Hayati Laurean Kardinal Rugambwa — Mtu Maarufu Katika Kanisa Pamoja na mambo mengine mengi, umaarufu wa Hayati Laurean Kardinal Rugambwa ulitokana na ukweli kwamba yeye alikuwa Kardinali wa kwanza mzaliwa wa bara la Afrika. Huo ni umaarufu wa paji la hadhi anayopewa mtu na ambao si lazima utokane na mastahili ya mtu binafsi kama vile kwa kufaulu mtihani au kwa kupambana vitani.
Umaarufu wa aina hiyo unahitaji daima kudhihirishwa uhalali wake kwa namna mbili: a) kwa maisha na mapato ya kazi za mtu mhusika katika utekelezaji wa hadhi aliyopewa. b) umaarufu anaopewa na watu wengine kulingana na hiyo hadhi aliyokabidhiwa na Kanisa. Kuhusu maisha na mapato ya kazi za Mwadhama Baba Kardinal Laurean Rugambwa, haihitajiki uchunguzi wa pekee sana mintarafu ya kazi zake nyingi kama Kardinali. Inatosha kutambua ukweli kwamba, kama Kardinali wa kwanza mzaliwa wa Bara la Afrika, Mwadhama Kardinali Rugambwa alikuwa kama kielelezo cha uwezekano wa mzaliwa wa Afrika kustahili hadhi kama hiyo ndani ya kanisa. Kwamba baada yake wametokea Makardinali wengi wazaliwa wa Afrika ni ishara wazi kwamba kwa maisha na matokeo ya kazi zake, Laurean Kardinali Rugambwa alifaulu binafsi kudhihirisha umaarufu wake kama Kardinali wa kufaa katika Kanisa Katoliki. Asingeishi na kutenda kama alivyotakiwa, Kanisa Katoliki lingesitasana kuteua Makardinali wengine wazawa wa Afrika.
Kuhusu sifa na umaarufu aliopewa na anaoendelea kupewa na watu wengine, yawezekana kuugawanya katika sehemu mbili. Wapo wanaomwenzi Hayati Laurean Kardinali Rugambwa kwa moyo mnyofu kabisa. Kwa bahati nzuri hao, nionavyo mimi, ni wengi zaidi kiidadi kutokana na ukweli kwamba katika maisha ya Mwadhama Kardinali Laurean Rugambwa yapo mambo mazuri mengi ambayo yanastahili kuenziwa. Polycarp Card. Pengo, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam