniambia maneno mazito ya kunitia moyo, akanipatia ushauri mwingi, akapokea na mwaliko wangu wa kufika Jimboni Iringa kuongoza Misa Takatifu siku ya kusimikwa kwangu. Katika nafasi hii ya kusimikwa kwangu tarehe 9 Machi 1986, Mwadhama alipokaa kwa siku takribani mbili, mtu aliweza kujifunza zaidi juu ya utu wake: alikuwa baba kwa wote: kwa maaskofu, kwa mapadri, kwa watawa, kwa walei. Kila mmoja wetu aliyebahatika kumsogelea na kumsikiliza alivutiwa na jinsi yake ya kuuliza maswali kwa utulivu, jinsi alivyomsikiliza kwa makini kila aliyekuwa anaongea naye, jinsi alivyopenda kujua zaidi na zaidi juu ya maisha na kazi zetu.


Rugambwa_Mtega

Mmoja aliweza pia kujifunza kwamba alikuwa mtu wa imani ya kina na thabiti, mtu aliyependa sana maendeleo na kukua kwa Kanisa na nchi. Papo hapo mmoja aliweza kung'amua kwamba licha ya kuwa Mwana (Prince) wa Kanisa, wa kwanza katika Afrika na Askofu wa Kwanza Mtanzania alibakia ni mnyofu, na mwana mpendwa wa Afrika, Mtanzania kwelikweli, mmoja aliyezaliwa na kukulia katika utamaduni wa nyumbani na vionjo vya Kihaya. Ninakumbuka Masista Wateresina waliguswa sana kiroho alivyokuwa amewajali kama Baba, na kule kuwa tayari kuongea nao alipokuwa amewatembelea katika Nyumba yao Kuu, hivi kwamba mara baada ya kurudi Dar es Salaam, walimtumia ujumbe wa masista watatu kumpelekea paketi nzuri ya senene "zilizoandaliwa kwa makini sana", ambazo, kama tunavyojua, ni chakula cha kipekee kabisa katika utamaduni wa Wahaya. Mwadhama naye alifurahia sana ishara na alama hiyo ya masista kwamba naye akawanunulia doti kadhaa za Vitenge ambavyo walivipeleka lringa. Walinisimulia tukio hilo wao wenyewe ili kutilia mkazo wa hisia walizozipata ambazo hawakuzitarajia za unyofu na urahisi wa kumkaribia Kardinali huyo, ambaye kwa nje alionyesha hali ya kuwa na tabia yenye haiba ya kichifu. Hapo walitambua kwamba ni baba wa wote, baba wa upendo, baba wa Kanisa na baba wa Afrika.

Kisha, mimi mwenyewe, nikiwa mmojawapo wa Maaskofu wa Tanzania, nilikuwa sasa na bahati ya kukutana naye mara nyingi zaidi wakati wa mikutano ya Maaskofu na katika matukio na maadhimisho mbalimbali ya kikanisa. Ukaribu huu wa kukutana kiurika unamwachia mmoja hisia zifuatazo juu ya nafsi ya Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa:

Mwonekano wake wa heshima, mtulivu, wa kitawala. Inatakiwa kujua na kukumbuka anatokana na damu na familia gani. Lakini hata akiwa Kardinali wa kwanza katika Afrika Nyeusi ya zama zetu, alidumu wa kawaida, halisi, wa kweli, na uthabiti wa hali ya juu.

Kwa umakini wa hali ya juu sana, kwa utulivu na amani ya maisha ndani ya Kanisa na katika jamii ya Kitanzania, na ulimwenguni. Kila aina ya vurugu, za karibu au za mbali, kila aina ya kutoelewana na kuhasimiana, na bila shaka kila wakati wa mapigano au vita, yalikuwa ni masuala ambayo yaliibua uangalifu. Hilo liliweza kuonekana wakati wa mikutano tulipokwa tunajadili masuala mbalimbnali. Uchaguzi wake katika masuala mengi sana ulikuwa ni: upatanisho, suluhu ya amani, kutaneni tena, fanyeni kazi pamoja.. Aliweza kushauri dhidi ya jaribio lolote la kutumia mabavu, kulazimisha, nguvu au hata kuamrisha bila sababu. Alipendelea zaidi mazungunizano ya amani, maelewano, na kuamsha dhamiri, kufanyia kazi uongofu. Ndiyo aina ya tabia — amani na maelewano katika upendo aliotufundisha Kristo.

