Kama Biblia isemavyo, ni kweli kuwa maisha ya binadamu hapa duniani hupita kwa kasi kama upepo. Na mara nyingi mtu husahahulika upesi na umaarufu wake ustaafu pamoja naye. Lakini jambo la ajabu ni kwamba baadhi ya watu waliogusa maisha yetu hasa ya utotoni hata katika mambo madogo yaliyoonekana kuwa ya kawaida sana bado kumbukumbu nzuri za maisha yao bora huchora alama isiyofutika moyoni na akilini mwetu.
Mmojawapo wa watu niwakumbukao na kuwaenzi sana ni hayati Baba Mwadhama Laureani Kardinali Rugambwa. Alipoteuliwa na kutawazwa kuwa Baba Askofu wa "Lower Kagera," mwaka 1952 nilikuwa kijana chipukizi wa miaka kumi na mmoja. Wakati huo mimi na vijana wa lika langu tulikuwa wapenzi bingwa wa kutumikia misa takatifu kila siku ambayo enzi hizo iliadhimishwa katika lugha ya Kilatini. Nasi tulikiporomosha Kilatini bila hitilafu rafiki yangu; hali hiyo ilitupa nafasi nzuri ya kuwa watumishi bora na hasa kutuwezesha kutumikia misa za sherehe maalum tulizozishabikia sana, mfano, Krismasi na Pasaka. Tulichopania zaidi ilikuwa kubahatisha kuteuliwa angalao mara moja kuwa mtumikiaji wa Misa kuu, huku ukilishikilia joho lefu la kiaskofu lililokuwa likivaliwa na Askofu Rugambwa wakati wa maandamano. Joho hilo lililoitwa kwa lugha ya Kilatini "Capa Magna" lilijivuta kwa nyuma urefu wa mita kama tano sita hivi. Sijasahau nilivyokuwa nafurahia kuvutana na joho hilo nikinyatia kwa nyuma kila alipoelekea Baba Askofu akiwabariki waumini. wakiwa wamepiga magoti na kufanya ishara ya msalaba hadi alipofika altareni. Kana kwamba hiyo haikutosha niliendelea kusindikizana nalo pindi aliporudi sakristia baada ya ibada. Na ule urefu na miondoko ya madaha ya Baba Rugambwa vilinogesha miondoko yetu na kuyapendeza macho hasa macho ya watoto; yaani ungedhani ni tausi mzuri akiongozana na kifaranga chake. Vivutio vingine nivikumbukavyo enzi za Mwadhama Rugambwa akiwa Askofu wa Rutabo ni kwamba ilikuwa kama kanuni, siku za likizo ndefu na fupi za shule, kila asubuhi baada ya misa tulikwenda kumwamkia Baba Askofu Rugambwa. Mwadhama alikuwa akitokezea midhilini ya twiga mzuri, uso wake ukingara kwa tabasamu lililojaa upole wa kibaba na ustarabu, nasi tulianguka magoti pake kumsalimia kwa furaha kubwa tukisubiri kutunukiwa zawadi nono toka kwake ambazo zilikuwa ni "pipi" na "kamwani" (chembe za kahawa zilizopikwa na kukaushwa) zilizofuatiwa na baraka yake. Wakati mwingine alikuwa akitupatia medali na sanamu za watakatifu au rozari za kuwapelekea wazazi wetu. Mara tulitimua mbio kwa furaha kubwa tukielekea nyumbani ambako lilikuwa gumzo na wazazi na majirani jinsi tulivyopokelewa na Baba Askofu Rugambwa. Uhusiano na Baba Askofu wetu huyo ulindelea kukomaa na wala hatukuchokana. Nakumbuka siku moja alituuliza: "Nani kati yenu angependa kuwa padre?" "Ninahitaji mapdre wa kupadrisha." Sote tulinyosha mikono juu tukisukumana mbele yake kwa mashindano makali tukijibu "ni mimi" "ni mimi baba" huku yeye akitabasamu tu. Huenda cheche za mwanzo za wito wangu wa upadre zilianzia pale, hiyo ni hadithi nyingine. Mpenzi msomaji ukweli nina kumbu kumbu nzuri nyingi za baba yetu Mwadhama Kardinali Rugambwa lakini nimeona ni vyema nikuonjeshe kidogo uhondo unaoendelea kunogesha kumbukumbu zangu kwake, si ajabu kuna wengine wenye kumbukumbu nyingi kunizidi. La maana zaidi nililojifunza kwake, ni kuwa alikuwa Mcha Mungu. Mpenzi wa Mungu na Mametu Bikira Maria na watu wa aina zote, mstarabu, mkarimu, mwenye hekima na busara ya hali ya juu.. Baba Rugambwa aliheshimu hata watoto wadogo kiasi kwamba hata nami nikavutiwa kuwa padre kama yeye tangu nikiwa mtoto mdogo. Ukaribu wake na watu wa kawaida ulionyesha karama ya ubaba aliyokuwa nayo. Yeye alipigana vita iliyo njema, alikamilisha vema safari yake hapa duniani kwa kuniachia kumbukumbu kibao na changa moto pia. Inabidi nimuenzi kwa kuiga mfano wake. Ninapiga makasia kwa moyo mkuu nikijaribu kufuata nyayo zake bila kurudi nyuma. Waswahili walisema "Mwenda pole hajikwai akijikwaa haumii. Buriani tena Baba. Upumzike kwa amani kwani wahenga walisema: "Chanda chema huvikwa pete." Baba Rugambwa nitakuenzi milele.
