Header

Alikuwa na Moyo wa Dhahabu: Askofu Nkalanga

Nkalanga Bp

Nilivyomfahamu mzee wetu Kardinali Rugambwa

"Alikuwa na moyo wa dhahabu"
Na Askofu Gervasius Placidius Nkalanga OSB

(Askofu Mstaafu wa jimbo la Bukoba ambaye sasa mzee wa miaka 93 ni mmonaki Mbenediktini. Alifanya kwa karibu na kardinali Rugambwa miaka 7 kama katibu wake wa elimu na miaka 5 kama askofu msaidizi).

Mwezi Novemba 1951, Rugambwa alirudi kutoka masomoni Roma. Alifika Kashozi kumwona Mheshimiwa sana padre Verdaasdonk W. F. ambaye alikuwa msimamizi wa Vikariati ya Bukoba. Kwani Askofu wa Jimbo Mhashamu askofu Laurence Tetrault alikuwa amefariki muda si mrefu huko kwao Canada, wakati wa kupasuriwa saratani ya kichwani. Mimi wakati ule nilikuwa Kashozi kama paroko msaidizi.

Padre Laurean Rugambwa alipangwa Kashozi kusaidia. Padre Laurean alifika Kashozi siku 2 au 3 kabla ya Krismas ya 1951. Alipangwa kwenda kuhudumia kigango cha Katoma, Padre Huwiler Ishozi, mimi Bumai, Padre Verbeek, Van Helden na Verdaasdonk.walibaki Kashozi.

Mkesha wa Krismas, baada ya chakula cha mchana tukiwa katika chumba cha maburudisho (recreation), Mzee Evarista Kashaga, baba wa marehemu Padre Felix, alifika na telegram 2 kutoka Bunena, Bukoba mjini. Moja ya Padre Laurean Rugambwa, na ya pili ya Padre Verdaasdonk. Zote mbili alizikabithiwa kwa Padre Verdaasdonk. (Padre Laurean hakuwepo pale chumbani, bila shaka aliishajua habari hizo).

Ya kwanza iliarifu kwamba Mheshimiwa sana Padre A. Lanctot ni Vicarius Apostolicus wa Vikariati ya Bukoba na ya pili kwamba Mheshimiwa sana Padre L. Rugambwa ni Vicarius Apostolicus wa Kagera ya chini (Lower Kagera). Mimi niliruka kama kichaa na kutoka nje kwenda kwa Padre Laurean nikaanguka kifuani mwake kumpongeza, (Kumugwa omu bikyai kumwihukya Ati; 'Nikwo bili'). Nilitoka nje kuwaambia vijana wagonge kengele. Piga kengele nikasema, watu wakadhani kuna jambo kubwa kengere kulia wakati huo wa saa 8. Watu walitimka kwa wingi na kumpogeza sana. Baada ya hapo kama ilivyopangwa aliondoka kwenda Katoma kupitia Kyamato. Wiki iliyofuata krismas watu kutoka 'Kagera ya chini' walianza kumiminika; hasa kutoka Parokia za Rutabo na Mugana. Wiki iliyofuata Baba Paroko wa Rutabo, Primus Kabyemera, alifika na usafiri wa kuaminika kumpeleka rasmi Rutabo.

Nimetanguliza haya kifupi nipate kuwapatia picha halisi ya tukio hilo; kwani mimi nilikuwepo kama testis ocularis (niliyashuhudia kwa macho yangu). Yafuatayo ni tangu kupewa uaskofu.

Kagera ya chini– Rutabo Diocese – Kuunganisha Bukoba na Rutabo-Kardinali na Tabia yake

Uaskofu wake ilikuwa tarehe 10/2/1952 Rutabo penyewe. Umati mkubwa wa watu ulihudhuria. Lilikuwa tukio la peke yake. Aliyetoa uaskofu alikuwa Askofu Mkuu David Mathew, mjumbe wa Baba Mtakatifu makao yake yakiwa Nairobi, Kenya, akisaidiawa na Mhashamu askofu. Blomjous W. F. Askofu wa Mwanza, wa pili alikuwa askofu Joseph Kiwanuka wa Masaka Uganda.