Hata hivyo hakuchelea kuachilia makosa na maoni yasiyo sahihi katika masuala ya msingi, ya imani na ya nidhamu.

Hakuongea sana, lakini alikuwa na nguvu ya kueleza mengi kwa alama na kwa ishara mbadala.

Hakuwa mwepesi sana kuwaendea watu, lakini alipenda kuwaalika na kuwaashiria wengine wamsogelee kushirikishana mawazo, na hata kuwataka wawe pamoja naye.

Mtu wa hadhi ya Kikardinali alihudhuria mikutano na vikao vyote vya Baraza kwa wakati wake na kusikiliza yote yaliyojadiliwa mpaka mwisho. Tulimstahi kwa hilo. Kwa namna hiyo na kwa moyo huo alilisaidia sana Baraza la Maaskofu kisaikobojia.

Alikuwa na upendo wa pekee kwa nchi yake ya Tanzania: Mapenzi yake makubwa kwa masuala ya kitaifa, yalikuwa bayana kwa msukumo wake chanya wa kusonga mbele na maendeleo, misaada yake kwa serikali.

Unyofu wake na uhalisia wake uliwavutia pia watu wa Roma, kwa nanma ya pekee wanafunzi Waafrika, kwa sababu kila alipokwenda alipata malazi katika Kolejio ile aliyokaa wakati wa masomo yake, na kule hakuwa na madai ya pekee, alikula pamoja na wanafunzi bila kutaka kitu cha kipekee, alishukuru kwa kila aina ya huduma aliyopewa, alimpokea kila aliyemwendea, na juu ya yote, alidumu ni mtu wa sala na wa imani ya kina.

Haya ni mawazo machache kadiri ya maoni yangu juu ya Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa, tunayemkumbuka kwa furaha, Askofu wa kwanza wa Tanzania, Kardinali wa kwanza Mwafrika wa zama zetu, Mkuu wa Mababa wa Afrika wa Mtaguso wa Pili wa Vatikano, Askofu wa Rutabo, Bukoba, na Askofu Mkuu wa Dar es Salaam. Mungu ampokee katika amani ya milele na apumzike kwa Utukufu wake na kwa wokovu wa roho za watu. Maisha na kifo cha Laurean Kardinali Rugambwa, kiwe mbegu ya imani halisi Tanzania na katika Afrika.

+Norbert Mtega


NITAKUKUMBUKA DAIMA MWADHAMA KARDINALI RUGAMBWA

Na askofu Aloysius Balina, askofu wa Jimbo la Shinyanga

Rugambwa_Balina

Baba huyu kwangu ni mfano wa Unyenyekevu na majitoleo makuu. Amekuwa ni mwalimu na baba ambaye daima nilipokutana naye nilisikia moyoni mwangu himizo la kujifunza karama zake za unyenyekevu. Hakuwa mwepesi wa kutoa maamuzi. Kila jambo kwake lilikwenda kwa tafakari nzito, ndio maana maamuzi yake yalikuwa na matokeo ya muda mrefu. Hakufanya maamuzi ya zima moto hata siku moja.Alifika siku moja Jimboni Geita nikiwa Askofu wa Jimbo hilo. Wakati huo alikuwa na afya mbovu. Barabara ya kutoka Mwanza kuja Geita ilikuwa mbaya sana, lakini alifika kuniona na kunisalimia. Yeye kama Kardinali mwenye umri mkuu na mimi kama Askofu kijana, lakini alikuja kwangu. Nilisikia moyoni deni la ajabu na hasa kwa maongezi aliyoniambia ya kunitia moyo katika utume wangu. Nitamkumbuka daima Mwadhama Kardinali Rugambwa.

