Header

Msgr.Mbiku: Kardinali Rugambwa alikuwa Mkweli, Muwazi na Mwenye Haki

Mbiku

Alikuwa mkweli, muwazi na mwenye haki, Mnyenyekevu na mtu wa sala

Na Msgr. Deogratias Mbiku
(Msgr. Mbiku alikuwa mmoja wa mapadre wake wa kwanza wazalendo DSM na akawa katibu wake)

Nilianza kumfahamu Mwadhama Laurian Kardinal Rugambwa, mwezi Julai, 1969, riilipolazwa katika hospitali ya Muhimbili, baada ya kupata ajali mbaya ya gari. Nililazwa jengo la Kibasila. Alipokuja asubuhi kuniangalia, aliwaagiza wauguzi wanihamishe na kunipeleka wodi ya daraja la kwanza. Kwa sababu hali yangu ilikuwa mbaya - nilikuwa kifoni -, walimshauri Mwadhama nisihamishwe, kwani nilikuwa nakufa; hivi haingekuwa vema kugharamia fedha nyingi kwa ajili ya mfu. Lakini yeye alisisitiza nihamishwe.

Rugambwa

Nikahamishwa. Mchana ndugu zangu walikuwa wa kwanza kuja kuniangalia. Wakaulizia hali yangu na kuambiwa nimefariki. Walikwishazungushia pazia kile kitanda, bila kujua kwamba kumbe aliyekufa ni mgonjwa mwingine aliyelazwa baada ya mimi kuhamishwa. Baada ya kitambo alifika Mwadhama. Baba yangu mdogo alimwendea kabla hajaingia wodini na kumwambia kwamba nimekwishaaga dunia. Mwadhama aliomba kuonana na Mkuu wa Wodi ile na kumwuliza iwapo agizo lake lilitekelezwa, la kunihamishia daraja la kwanza. Mwadhama alijibiwa kwamba nilikwishahamishwa na kupelekwa Wodi Namba 16, kitanda Na. 5. Wakaja na kunikuta ningali hai.

Kwa tukio hili niitambua kuwa Mwadhama alijali sana wenye shida bila kuwa mbanifu au bahili wa gharama. Alijali utu zaidi kuliko mali. Alijawa na huruma na wema kwa watu, hasa wenye shida.

Nimemfahamu vizuri zaidi baada ya mimi kuteuliwa kuwa Katibu wake, mwaka 1972. Kwanza nilihofu sana na kujisikia mnyonge. Padre kijana wa mwezi mmoja tu, kuwa Katibu wa mtu mwenye wadhifa mkubwa vile. Wasiwasi wangu ilikuwa ningeishije na mtu kama huyu.

Hofu na unyonge wangu vilitoweka baada ya muda si mrefu sana. Nilitambua kwamba si mtu mwenye makuu; bali ni mtu anayeweza kuishi na watu wa rika na hali yoyote. Kwangu alikuwa BABA mwenye kumwelewa mwana na kumchukulia alivyo. Nikikosea au kukosa, alitumia busara na upendo katika kunisahihisha na kunirudi. Tulikuwa na gari la ofisi, Peugeot 304. Lakini mara kwa mara tulitumia gari aina ya Renault 4, gari la kimaskini alilowanunulia Masista kwa ajili ya kwendea sokoni. Mara nyingi aliendesha mwenyewe gari la ofisi kutoka maskani kwake, Oysterbay, hadi ofisini, St. Joseph's na kurudi.

Ofisini hakuwa na ubaguzi wa aina ya watu wa kuonana naye. Watu wa rika zote, wenye elimu nyingi au ndogo, wenye vyeo na wa kawaida, wenye akili timamu na punguani au vichaa, wote hao aliweza kuwamudu.

Rugambwa

Sifa kuu aliyokuwa nayo katika shughuli za ofisi na nyinginezo ni KUWAHI (puncutuailty). Alijua kushika muda na kwenda na wakati. Hii nimejifunza sana kwake. Sifa nyingine aliyokuwa nayo ni upole. Alipokasirika hakufoka wala kuonyesha jazba; bali alitulia na kutafakari la kufanya. Ilipombidi aseme, alisema kwa upole na utulivu. Lakini mara nyingi alinyamaza na kuongea baadaye sana baada ya kutulia.

Aidha alikuwa mkweli, muwazi na mwenye haki. Alipoona kosa, hakulifumbia macho, bali alikosoa, ila bila jazba; badala yake alifanya hivyo kwa upendo, kwa lengo la kumsahihisha na si kumkashifu au kumdhalilisha mtu. Alijali sana utu wa mkosefu. Alikuwa na hekima na busara ya lini aseme nini na kwa nani. Kwa maneno mengine alijizuia sana kuwa kikwazo au kuleta vikwazo kwa wengine; hasa akijua kwamba kwa hadhi na cheo chake watu wengi walimwangalia kwa namna ya pekee.