Jimbo au (Vikariati) ya Kagera ya chini lilipoanza makamu wa askofu alikuwa Mheshimiwa Padre Modestus Rwiza, mweka hazina alikuwa Padre Dominic Tinkagira, Mkuu wa Mashule (Katibu wa Elimu) alikuwa Padre Telesphore Kachubo na Paroko wa Parokia ya Rutabo alikuwa Padre Primus Kabyemera.

Mimi nilikaa Kashozi mwaka mzima wa 1952. Askofu A. Lanctot W. F. alikataa kuniruhusu niende Rutabo (au Vikariati ya Kagera ya chini) kwa kisingizio kwamba hapakuwepo Padre wa kushika shule za Kashozi. Mwaka uliofuata 1953 niliruhusiwa rasmi kwenda Jimboni kwangu. Basi nilienda na kufika tu nilikabishiwa shule za Parokia ya Rutabo kama paroko msaidizi. Tulikuwa watatu:- Mheshimiwa sana. Msgr. M. Rwiza Makamu wa askofu na Paroko, Padre Aloys Mwesigwa na mimi. Parokia ya Rutabo lilikuwa eneo kubwa sana, sasa ndizo parokia ya Rutabo, Ichwandimi, Igoma, na nusu ya Mwemage (i.e Rutete na Migongo).

Nilifanya kazi parokiani hadi mwaka 1954 ndipo nikapelekwa Dar es Salaam kwa Padre Walsh W.F. na Padre Gustav OFM Cap, katika ofisi ya T.E.C. ya wakati huo ili nifundishwe mbinu za kuwa Katibu wa Elimu na Mkaguzi wa Mashule. Kusema kweli kwa lugha ya kisasa, ilikuwa namna ya tuition (mafunzo). Nilikaa huko miezi mitatu. Niliporudi Rutabo nilipewa kazi ya kuwa Katibu wa Elimu wa vikariati.

Mwaka wa 1953 Kagera ya chini ikawa Jimbo la Rutabo

Kazi ziliendelea kwa shida kubwa lakini bila kukata tamaa. Zilikuwa hasa kazi za kujenga Parokia, mashule, hospitali na zahanati na vigango vikubwa ambavyo baadaye vitageuzwa kuwa parokia.

Wazungu wote, mapadre kwa masista walikuwa wamehamia jimbo la Bukoba. Wakati huo ilibidi kujenga mashule ya kati (Middle Schools). Zilipotengwa vikariati hizi mbili Bukoba na Kagera ya Chini. Sehemu ya Kagera ya Chini ilikuwa na shule ya kati moja tu, Mugana Middle school ambayo ilikuwa bado kumalizika. Tulikamilisha hiyo na kuongeza nyingine tatu, ile ya Rutabo, Ibwera (Mwemage) na Bugandika; na baada ya masista wa Canossa kufika Mugana 1956, ilianzishwa ya shule ya kati ya wasichana hapo Mugara.


Tukitathimini vizuri vikariati ya . Kagera ya chini walivyokuwa wameitengeneza ilikuwa na Parokia tano tu: (1) Rutabo, (2) Kishogo, (3) Kasambya, (4) Mugana na (5) Kanyigo; pamoja na vigango vikubwa vitatu (1) Mwemage (Ibwera); (2) Buyango (Kabashana); na (3) Ishozi. Hivyo Roma walitaarifiwa kuwa kuna Parokia nane.


Basi hii ndiyo hali halisi ilivyokuwa ambayo Mzee wetu Kardinali Rugambwa aliipokea kama Vikariati ya Kagera ya chini. Hapakuwepo hospitali hata moja, isipokuwa vizahanati viwili vidogo; kile cha Mugana ambapo masista weupe (White Sisters) waliondoka, na kile cha Kishogo. Navyo vilikuwa vikiendeshwa kiparokia.