+ Aloysius Balina


UHUSIANO KATI YANGU NA LAUREN KARDINALI RUGAMBWA (1954-97)

"Katika shida nilionja upendo na ukaribu wa Mwadhama"
Na Askofu Mathias Isuja Joseph: Mstaafu wa Jimbo la Dodoma

I. mwaka 1954. Kwa mara ya kwanza nilimwona Askofu mwafrika nikavutiwa sana naye kwa jinsi alivyoonekana nadhifu na wa kupendeza mbele ya Maaskofu wote. Sisi waseminaristi tulifurahi sana kumwona, kwa upande wangu aliniimarisha katika wito wangu wa upadri, nikatamani sana kuwa Padri, na hata kuwa Askofu Mungu akinijalia. Na ndivyo ilivyokuwa.

Rugambwa_Isuja

Nikiwa katibu wa elimu jimboni Dodoma, katika mikutano yetu ya makatibu wa elimu wa Majimbo tuliba­dilishana uzoefu kati ya Makatibu. Nilivutiwa sana na mipango wa elimu wa Jimbo ni Bukoba ambayo ilikuwa ikiongozwa na Mwadhama kardinali Rugambwa, na katibu wake wa elimu akiwa hayati Padri Longino. Nilifurahi sana kufanya kazi kwa ushirikiano na marehemu Padri Longino ambaye alinisaidia sana kwa utendaji kama katibu wa elimu wa Jimbo. Lakini mpango mzima wa elimu ulikuwa ni wa Mwadhama Kardinali ndiye aliyetupa mbinu za kuiongoza elimu katika majimbo yetu.

Mwakaa 1969, Mwadhama alihamia Jimbo Kuu la Dar es Salaam, na hivyo akawa Askofu Mkuu wa Kanda yetu ya Dar es Salaam. Nami nilifurahi. sana kuwa karibu naye, na hasa tulipokuwa katika mikutano yetu ya kichungaji ya kanda. Katika mikutano ya elimu hasa ya Seminari zetu za Kanda zile za: St.Peter's Morogoro, St.Augustine- Bihawana Dodoma, Soni Tanga, Kasita Mahenge na baadaye Visiga Dar es Salam.

Mwadhama Rugambwa alionyesha tamaa yake kubwa ya kuziunganisha seminari zetu za kanda kwa kuwa na mipango endelevu. Mimi binafsi nilivutiwa sana na ushauri wake. Ni kutokana na mawazo yake sèminari yetu kuu ya Segerea ilianzishwa. Mwadhama alitia maanani. sana elimu ya juu kwa mapadri. Ndiyo maana aliwatuma mapadri. wengi katika Jimbo la Bukoba kuchukua masomo ya juu.

Nikiwa makamu wa Askofu Dodoma, Mwaka 1969, Mwadhama alihamia Jimbo Kuu la Dar es Salaam, na hivyo akawa Askofu Mkuu wa Kanda yetu ya Dar es Salaam. Nami nilifurahi. sana kuwa karibu naye, na hasa tulipokuwa katika mikutano yetu ya kichungaji ya kanda. Katika mikutano ya elimu hasa ya Seminari zetu za Kanda zile za: St.Peter's Morogoro, St.Augustine- Bihawana Dodoma, Soni Tanga, Kasita Mahenge na baadaye Visiga Dar es Salam. Terehe 26.6.1972, Papa Paulo wa VI aliponiteua kuwa Akofu wa Jimbo la Dodoma.Nilipewa daraja ya Uakofu na Mwadhama Kardinali Rugambwa, akisaidiwa na Mhashamu Askofu Mkuu Marko Mihayo na Mhashamu Askotu Adrian Mkoba tarehe 17.9.1972 katika kiwanja cha taifa cha Dodoma na kusimikwa rasmi siku hiyo katika kanisa kuu la Mt.Pauho wa Msalaba. Nilianza kuliongoza Jimbo la Dodoma katika hali ngumu nikiwa na upungufu wa mapadre na hali ya uchumi mbaya lakini Mwadhama alinipa moyo na daima tulipokutana aliniambia Mathias 'Sursum corda' (maanake inua moyo). Nilipata moyo na nguvu mpya kuendelea na kazi yangu.