Msgr. Deogratias Rweyongeza BishotaRoma na Aachen Mazingira yaliyoniwezesha kumfahamu vizuri zaidi Kardinali Rugambwa ni Roma wakati niko masomoni, na baadaye mwaka 1996 nilipomsindikiza katika safari yake ya mwitikio kwa mwaliko wa Baba Mtakatifu Yohane Paulo II kwenye Yubilei yake ya dhahabu ya Upadrisho.
Inafahamika kwamba miaka michache baada ya upadrisho, Rugambwa alipelekwa Roma kusoma. Alipopewa ukardinali akiwa Kardinali wa Kwanza Mwafrika, Collegio San Pietro Apostolo, mahali alipokuwa akikaa kama mwanafunzi ililipokea tukio hilo kama heshima ya pekee kwa taaasisi yenyewe. Hivyo taasisi hiyo ikatenga nyumba kubwa kwenye horofa na kumzawadia Kardinali iwe mahali pake pa kufikia wakati wowote alipotembelea Roma. Nilipokuwa masomoni nilikuwa ninakaa siyo tu katika mazingira ya Taasisi ya Collegio san Pietro Apostolo, bali pia kwenye orofa yenye nyumba ya Mwadhama. Hivyo kila alipokuwa anakuja Roma, nilikuwa kwake jirani wa karibu na msaada wa haraka, hasa ikizingatiwa kwamba wakati huo kipindi chake cha uzee kilikuwa kinaanza kubisha hodi. Ilikuwa wakati wa mojawapo ya safari zake Roma aliponikaribisha nimsindikize Aachen nchini Ujerumani. Hii ilikuwa safari ya kikazi. Shughuli zake huko Aachen zilionyesha wazi kwamba hata katika uzee tamaa yake Mwadhama ilikuwa bado ni kujaribu kwa uwezo wake wote kuinua hali ya watu wake kiroho na kimwili. Wakati huu ndoto yake ilikuwa kuboresha makao ya masista wa Shirika jipya la Masista wa Jimbo Kuu Dar es salaam, na kupanua Hospitali ya Ukonga kwa ajili ya huduma za afya kwa wananchi. Shughuli alizofanya na mazungumzo aliyonishirikisha kipindi cha safari hiyo vilinifanya nikumbuke methali moja isemayo, "Usione vyaelea, vyaundwa". Ilijitokeza wazi kwamba uwajibikaji kwa ajili ya kondoo una gharama zake ambazo ni pamoja na jasho na kujitoa mwenyewe sadaka kama mtumishi hasa. Baadhi ya Mambo niliyojifunza kwa Mwadhama Kardinali Rugambwa Nikiyaunganisha mambo mbalimbali yaliyojitokeza ningeweza kutoa muhtasari ufuatao juu ya Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa:
Imani kwa Mungu na ibada kwa Bikira Maria: Aliamini kwamba uhai na mafanikio yetu vimo mikononi mwa Mungu. Katika safari nilizosafiri naye, kila ndege yetu ilipoanza kuondoka alifanya ishara ya msalaba na kuanza kusali angalau fungu moja la Rozari.
