Header

Askofu Amedeus Msarikie:
"Ukardinali wa kweli, na kutoka Afrika, ndio huu"

Askofu Msarikie:   Nilivyomfahamu Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa


Aliteuliwa awe kionyesho cha hadhi ya Kardinali, watambue kuwa "Ukardinali wa kweli, na kutoka Afrika, ndio huu" (Askofu Amadeus Msarikie - Jimbo la Moshi).

Maandishi yafuatayo ni masimulizi juu ya mtu niliyemfahamu kama Baba na Rafiki katika Kanisa. Haya ni maoni yangu juu ya Baba wa Kanisa ambaye nilimheshimu sana, ninamshukuru kwa mfano wake mzuri kama Kiongozi wa Kanisa, - Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa.



Nilianza kusikia jina "Rugambwa" nikiwa najifunza Teolojia katika Seminari Kuu ya Kibosho. Tuliarifiwa na wakubwa wetu kwamba Baba Mtakatifu Yohane wa Ishirini na Tatu amemteua Askofu wa Bukoba Laurean Rugambwa kuwa Kardinali wa kwanza Mwafrika, tena Mwafrika mweusi. Tuliambiwa kuwa uteuzi huu umefanyika Mwezi Machi 1960. Habari hizi zilitushangaza na kutufurahisha sana, ingawa hatukuwa tumeelewa hadhi ya Kardinali na ukaribu wake na Papa ni nini. Tulibaki tunashangaashangaa tu. Sababu zilikuwa nyingi.

Mosi, majimbo ya Tanganyika wakati ule, karibu yote yalikuwa chini ya Maaskofu wamisionari Wazungu. Mara kwa mara tulikuwa tunasikia kuwa kuna askofu mmoja rnweusi aitwaye Joseph Kiwanuka wa Uganda. Huku kwetu Moshi ilikuwa ndiyo tu tumempata Askofu wa kwanza mzalendo, Mhashamu Askofu Joseph Kilasara. Lakini ingawa alikuwa mzalendo bado alizungukwa na wamisionari wengi wa nchi za kigeni hivyo kwamba jimbo letu bado lilikuwa linanukia umisionari na "uzungu-uzungu." Haikuwa rahisi kufikiria Mwafrika kuwa Kardinali. Hadhi hiyo ilikuwa juu mno kufikirika kwa mawazo yetu.

Shida nyingine ya wakati ule ni kwamba ukoloni ulikuwa umekolea hivyo kwamba tulikuwa tunajisikia wanyonge sana na duni kama Waafrika. Ni kweli kuwa mwaka 1960 TANU ilikuwa imepamba moto katika kupigania uhuru chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Hata hivyo hatukuamini kuwa heshima walizokuwa wanapewa Wazungu zingekuja kuwa za Mwafrika; waje watu weusi waketi na kutulia kwenye viti vya madaraka kwa haki bila kuonekana kama wanaigiza tu.! Hii ilikuwa kasumba ya ukoloni.

Katika historia tulisoma kwamba Ghana imepata uhuru na kujitawala yenyewe ikiongozwa na mtu maarufu aitwaye Nkwameh Nkrumah. Huyu Nkrumah alionekana kwetu kuwa mtu wa ajabu sana, mtu ambaye amewatiisha Wazungu mpaka wakampa heshima ya kutawala nchi. Basi katika dhana za aina hii juu ya watu mashuhuri wa Afrika ya wakati ule, tulimlinganisha Mwadhama na hao mashujaa wa Afrika ya zama zile. Tuliwaona ni watu waliopelekwa na Mungu kwa malengo ya kipekee —kama Manabii au wakombozi. Waingereza wanasema "Men of Destiny" au "Charismatic Leaders."



Rugambwa na Papa

Hivyo huyu Kardinali wa kwanza Mwafrika katika historia ya Kanisa Katoliki amechaguliwa na Mungu kwa namna ya pekee kabisa — yeye peke yake katika Afrika nzima! Tulimwaza kama mteule wa Mungu.


Nilibahatika kumfahamu Mwadhama zaidi na kuwa karibu naye tangu nilipowekwa wakfu kuwa Askofu wa Moshi Mel 1, 1986.

Wakati huo ndiye alikuwa Askofu Mkuu wa Kanda ya Mashariki ambayo Jimbo Katoliki la Moshi lilikuwa sehemu yake. Makao makuu ya Kanda hii yalikuwa Dar es Salaam. Kutokana na taratibu za Kanisa Mwadhama ndiye alinikabidhi Kanisa Kuu Ia Jimbo, Aprili 30, 1986. Hali kadhalika, ndiye aliyekuwa Kiongozi wa pili katika ile Misa ya kuniweka wakfu; wa kwanza akiwa ni Mwadhama Jozef Kardinali Tomko, na wa tatu akiwa ni Maurice Kardinali Otunga wa Nairobi. Kwa mpango wa Mungu hawa wababa watatu ndio wameniingiza katika mlolongo wa kupitishiwa "madaraka ya kitume" (apostolic succesion).