Mwadhama alinishauri kufungua mara moja seminari ndogo ambayo wakati huo ilikuwa imefungwa. Niliitikia wito wake na mwaka 1982 baada ya matayarisho ya walimu nilifungua seminari ya Bihawana. Mapato yake ni kwamba seminari hiyo tayari imekwisha toa zaidi ya mapadri 40. Baada ya kuwa askofu uhusiano wangu na Mwadhama ulizidi kuongezeka.

Mwadhama Laureani Kardinali Rugambwa baada ya kustaafu kuwa askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam mwaka 1992 alihitaji misaada mbali mbali ya hali na mali. Nami kama mtoto wake nilikuwa tayari wakati wöte kumpatia alichohitaji, Mara nilipotambua shida zake sikungoja aombe.

Ni kweli mtumishi huyu wa Mungu alikuwa na imani thabiti, upendo na unyenyekevu mkubwa nilivyomjua mimi kwa ukaribu. Alikuwa mpenzi wa Mama Bikira Maria na daima alimtaja kama "Mater boni concilii" (Mama wa shauri jema).. Siyo kwa bahati alikufa tarehe 8 Desember 1997 katika sikukuu ya Mama Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya asili. Ni mapenzi yake Mungu, Alipenda mtumishi wake, mpenzi wake mama wa Mungu afe siku hiyo. Tumwombe Mungu mtumishi huyu wa Mungu aingizwe katika mchakato wa mwanzo wa kutajwa kuwa mwenye heri na baadaye Mtakatifu.

A .M • D • G. Matthias Isuja Joseph Episcopus Emeritus Diocese of Dodoma.


NILIVYOMFAHAMU KARDINALI RUGAMBWA

"Nilimfahamu kama mwadhimishaji mahiri wa liturjia ya kanisa"
Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Jimbo la Iringa

Ulikuwa ni mwaka wa 1960. Wakati huo nilikuwa na umri wa miaka 11 na miezi 6. Nilikuwa ninasoma katika Seminari ya Tosamaganga Jimboni Iringa, Darasa la Tano. Vuguvugu la Uhuru lilikuwa hewani na jina la Julius Kambarage Nyerere lilikuwa tayari vichwani mwa 'Watanganyika'. Ndipo vyombo vya habari vilipotangaza kuwa mwana wa 'Tanganyika' Lauriani Rugambwa alikuwa amechaguliwa na Papa Yohane wa XXIII kuwa Kardinali. Baadaye ilielezwa wazi kuwa Rugambwa alikuwa Kardinali wa kwanza kutoka Bara la Afrika, Aidha ilijulikana kuwa Kardinali huyu alikuwa ni Askofu wa Jimbo la Rutabo, Bukoba, Magharibi mwa Ziwa Victoria, katika kilichokuwa wakati huo Lake Province.

Rugambwa_Ngalalekumtwa

Mwaka 1988 niliteuliwa kuwa Askofu Mwandamizi wa Jimbo la Sumbawanga. Baada ya kupokea daraja la Uaskofu huko Roma tarehe 6 Januari 1989, nilirudi Jimboni Iringa kupitia Dar es Salaam, mwanzoni mwezi Februari. Hapo nilipata fursa ya kumsalimia Mwadhama Kardinali Rugambwa. Alinipokea kwa upendo wa Kibaba. Niliongea naye. Alinipongeza na kunipatia baraka yake, na kunitakia utume mwema.