Utii, unyenyekevu na heshima: Licha ya cheo chake, Kardinali Rugambwa hakupenda hata mara moja kwenda kinyume cha miongozo au maelekezo ya viongozi wa jumuiya iliyomkaribisha. Niliuchukulia mtazamo wake huo wa maisha kama kielelezo cha imani yake katika umuhimu wa utii, unyenyekevu na heshima maishani.
Ubinadamu na Msamaha: Alikuwa na ujasiri wa kuomba msamaha hata kwa mdogo wake bila kujali cheo chake iwapo angehisi kwamba labda amekukukosea.
Sadaka: Alifurahi kujitoa sadaka kwa kuwasumbukia wengine. Mfano, haikuwa rahisi kwake kupata misaada ya kuleta maendeleo kwa watu aliokabidhiwa kuwahudumia. Jitihada alizopitia kuweza kujenga shule, hospitali n.k. mara nyingi zilimuacha amechubuka. Lakini, alifanya, kwa sababu njia za mkato za kuweza kuwasidia watu hazikuwepo.
Baada ya kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Dar es salaam Mwadhama na msindikizaji wake walionyeshwa chumba cha Wasafiri Maalum (VIP) wakati wanasubiri mizigo yao au usafiri. Huko wakakutana na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wakati ule, Mheshimiwa Jakaya Kikwete. Mwadhama na Waziri waliketi pamoja wakawa wanazungumza huku wakisubiri hatua zinazofuata katika mipangilio ya safari zao. Sijui kama wakati huo hawa wawili walikuwa wameishawahi kuketi karibu hivi kwa faragha. Wakati fulani katika mazungumzo yao yaliyoonekana wazi kutawaliwa na furaha pande zote mbili, Mwadhama Kardinali akawa anamsifu Waziri kwa kazi nzuri aliyokuwa anafanya, naye Mheshimiwa Kikwete akamjibu Mwadhama, "Sisi tunajega katika misingi mliyoweka nyinyi".
Rugambwa, Kardinali wa kwanza Mwafrika, ameliachia jina taifa letu na wala siyo taifa letu tu bali pia bara zima la Afrika. Lakini kumbukumbu kubwa zaidi aliyoacha nyuma yake kama kiongozi ni bidii pamoja na busara ya kuitangaza imani kwa maneno na hasa kwa matendo kwa watu wote.
Mungu apende kumjalia pumziko la milele mbinguni. Amina.
Fr. Stanislaus Mutajwaha.
Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa
Na Padre Felician Rwehikiza
(Pd.Felician Rwehikiza anatoka parokia moja na Kardinali Rugambwa na alikuwa katibu wake wa kwanza alipohamia Jimbo kuu la Dar es Salaam).
Mwendapole, mrefu katika warefu wa mstari wa mbele, wa umbo la kupendeza kulingana na urefu wake, sura ya wengine kuwa na shaka kama ni mzungu au Mwafrika, aliyerishari busara na hekima, kumwona ilikuwa kumpenda. Huyo si mwingine bali ni Mwadhama Kardinali Laurian Rugambwa. Kwangu alikuwa Baba. Babu yangu na baba yake walikuwa marafiki wakubwa na, isitoshe, alipewa jina "Laurian" na babu yangu. "Nimpe jina gani," baba yake alimwuliza babu yangu, "mpe jina langu, Laurian, Babu alijibu. Kwa kuwa pia alisoma pamoja na baba yangu seminari Rubya, ilikuwa rahisi kunitambua kutokana na kujua fika familia na ukoo wa babu. Ilitokea kwa bahati. Mwezi Januari, mwaka 1952 nilijiunga na Seminari Ndogo (Preparatory Seminary), Bunena, Vikariati ya Bukoba, lakini kabla ya mwisho wa mwezi huo nilishindwa ugali nikarudi nyumbani. Wazazi walipokuwa wanashughulikia usajiri wangu tena, Shule ya Msingi ya Rutabo, nilipokuwa nimetokea kwenda seminari ndipo tukio maalumu na la kihistoria Tanganyika lilipotokea, uaskofu wa Padri Laurian Rugambwa, 10 Februari, 1952 Parokiani Rutabo. Ilikuwa bahati ya pekee kwangu kushuhudia