Mzee wetu Kardinali Rugambwa tabia yake inajitokeza ukimfuatilia kupitia hali alizozikabili na kuzipitia kiushujaa na bila manug'uniko yoyote, toka mwanzoni hadi mwisho wa maisha yake. 'Alikuwa mtu wa mipango' Yaani hakufanya mambo kiholela, wala kienyeji. Tutoe mifano:-


  1. Kujenga Parokia mpya, shule, makanisa, hospitali, na zahanati; kupeleka watu kusoma waseminari, mapadre na walei; yote yalienda kimpango. Yalifanywa vizuri na kukamilishwa vizuri mpaka mwisho. Kutoa mfano mwingine mdogo lakini wa kushangaza. Kwa wakati ule aliunda chama cha walei wasomi, ambacho kwa sasa tungekiita C.P.T. Alikiita chama cha Mt. Augustine. Hawa wasomi walisaidia wakati wa siasa ulipoanza kujitokeza. Baadhi yao walipelekwa ng'ambo kusoma, na waliporudi walisaidia jimbo wakati wa kuunda halmashauri za walei. Baadhi yao walichaguliwa na Serikali yetu baada ya uhuru, kuwa mabalozi wa Tanzania katika nchi za Ng'ambo.

    Mifano mingine ni Hospitali ya Mugana, zahanati ya Mwemage, Seminari na Vyuo
    Seminari kuu ya Ntungamo, shule ya sekondari ya wasichana ya Rugambwa; kukarabati na kupanua sekondari ya wavulana ya Ihungo, na shule ya seremala Kashozi. Kujenga makanisa mapya na kukarabati makanisa mengi jimboni. Kujenga seminari ya Rutabo na kuboresha seminari ya Rubya; kujenga Katedrale nk yote alikuwa anatafuta pesa yeye. Na hakukubali kubadili mipango yake kiholela bila kutaarifiwa.

    Aliwezaje kufanya hayo yote kwa muda mfupi hivi, tena kwa wakati mmoja. Pesa alizipataje. Wafadhili aliongea nao kwa vipi? Hayo ni yeye aliyajua, lakini alifaulu. Alikuwa mfuatiliaji mzuri sana. Daima alifanya mikutano na wahusika, hasa wahasibu wa jimbo. Mimi najua hayo kwa sababu nilikuwa Katibu wa elimu na askofu msaidizi wake. Daima alionyesha kuthamini mpango ulipofanikiwa vizuri. Na alitoa pongezi kweli kwa kazi nzuri.


  2. Kuona mbali
    Alijua atangulize kitu gani na kifuate kitu kipi. Kwa mfano tulipopata vikariati ya Kagera, tulikuwa mapadre 18 na yeye wa 19 na hatukuwa na Seminari. Rubya ilikuwa Seminary ya jimbo la Bukoba. Tuliruhusiwa kupeleka 1/3 ya wanafunzi na Bukoba iliingiza 2/3 kadiri ya ukubwa wa eneo letu. Eti Kagera ya chini ilikuwa 1/3 ya jimbo la Bukoba. Lakini kimaendeleo na waumini tulikuwa nyuma sana. Mtu mwenye huruma angepaswa kutufikiria kwa namna ya pekee, kusudi tuweze kuinuka. Lakini kinyume chake ndicho kilichofanyika. Kila mpago ulikuwa wa kutugandamiza. Askofu wetu asingekuwa mtu wa moyo mkuu, angekata tamaa. Alifanya nini? Aliamua apeleke baadhi ya waseminari wengine wasome Roma. Kwa sababu kozi ile ile tuliyofanya Katigondo kwa miaka 10 Roma ilifanyika katika miaka 6 tu. Hivyo kwa miaka michache tutapata mapadre wengi; nao watakuwa na ufuzu (qualifications) nzuri zaidi, kuliko wanaotoka Katigondo.