Mwaka 1990 tulikuwa na ziara ya kwanza ya Papa Tanzania. Hivyo Maaskofu tulikuwa na vikao kila mwezi kuanzia Januari hadi Septemba alipofika nchini Papa Yohane Paulo wa 11. Mwadhama Kardinali Rugambwa alishiriki vikao hivyo, na kutushirikisha uzoefu wake. Nilifurahi daima ushiriki wake. Na mara nyingine nilijitahidi kukaa jirani naye.

Mwadhama Kardinali Rugambwa aliendelea kushiriki vikao vya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania muda wote alipokuwa Asfofu Mkuu wa Dar es Salaam na hata baada ya kustaafu. Baadaye afya yake ilipoanza kushuka Maaskofu wa Kamati Tendaji ya Baraza tulimtembelea nyumbani kwake. Alitupokea kwa upendo na upole.

Tarehe 8 Desemba 1997 Mwadhama Kardinali Rugambwa aliitwa na Mungu kurudi kwake. Nilishiriki adhimisho la Misa Takatifu ya kumuaga ndani ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu, Dar es Salaam. Halafu nilikuwa katika msafara wa kusindikiza maiti yake uwanja wa ndege wa Dar es Salaam. Hapo nilimuaga akielekea Jimboni Bukoba, kwa ajili ya mazishi yaliyofanyika huko. Nami nilirudi Jimboni Iringa nikiwa na kumbukumbu za shukrani kwa Mungu kwa mwana huyu wa Kanisa, Mtanzania, Mchungaji katika ngazi ya Ukardinali. Mchango wake katika Kanisa la Mungu Tanzania, na katika ulimwengu, hautasahaulika. Mungu ampokee kwake na kumstarehesha katika amani ya milele.

+Tarcisius J. M. Ngalalekumtwa.


ASKOFU MGULUNDE NA MWADHAMA RUGAMBWA

Na Mha. Askofu Mario Mgulunde wa Iring: Siku ya Jubilei ya Fedha ya Uaskofu 1977

Hayo tumepata fursa ya kuyatafiti leo hii tunaposherekea miaka 25 ya Uaskofu wa Mwadhama Kardinali Laurian Rugambwa. Tunaungana naye katika kuzitoa dhabihu za shukrani kwa neema alizomjalia muda huu wote. Imekuwa ni miaka ya kazi nyingi za kitume. Kanisa la Rutabo, Bukoba, DSM na Tanzania nzima, na kanisa zima la ulimwengu wote limeshuhudia bidii yake katika kutenda kazi kwa ajili ya Taifa la Bwana. Matunda wote tumeyaona.

Rugambwa_Mgulunde

Katika dhiki mbalimbali hakukata tamaa, maana alimjua yeye aliyemwamini na hakutahayarika. Tuna haki na sababu ya kufurahi pamoja naye . "Atukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli, kwa kuwa amewajia watu wote na kuwakomboa. Ametusimamishia pembe ya wokovu, katika mlango wa Daudi, mtumishi wake" (Lk 1:68-9).

Hii ni ishara wazi ya upendo wa Mungu. Neema zake kwetu sisi hazikuwa bure. Ametuinulia mchungaji kadiri ya roho yake akampaka mafuta ya ukuhani kati ya ndugu zake. Naye amekuwa mchungaji mwema wa ndugu zake akiwasitawisha katika neema za ukombozi. Moyo wetu unamfurahia Bwana Mungu wetu kwa ajili ya fadhili zake. Siku hii ndiyo aliyoifanya Bwana, tutaishangilia na kuifurahia.

Askofu Mario Mgulunde: Baadaye akawa Askofu Mkuu wa jimbo Kuu la Tabora



Contact Information
Bishop's House Ntungamo,
P.O.Box Private Bag,
Bukoba, Tanzania.
Tel. & Fax. 028 - 2220746
Office: Tel. 028 - 2220194
E-mail: b.officebk@yahoo.com
Website: www.bukobadiocese.co.tz
© Bukoba Catholic Diocese 2023
Find us on
Facebook: Bukoba Catholic Diocese
Twitter:  @bcdcatholic