tukio hilo lililojumuisha wageni kutoka ndani na nje ambao nisingalibahatika kuona. Baada ya tukio hilo, siku moja nilitumwa na Baba hapo Rutabo parokiani. Nikiwa pamoja na watoto wengine wanne kwenye eneo la kanisa, alitokea Askofu mpya, Rugambwa, kutoka nyumba ya mapadri tukamjongea kumsalimu. Kila mmoja wetu alimsalimu na kujitambulisha. Zamu yangu ilipofika, baada ya kujitambulisha aliniuliza nilikuwa nafanya nini hapo kwani alikuwa na habari kuwa nilikuwa nimejiunga na seminari. Nilikosa jibu, lakini mambo hayakuishia hapo. Alifuatilia. Baadaye kidogo, Paroko wetu, Padri Primus Kabyemera, aliwaita wazazi wangu; hawakujua alichowaitia. Waliporudi nyumbani waliniomba tu nifikirie tena kuacha kwangu seminari. Sikuwa na la kufikiria, niliwaambia tu, "Basi nitarudi,". Paroko alinipa barua, nikarudi Seminari Bunena, nikapokelewa tena. Niko hivi, padre, kwa sababu ya kuingilia kati Mwadhama Kardinali Rugambwa. Mungu ana njia zake, na huo ulikuwa ufunguo wa kuwa karibu naye. Mwaka 1968 Mwadhama kuhamishiwa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Askofu Gervase Nkalanga aliyechukua nafasi ya Mwadhama kama Askofu wa Bukoba, alinipa ujumbe kuwa Mwadhama alimwomba nimfuate kumsaidia huko Dar es Salaam. "Jiandae na kuondoka mapema iwezekanavyo" aliniambia. Tangu mwanzo Mwadhama alinitayarisha na akanishirikisha katika yote na kuniamini (trust) katika majukumu aliyonipa. Alikuwa mfuatiliaji na mshauri mzuri wa yote niliyokuwa nafanya na ya wengine katika idara na taasisi mbali mbali jimboni. Katika majukumu yangu hasa nakumbuka shughuli za kupanga mambo yetu ya kazi katika mazingira mapya ya Jimbo Kuu la Dar esSalaam, hususan hapo St. Joseph's Cathedral tukiwa Waafrika peke yetu kati ya jumuia ya Makapuchini; kushughulika na Wizara ya Mambo ya Nje kwa ajiri ya Diplomatic Passport, uwekaji wa bendera ya Vatican kwenye gari lake, n.k. Katika haya na mengine Mwadhama alikuwa ananipa moyo na maelekezo. Katika JimboKuu la Dar es Salaam tulimoingia mazoea ya uongozi wa kikapuchini au niseme ya kizungu hayakurahisisha kutoa maelekezo kwa baadhi ya wadau kadiri ya nafasi na majukumu yangu lakini alinifariji kweli na kunielekeza namna ya kufanya kazi katika mazingira hayo, akinipa mifano ya yaliyokwisha msibu yeye mwenyewe katika wadhfa wake. Alinielewa fika, aliniamini. Nilikuwa kama mwanae hivyo baada ya mlo wa jioni, mara nyingine tuliongea hadi kama saa nne na nusu. Maongezi yenyewe kwa kawaida yalihusu mambo ya maisha ya kawaida. Jioni moja, kati ya mengine, alikumbuka watu wa rika yake nyumbani, kijijini kwake, Bukongo, na hali walizokuwemo akaniuliza, "Mwanangu," unafikiri ningalikuwa na hali gani mwenyewe kijijini? Ningaliweza kujumuika na wengine nikiwa na kibuyu cha rubisi kwa fulani au kwangu? Sijui ningalikuwa mtu wa aina gani kijijini. Naona ningalikuwa mtu wa hivi hivi tu." Baba yangu alinipa na kunifundisha upendo. Alinifundisha uchungaji. "Katika kutatua matatizo ya waumini," aliniambia, "mbali na sheria na mengine, jiulize Kristu angalikuwa hapa angalisemaje, angalifanyaje?" Alinifundisha manejimenti, kupanga na usafi wa ofisi, mengi ya kiroho, n.k. Nilivyojisikia nikimwacha sasa baada ya kuwa naye muda mfupi mara ya mwisho hapa duniani, siwezi kuelezea.
Pd. Felician Rwehikiza