Header

MABINTI WA RUGAMBWA

Mabinti

Ninavyomfahamu: Kardinali wa kwanza Mwafrika na Mwanzilishi wa Shirika letu

Na Dada Maria Goretti Sisiani wa shirika la Dada Wadogo wa Mtakatifu Fransisko Dar es Salaam (LSOF)

Ndiye aliyenipa sakramenti ya kipaimara kati ya vijana 350 katika Parokia ya Msimbazi. Mimi ni kati ya Masista wa kwanza wa shirika la Dada Wadogo wa Mt. Fransisko wa Asizi, Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Tulifika utawani mwaka 1982 na tukaweka nadhiri za kwanza mwaka 1987, wenzangu ni Dada Theopista na Dada Coletha.

Mabinti

Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa ambaye ni mwanzilishi wa Shirika letu naweza kusema namfahamu kama baba na mtu wa watu. Ni baba aliyekuwa na mang'amuzi makubwa kuhusu mahitaji ya Jimbo kuu la Dar es salaam. Hii inajidhihirisha ukiangalia taratibu alizokuwa ameziweka kwa wale ambao wangependa kujiunga na shirika lake changa; walipaswa kuwa wamezaliwa, wamekulia au kusoma hapa jijini. Alitupa sisi wakandidati wa Jimbo Kuu changamoto ya kuishi katika hostel ya Fatima Msimbazi ambapo kwa mambo mengi tulilazimika kujichanganya na wasichana wengine na kubaki katika msimamo wa kitawa.

Alipenda kututembelea mara nyingi sana, aliimba na kucheza na sisi, alitujua kwa sura, majina na hata tulipotoka, yaani sehemu zetu za asili. Mwadhama hakuonesha ubaguzi hata siku moja alitupenda sawa. Mwadhama hata akuone wapi hawezi kuondoka bila kukusalimia hata kama wewe hujamwona atawaambia watu wakuite.

Mabinti

Alizoea kututania sana, kila nilipokutana naye alionesha mwanya wake, akaniambia "mwanangu hebu simama tuone nani mrefu mimi na wewe, nitakununulia geti kwa ajili ya huo mwanya wako." Basi alizoea kututania sana na kutupachika majina ya utani, kwa mfano alizoea kumwita Dada Coletha "Askofu wa kibiti." Kila tulipokutana alirudiarudia kusema maneno haya "Wanangu ninawapenda/ binti yangu ninakupenda sana". Tulimzoea kiasi kwamba tulipomwona kwa mbali tulimkimbilia kama watoto wa chekechea, tulijisikia salama mikononi mwake. Mbele yake hakuna aliyeweza kuhuzunika hata kama ungekuwa na uchungu wa binafsi ulitoweka bila wewe kujua. Alituhimiza kupendana na kushirikiana katika kila kitu.

Mwadhama alionesha uvumilivu mkubwa sana, mara nyingine alipofika kututembelea hakutukuta kwa sababu tulikwenda kuchota maji mbali na hostel, alikaa na kutusubiri hadi tuliporudi kwa vile alijua mwisho wa kurudi ni saa 12.00 jioni. Alizoea kutuletea zawadi yaani chocolate na vitafunwa vingine tulivyozoea kuviita mchezo wa meno.

Alipowaona watu wanaokaa au wanaoishi Msimbazi alizoea kuwatuma watusalimie na aliwapa zawadi watuletee, bado naweza kumwona katika macho yangu Ndugu Peter Keller OFMCap akishusha kapu kubwa lililosheheni mchicha na nyanya, na mara nyingi Fr. Muba aliyekuwa Naibu wake alizoea kutuletea unga wa njano.

Mabinti

Mara nyingi sana alitualika nyumbani kwake Oysterbay. Tulipofika alitupeleka kwenye pango la Bikira Maria mbele ya nyumba yake tukasali pamoja, halafu alituandalia mbuzi, alimleta mbuzi akatuonesha, muda mfupi alichinjwa, masista walioishi naye walitutengenezea kisusio, wakati tukisubiri chakula chote kiwe tayari, tulikaa naye akitusimulia habari za Roma na jinsi anavyotupenda, nyakati zote kutupiga picha za kumbukumbu pamoja, na kutuonesha albamu mbalimbali. Tulikaa kwake tukila na kunywa, kuimba, na kucheza na jioni tulirudi nyumbani. Nyakati hizo zimeweka historia katika maisha yetu na jinsi alivyotupa moyo katika kipindi kigumu ambapo shirika lilikuwa halijapata mwelekeo. Na sisi wenyewe umri wetu ulikuwa mdogo kati ya miaka 15-17.

Mwadhama aliona fahari sana juu yetu, kwa maana alipenda kumsimulia kila mtu juu yetu, akimwonesha picha zetu na kumsisitiza afike kututembelea au hata aliwaleta wageni mwenyewe. Bado nakumbuka marehemu Askofu James Sangu wa Mbeya aliyegeuka kuwa rafiki yetu kiasi kwamba kila alipofika Dar es Salaam alileta mikanda ya video ya watakatifu ili kutuonesha maisha yao, mf. Mt.Maria Goretti, Bikira Maria wa Lourdes, Fatima n.k. Nakumbuka alipotupokea katika hatua ya Upostulanti mwaka 1984 alisema "Wanangu milango ikishafunguliwa haiwezi kufungwa tena, milango ya shirika sasa ni wazi." Hapo ukawa mwanzo rasmi wa malezi ya shirika hapa jimboni. Katika harakati zote za kupata kibali cha kuanzisha malezi Jimboni, daima alikuja kuomba tusali kwa ajili ya kitu alichokwenda kufanya na aliporudi alitushirikisha matukio na mafanikio yote. Alisali na sisi mara nyingi na alituhimiza tuwe watu wa sala.