    Alilaumiwa sana na maaskofu wenzake; lakini yeye akakaza nia tu. Baba Askofu Kilaini unaelewa fika matokeo ya mpango huu, kwa sababu na wewe ni matokeo yake. Mimi nilirithishwa na mpango huo, na mimi nilimshirikisha askofu Timanywa, kusudi aendelee kupeleka watu ng'ambo kusoma. Nadhani mpango huo unaendelea. Ni budi tujifunze mapokeo hayo kutoka kwake. Ingawa sasa hawapendelei kupeleka sana waseminari; lakini mfumo unapaswa kukaa palepale. Tupeleke mapadre na tusirudi nyuma.


  3. Alikuwa mvumilivu
    Katika pirika pirika hizi za kujenga jimbo lake, alipambana na matatizo makubwa na mengi sana. Kwa mfano:- Matatizo ya watenda kazi, matatizo ya mapadre, matatizo ya watawa, matatizo ya wakristu, matatizo ya dini tofauti au madhehebu mengine ya kikristu, matatizo na wamisionari waliotukabithi jimbo, matatizo ya pesa, matatizo mapadre walioasi au kumshtaki Roma, nk. Hayo yote aliyavumilia kama mwanamume na kwa utulivu.


  4. Alikuwa Kasisi Mkuu wa mapendo na moyo mkuu kwa kondoo wake
    Alipenda sana mapadre wake na wakristu wake, kwa neno moja alikuwa mchungaji mwema; kila aliyekuja kumuona kwa mashauri, au kumtembelea alimpatia muda wa kutosha wa kuonana na kuongea naye; na kila mmoja alitoka ameridhika. Hivyo mahusiano yake kwa watu jimboni na nje walimpenda na kumheshimu. Wafadhili waliridhika sana kwa mawawasiliano naye. Alialikwa mara nyingi kwenda kwenye sherehe mbalimbali. Alijua kuchagua vizuri wafanyakazi wake na alikuwa na uhusiano nao wakati wote. (He was always available – He had a golden and generaous heart.) ie. Kila mara alipatikana na alikuwa na moyo wa dhahabu. Ila watu walimwogopa kwa sababu ya unyamavu wake. Hakuwa mtu wa kusema hovyo au kiholera, mara nyingi majibu yake hayakuwa ya mchezo.


  5. Alikuwa mtu wa kufuata ratiba: i.e 'omnia tempus habent'
    Ratiba ya kazi ofisini, ratiba ya sala, ratiba ya saa ya kula, ratiba ya mapunziko, ratiba ya kulala na ratiba ya kuamka. Hakukesha usiku wala kuchelewa kuamka asubuhi.


  6. Alikuwa nadhifu sana
    Nyumbani mwake chumbani , mezani pake (ofisini) na kwenye maktaba yake kulikuwa na mpangilio mzuri. Aliweza kujua kila kitu kiko wapi alipoingia vyumbani mwake. Alipokuta vitu vimekaa ovyo chumbani au karatasi hazikupangwa vizuri mezani, daima alitoa angalisho 'unawezaje kuelewa vitu vyako viko wapi, katika vurumai hii?'


  7. Alikuwa mtu wa kujinyima na kujikatalia sana hasa kifedha na kimatumizi
    Aliingiza pesa nyingi majimboni alimofanya kazi; Rutabo, Bukoba, na Dar es Salaam; lakini matumizi yake ya binafsi yalikuwa ya kawaida na madogo. Hakutumia fedha ya ajabu ajabu kwake yeye mwenyewe, wala kwa familia yake. Nyumba aliyojenga nyumbani kwake ilikuwa ya kawaida tu, banda. Lakini nyumba ya Askofu kwa sababu ni ya umma, ilikuwa nzuri, vg. Rutabo, Ntungamo, Dar es Salaam. Kila mahali kadiri ya hadhi yake. Hivyo hawezi kulaumiwa kuwa ameharibu ama kusambaratisha pesa ya jimbo. Uwajibikaji (Accountability) ulikuwa mfano wake.


