Mzee huyu alikuwa mtu mtaratibu sana, aliyejiheshimu na kuheshimiwa na watu wengine. Alikuwa mpole, lakini mwenye msimamo. Alipenda ushirikiano na viongozi wa Makanisa mengine bila kuruhusu kupoteza msimamo wa Kanisa lake na heshima ya Kanisa lake. Alikuwa mwangalifu sana katika mazungumzo yake, jambo lililomfanya asiwe msemaji sana , hasa katika mikusanyiko ya watu wengi wa aina mbalimbali.
Pamoja na ushirikiano na viongozi wa Makanisa mengine, kulikuwa na ushirikiano wa pekee na viongozi wa Makanisa ya Anglikana na Lutheran yaliyoko Dar es salaam. Katika ushirikiano huo, Mwenyekiti wetu wa kwanza alikuwa Mhasham Askofu Mkuu John Sepeku wa Anglikan, na baadae alikuwa Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa. Ni katika ushirikiano huo wa pekee Makanisa hayo matatu yaliandaa na kufungua jengo la ibada la pamoja Utete-Rufiji. Wakristo walisali kwa ushirikiano kwa kupishana muda. Pia tukafanikiwa kujenga na kufungua kwa pamoja jengo la ibada Muhimbili. Kila Chaplain alikuwa na ofisi yake katika jengo hilo, ambalo ni mali ya Makanisa haya matatu. Pia tulizungumzia na kuwa na muafaka juu ya viwanja vyetu vya Mafia. Kanisa Katoliki likatoa kiwanja chake kimoja kwa Anglikana. Mwadhama Kardinali Rugambwa alishiriki vizuri ibada za Umoja wa Makanisa ambazo zilifanyika nyakati za Krismas, Paska, na Pentekoste. Nakumbuka kwamba alihubiri mara chache sana katika ibada hizo, ila karibu mara zote aliombwa kutoa baraka ya mwisho na alifanya hivyo. Kwa unyenyekevu wake, wakati wa mikutano ya viongozi wa Makanisa yale matatu tulizunguka kwa zamu katika ofisi za viongozi hao. Kwa kuwa Askofu Mkuu John Sepeku na Mwadhama Kardinali Rugambwa walikuwa wazee walionipita sana kwa umri, nilijisikia kupwaya sana wakati kikao kilipofanyikia katika ofisi yangu. Hapo niliuona unyenyekevu mkubwa wa wale wazee, na nilijifunza mengi toka kwao. Baada ya kifo cha Baba Askofu Mkuu John Sepeku, aliyekuwa mzee mwenzake na Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa, viongozi wa Makanisa ya Dar es Salaam tulimchukulia Mwadhama kama Baba wa viongozi wa Makanisa ya Dar es Salaam. Baada ya kustaafu kwake niliweza kumtembelea mara kadhaa nyumbani kwake, karibu na Kanisa Ia Mt. Petro. Alikuwa akinipokea kwa furaha na uchangamfu wa pekee, hata wakati mwingine akinitembeza katika bustani yake ya migomba ambayo aliipenda sana. Naamini ndivyo alivyofanya kwa wageni wake wote waliomtembelea pale nyumbani kwake. Kama nilivyoandika juu, Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa hakuwa mzungumzaji sana katika vikao, lakini kila alipozungumza alitoa maneno yenye uzito ambayo hayakuwa rahisi kupingwa. Hivi ndivyo mimi mlivyomfahamu Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa kwa kipindi nilichoshirikiana naye. Askofu Mstaafu Elinaza E. Sendoro