Mabinti

Kutuletea wageni haikuishia Msimbazi na Mbagala, hata tulipoishi Oysterbay conventini alitutumia rafiki zake wafike kutusalimia, nakumbuka Askofu mstaafu wa jimbo la Bukoba Nkaranga ambaye nilipomfungulia mlango alisema; nimetumwa na Mwadhama nifike kuwaona. Kweli Mwadhama alikuwa mtu wa watu. Hii iliwafanya wengi watuite "Mabinti wa Rugambwa".

Katika Conventi ya Oysterbay tuliishi masista Dada Wadogo watano; hakuweza kuvumilia kukaa wiki nzima bila kumwona hata mmoja. Mara nyingine alisimama dirishani kwake alipotuona bustanini, alipiga simu au aliwatuma masista walioishi nao kutuita, ukifika unamsalimia anakuuliza wenzako wote hawajambo? "Nakurudia neno lake Mwanangu nakupenda, nenda kawaambie wenzako ninawapenda." Kweli tulijisikia salama na ukarimu wake umeacha alama maishani mwetu.

Mwadhama alituhimiza kushirikiana na kuwapenda masista wa mashirika mengine tulipokutana katika umoja wa msista unaojulikana kama " Ujirani mwema." Alitambua na kuheshimu umuhimu wa masista katika kanisa la Tanzania, alizoea kusema "Kama wasingekuwa masista sijui kanisa lingekuwa na hali gani?".

Mwadhama Rugambwa alimpenda sana Bikira Maria na alituhimiza kumpenda sana, katika muda wote wa kutafuta makao ya shirika tulisali sala ya Mt. Yosefu iliyotungwa na kubarikiwa na yeye mwenyewe, na tulimwaomba daima Mama wa Shauri jema kusimamia yote.

Katika kipindi cha mwisho wa maisha yake aliugua sana na mara nyingi tulipopata habari tulikwenda kumsalimia. Mimi na wezangu tulionja jinsi uhusiano wake na Mama Maria ulivyokuwa na nguvu, ilipokaribia tar.15/8/1997 hali yake ilikuwa mbaya sana na kila mtu alifikiri Baba atakufa, siku ilipopita akapata nafuu kidogo, tarehe 4/10/1997 Shirika letu lilitimiza miaka kumi, Mama Paulin na Mama Jeannetti na Dada Wadogo walikwenda kumwona na waliweza kuongea naye ya kutosha.

Nilibahatika kumwona Mwadhama siku 2 kabla ya kifo chake. Mimi na Dada Coletha tulikwenda kumjulia hali, tulikuta amefumba macho lakini alikuwa bado na ufahamu, tulimshika mkono wa kushoto na mwingine wa kulia, tukataja majina yetu alitumia kichwa kutuonesha ishara ya kutufahamu. Tulimsemesha hakuweza kujibu neno bali alitumia ishara kwa kichwa. Tuliondoka na simazi kubwa lakini tukamshukuru Mungu kwa kumkuta hai.Tarehe 8/12/1997 kila mtu alikuwa na mashaka kama tutamaliza sherehe shirikani Mwadhama akiwa hai. Kikundi cha mwisho kilichoweka nadhiri za kwanza mbele yake ndicho kilichokuwa kinaweka nadhiri za maisha siku hiyo. Mwadhama alitupenda hakutaka avuruge sherehe yetu, tulifanya sikukuu yetu vizuri na kuendelea na sherehe hadi saa 4.00 usiku. Baada ya sherehe hiyo Mwadhama Laurean aliaga dunia usiku ule.

Asubuhi tulijihimu mapema kwenda kanisa kuu Mt.Yosef ili kuanza maandamano ya hija kwenda Pugu, hatukukuta mtu, tukapata habari za kifo cha baba, tukashikwa na majonzi makubwa. Kurudi nyumbani mama Paulin na Mama Jeannette walikuwa na habari tayari, wakatupokea na kutufariji, tulisali wote kwenye kikanisa cha nyumba mama baadaye tulikwenda nyumbani kwake. Kweli nyumba ilichukiza, hali niliyozoea kuikuta ilipotea kabisa. Mwili ulipoletwa kanisani St. Joseph, Dada Wadogo hatukuondoka kanisani tukakesha na kesho yake mwili wake, tukausindikiza Uwanja wa ndege, Dada Theopista na Dada Concessa waliusindikiza hadi Bukoba alipozikwa. Tunamshukuru kwa kuwa alituacha katika mikono salama, kabla ya kifo chake, kwa sababu Mwadhama Polycalp Kardinal Pengo alipotwaa madaraka tulianza kumwita Baba na mtangulizi wake tukaanza kumwita Babu. Tunawashukuru wote wanaotusaidia wakienzi kazi yake. Apumzike kwa amani Amina.

Kwa niaba ya Dada Wadogo




Contact Information
Bishop's House Ntungamo,
P.O.Box Private Bag,
Bukoba, Tanzania.
Tel. & Fax. 028 - 2220746
Office: Tel. 028 - 2220194
E-mail: b.officebk@yahoo.com
Website: www.bukobadiocese.co.tz
© Bukoba Catholic Diocese 2023
Find us on
Facebook: Bukoba Catholic Diocese
Twitter:  @bcdcatholic