  8. Alifundisha majimbo hali ya kujitegemea
    Kwa kuingiza mfumo huu alipata upinzani mkubwa sana popote katika majimbo yake alipoongoza i.e Rutabo, Bukoba na Dar es Salaam. Lakini hakukata tamaa.


  9. Alikuwa mtu wa taswira (Vision)
    Je hii siyo sawa na kuona mbali kama katika No 2? Kadiri ya maono wangu ni tofauti kidogo. Mtu mwenye vision ni yule hasa anayekuwa genius au mwenye master-mind, talented; mwenye uwezo to discern (yakinifu) mambo na kuyaendeleza hadi mwisho bila ya kuchanganyikiwa, ingawa katika safari yake ya kimaisha yatajitokeza matatizo makubwa. Katika jambo hili, Mzee wetu amejionyesha hivi, Kwa mfano, pale Rutabo alipoteuliwa kama Kardinali na baadaye aliposhika Bukoba nzima, Mzee wetu alitunza kichwa. Hakubadilika badilika. Alikaa yule yule. Alianzisha Seminari ya Ntungamo ikiwa ya kijimbo. Alianzisha Secondari ya wasichana ya Rugambwa. Alikarabati shule ya Secondari ya Ihungo na kuipatia kidato cha tano na sita, na kufuta T.T.C ya Ihungo ya walimu wa Grade I na kuiruhusu ihamie Morogoro T.T.C. kama ya Kitaifa (T.E.C.). Kwa kufanya hivyo tulipata vijana wengi wa kuingia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

    Alipokuwa bado Rutabo alianzisha Seminari ndogo, akaiita Preparatory Seminary. Lengo lake lilikuwa kuanzisha Seminari ndogo ya jimbo la Rutabo. Roma ilipochanganya majimbo yote mawili, ilibaki Prep-Seminary na vijana wakahamishiwa Rubya. Alipofika Dar es Salaam alianzisha Seminari Kuu ya Segerea. Watu wengine walikuwa wakipinga. Ila yeye hakujali. Wakataka kuvuruga nia na mipango yake na kushauri ijengwe karibu na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

    Alikazana na mpango wake, akatafuta kiwanja Segerea,. Seminari ilijengwa na sasa ipo na inafanya kazi. Hapo Jimbo Kuu la Dar es Salaam, kila mmoja alifikiri kwamba ataanzisha mara moja seminari ndogo ya Jimbo, lakini Seminari ya Visiga ilikuwa karibu kitu cha mwisho alichofanya katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Ila kwanza alikaribisha mashirika mbali mbali ya watawa, wanaume kwa wanawake, na kupata viwanja vya kujenga maparokia na hospitali. Akafanya mpango mashirika hayo yakutane na kujadiliana pamoja na kuelewana kwa kuunda umoja wa watawa. Lengo lake kadiri alivyonielewesha, hakuna shirika lolote linaloweza kusema lenyewe ni la maana zaidi kuliko shirika lingine. Mashirika yote yanafanya kazi ile ile kwa pamoja wakitumikia taifa la Mungu.


  10. Nadhani hadi hapa nimekupatia picha ya Mzee wetu. Hivyo ninaomba nikomee hapa. Ni matumaini yangu ya kwamba wewe na wengine mtachangia mawazo mengine ili kukamilisha kitu kizima.

    Ninabaki wako katika Kristu

    +P.G. Mkalanga O.S.B


Contact Information
Bishop's House Ntungamo,
P.O.Box Private Bag,
Bukoba, Tanzania.
Tel. & Fax. 028 - 2220746
Office: Tel. 028 - 2220194
E-mail: b.officebk@yahoo.com
Website: www.bukobadiocese.co.tz
© Bukoba Catholic Diocese 2023
Find us on
Facebook: Bukoba Catholic Diocese
Twitter:  @bcdcatholic