Baada ya tukio hilo, nilipata fursa pana zaidi ya kumfahamu Mwadhama katika mikutano ya Maaskofu hasa kupitia Kamati Tendaji za Baraza Ia Maaskofu Tanzania. Uwepo wake katika mikutano daima ulileta heshima ya ziada katika vikao vyetu. Daima aliwahi katika mikutano kwa wakati, na hakukosa kikao isipokuwa kwa sababu kubwa, kama vile safari zake za kikardinali. Kwa kweli hapo tulipata bahati ya kutambua hekima ya Mzee wa Kanisa -— Baba wa Kanisa, mtu mwenye mang'amuzi ya ulimwengu na mwenye roho ya kimungu.

lngawa hakuwa mtu wa kusema maneno mengi, tuliweza daima kuhisi uwepo wake ambao ulifanya mambo mengine yajirekebishe yenyewe yaende kwa utaratibu unaotakiwa.

Tungeweza kuuliza swali: Mtu aliyemfahamu Baba Kardinali Rugambwa, angebaki na picha ya namna gani akilini mwake? Kwanza, ni liIe umbo lake la mtu mrefu, mwembamba anayejichukua kwa heshima inayomkaa; mtu wa nafsi tulivu inayoangaza ukuu wa ndani. Mtu aliyemfahamu alimwona kama mtu aliyezaliwa awe mtu mkubwa; awe na heshima aliyoandaliwa na Mungu kwa ajili ya Kanisa, — mtu mashuhuri wa Kanisa. Karibu tuseme Mungu alikuwa amemnuia awe Kardinali; naye Mwadhama akapokea mwelekezo huo kamili; akauishi kwa ukubali wote, ukawa sehemu ya nafsi yake. Kwa yakini alisimama na kujistahi kama Kardinali mpaka mwisho wa maisha yake, Desemba 8, 1997.

Kuhusu tulivyomwona katika imani yake, alionekana mtu mwenye imani nzito iliyomfanya aishi kwa utulivu sana licha ya majukumu mazito ya Uaskofu na Ukardinali. Mwadhama alimtegemea sana Mama Bikira Maria. Mara kwa mara alipomalizia sala ya kufungua au kufunga mkutano, alisikika akitamka sala ya mshale aliyoizoea: "MATER BONI CONSILII" Hakuna shaka kwamba Mama wa Mungu alikuwa mshauri wake mkuu.

Mwadhama alikuwa mtu aliyejisimika imara katika utamaduni wake wa kuzaliwa. Hii ilionekana mara nyingi alipokutana na wazaliwa wa Bukoba ambapo, kama vile kufuata silika, walianza kuzungumza katika lugha yake ya kuzaliwa ya Kihaya. Huenda Mwadhama alijifunza misingi ya Dini katika lugha yake ya kuzaliwa hivyo kwamba tangu utoto lugha yake ya asili imekua naye popote alikokwenda.

Nakumbuka siku moja nyumbani kwake alinipa punje za kahawa zilizokaangwa ili nitafune. Kumbe kutafuna kahawa ya namna hiyo ni heshima anayopewa mgeni katika utamaduni wa Kihaya. Nami nilitafuna punje za kahawa kama Mangi wa Kihaya!

Je, tumkadirie Mwadhama Laurean Rugambwa namna gani, au tumweke katika kundi la watu wa aina gani? Katika historia ya wanadamu kuna watu wanaopelekwa na Mungu huku duniani kwa malengo maalumu ya kijamii au ya Mungu mwenyewe. Ni kama mapandikizi shujaa katika historia ya wanadamu. Karne yetu iliyopita ina watu kama Mahutma Gandhi na Uhuru wa India; Julius Kambarage Nyerere na Uhuru wa Tanzania na Afrika nzima; Yohane wa lshirini na Tatu na Vatikano ya Pili; Yohane Paulo wa Pili — Papa wa Karne ya Ishirini na Moja; na wa Dunia Nzima. Mama Teresa wa Kalkuta -— Mpenda Maskini wa Wamaskini.

Mwadharna Kardinali Rugambwa aliwakilisha Afrika na watu weusi katika Kanisa Katoliki na katika ramani ya ulimwengu. Alikuwa kama bendera iliyowekwa juu ya mlingoti ili kila mtu aione, na ionyeshe kuwa watu weusi wanastahikika katika Kanisa na katika ulimwengu. Changamoto kwake ilikuwa awe hicho kitu kinachoitwa "Kardinali." Aliteuliwa awe kionyesho cha hadhi ya Kardinali, ulimwengu na Afrika nzima ukubali kuwa "Ukardinali wa kweli, na kutoka Afrika, ndio huu"



+Amedeus P. Msarikie Askofu wa Jimbo la Moshi

Contact Information
Bishop's House Ntungamo,
P.O.Box Private Bag,
Bukoba, Tanzania.
Tel. & Fax. 028 - 2220746
Office: Tel. 028 - 2220194
E-mail: b.officebk@yahoo.com
Website: www.bukobadiocese.co.tz
© Bukoba Catholic Diocese 2023
Find us on
Facebook: Bukoba Catholic Diocese
Twitter:  @bcdcatholic