Kadiri nilivyomwelewa, naye kunielewa, niligundua kuwa ni mtu aliyeweza kufanya na kupokea mizaha na vichekesho. Alikuwa na kipaji au karama ya kuwatambua watu walivyo na kuwachukulia hivyo: wenye akili na wapumbavu; wenye hasira na wapole; wenye busara na waropokaji. Jambo lingine ni kwamba alikuwa mtu wa sala; hususan breviary, rozari, Misa takatifu, na ibada hasa kwa Bikira Maria. Alinitolea mifano ya watu mbalimbali: Mapadre na watawa walioanguka na kuishi katika upotofu kwa sababu ya kuzembea sala; na wale waliobaki imara kutokana na sala. Nimejifunza vizuri jambo hili kwake na linanisaidia sana.

Aidha alikuwa mnyenyekevu. Si tu hakuwa na makuu, bali pia aliweza kuishi kikawaida, bila ya kujiona kwamba yeye ni kiongozi mkubwa katika Kanisa.

Rugambwa

Katika shughuli za kichungaji alijitahidi sana kuwapata mapadre na watawa wa kufanya kazi humu Jimboni. Kwa kuwa Jimbo Kuu la Dar es Salaam lilikuwa na mapadre wazalendo wachache sana, alijibidisha kuwapata mapadre wazalendo kutoka majimbo mengine Tanzania. Hivi alipata mapadre kadhaa kutoka Jimbo la Songea (siku hizi Jimbo Kuu la Songea na Jimbo la Mbinga). Pia alipata mapadre kutoka Jimbo la Moshi na Jimbo la Bukoba. Zaidi ya hayo, aliyaomba Mashirika ya Kitawa ya kiume na kike kupeleka watenda kazi katika Jimbo hili Kuu la Dar es Salaam. Baadhi ya Mashirika hayo ni haya yafuatayo: Wamisionari wa Afrika (M.Afr.); Mitume wa Yesu (A.J.), Shirika la Roho Mtakatifu (0SS); Shirika la Wakamiliani; Shirika la Wakonsolata; Shirika la Wasalvatoriani; Shirika la Damu Takatifu ya Yesu; Shirika la Waselesiani (Don Bosco); Shirika la "Brothers of Christian Instruction".

Kwa upande wa Watawa wa Kike: "White Sisters"; "Cannosian Sisters"; Ivrea Sisters; Holy Union Sisters; Missionaries of Charity (Mama Tereza); Salesian Sisters; Sisters of Charity of St. Charles Borromeo; Carmelite Missionary Sisters; Salvatorian Sisters; Masista wa Mahenge, Masista wa Kilimanjaro; Masista wa Mt. Teresia wa Mtoto Yesu (Bukoba); Masista wa Mt. Gemma na Daughters of St. Paul.

Rugambwa

Katika jitihada zake za kuwa na watenda kazi wazalendo, alianzisha Seminari Kuu ya Segerea; lakini tangu mwanzo aliwahusisha Maaskofu wenzake wa Tanzania. Hivyo, ikawa seminari kuu ya taifa. Ila ni yeye Mwadhama aliyeshughulikia kutafuta kiwanja, upimaji na ujenzi. Aidha alianzisha seminari ndogo ya Jimbo iliyopo Visiga. Pia ameanzisha Shirika la Masista wa Jimbo, Dada Wadogo (Little Sisters of St. Francis of Assisi).



Katika nyanja ya Elimu: alianzisha Shule ya Sekondari ya Mt. Antoni, Mbagala, chini ya hayati Padre Fidelis Aversari.

Katika nyanja ya Afya: aliwahimiza Masista wa Mashirika mbalimbali kujenga na kuendesha Zahanati Jimboni. Baadhi ni hizi zifuatazo: Chang'ombe, Yombo, Kawe, Tegeta. Hatimaye alijenga hospitali ya Jimbo, Ukonga.

Katika nyanja ya Mawasiiano: kulikuwa na gazeti la Jimbo (bulletin) lililoitwa: "Jimbo Kuu", chini ya Mkurugenzi wa Msimbazi Senta. Hatimaye akaanzisha kituo cha Radio - Video Tumaini.

Msgr. D.H. Mbiku




Contact Information
Bishop's House Ntungamo,
P.O.Box Private Bag,
Bukoba, Tanzania.
Tel. & Fax. 028 - 2220746
Office: Tel. 028 - 2220194
E-mail: b.officebk@yahoo.com
Website: www.bukobadiocese.co.tz
© Bukoba Catholic Diocese 2023
Find us on
Facebook: Bukoba Catholic Diocese
Twitter:  @bcdcatholic