Header

MAISHA YA KARDINALI RUGAMBWA RUTOBO NA BUKOBARugambwa - Mwana Harakati wa Elimu kwa Mapadre

'Alijionyesha Mkereketwa wa Elimu'
Askofu Damian Kyaruzi – Jimbo la Sumbawanga

Padre Laurean Rugambwa aliwekwa wakfu kuwa Askofu tarehe 10 Februari,1952, akiwa ni Mtanzania wa kwanza kukabidhiwa wadhifa huo. Hii ilikuwa ni miezi michache baada ya kurejea nchini kutoka Roma, Italia, ambako alikuwa anasomea Sheria za Kanisa katika Chuo Kikuu cha Urbaniana. Alirudi na digrii ya Udaktari katika fani hiyo.Tangu mwanzo mwa uchungaji wake alijionyesha kuwa Askofu mwenye busara na hekima.


Bp Kyaruzi

Hakuwa Askofu wa maneno mengi bali matendo yake yaliongea kwa sauti kubwa zaidi kuliko maneno. Hivyo mipango yake kama ya elimu haikutangazwa kwenye mimbari au majukwaani. Hakutaka awe ni yeye peke yake mwenye kisomo cha juu katika elimu ya Kanisa bali alitaka na baadhi ya mapadre wake wapewe fursa kama yeye aliyopewa. Katika hili alijionyesha kuwa mkereketwa wa elimu kwa mapadre.

Jimbo Katoliki, Rutabo, alilokabidhiwa kuliongoza lilikuwa na parokia tano tu, ambazo ni Rutabo, Kishogo, Mugana, Kanyigo na Kashambya. Kama parokia zilivyokuwa chache vivyo hivyo na mapadre aliokuwa nao walikuwa wachache.Katika eneo lote la Jimbo hilo hakukuwepo shule yoyote iliyokuwa juu ya darasa Ia sita ( au District School). Alijionyesha mkereketwa wa elimu kwa kuhimiza ujenzi wa shule za msingi parokiani na vigangoni kwa njia ya kujite­gemea. Licha ya hizo alijenga shule za kati (Middle Schools) za Rutabo, Mwemage na Mugana. Alijenga pia shule za ufundi pale Rutabo na Mugana.

Tangu mwanzo alikabiriwa na uchache wa mapadre na hata wanafunzi wa upadre. Kwa sababu hiyo alianza kukabiriana na tatizo hilo kwa kujenga Seminari Ndogo (Preparatory Seminary) hapo Rutabo. Seminari hii ilifunguliwa mwaka 1958 chini ya uongozi (Gombera) wa Padre Joseph Benedicto Labre Rugemalira.Padre, tunda la kwanza la seminari hiyo alipadrishwa mwaka 1970. Lengo zima la kuanzisha seminari lilikuwa kupata mapadre wa kutosha na akiwa na idadi nzuri ya mapadre na mafrateri angeweza kuwa na unafuu wa kuchagua baadhi yao kwenda kuchukua masomo ya juu katika fani mbalimbali. Hata hivyo ili kutimiza azma yake ya kuwawezesha mapadre kusoma katika vyuo vikuu hakusubiri idadi iongezeke, kwani mwaka 1956, miaka mitatu baada ya uaskofu wake alimtuma Frater Longino Rujwahura Roma ili aendeleze masomo yake katika Chuo Kikuu cha Urbaniana. Huyu alifuatiwa na Padre Justinian Laurent Bamanyisa aliyetumwa Amerika kwa masomo ya uhazili.

Mwaka 1960 alipoteuliwa na Baba Mtakatifu Yohane XXIII kuwa Kardinali, ulikuwa ni mwanzo wa kuonyesha azma yake ya kuelimisha mapadre. Mwaka huo huo alipeleka mafrateri wawili Uingereza na wawili Roma. Kuanzia hapo kila miaka miwili alikuwa anapeleka mafrateri wawili Roma mpaka alipohamia Jimbo Kuu Ia Dar~es-Salaam, mwaka 1969. Si mafrateri tu bali na mapadre nao walipelekwa katika vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi. Mmoja wa mapadre hao alikuwa Msgr.Robert Rweyemamu ambaye alikuwamtanzania wa kwanza kuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu, Tanzania.


Rutabo

Kama nilivyotangulia kueleza hapo juu, tangu mwanzoni mwa uaskofu wake alinuia kuwa na seminari zake, ndogo na kubwa ili aweze kuwa na uhakika wa kupata mapadre wa kutosha. Nia hii inathibitishwa na ujenzi wa Seminari kubwa ya Ntungamo iliyofunguliwa mwaka 1964. Seminari hizi zilihitaji walimu wenye sifa katika taaluma mbalimbali. Kwa kuwapeleka mafrateri na mapadrekwa masomo katika vyuo mbalimbali alikuwa na lengo la kuandaawalimu wa kufundisha katika seminari zake ndogo na kubwa. Lengo lake halikuishia kwenye seminari tu, bali pia alilenga kupata walimu wa kufundisha katika taasisi za kanisa za masomo ya juu na pia kupata mapadre wataalam wa kufanya kazi ya utume katika sekta mbali mbali zinazohitaji utaalam wa aina fulani kama vile wa kisheria au nyadhifa za juu katika Kanisa.

Mpaka alipohamia Dar-es-Salaam kutoka Bukoba alikuwa amekwisha anza kuvuna matunda ya kazi yake, kwa mfano mmoja wa mafrateri aliowatuma Roma, 1960, alikuwa tayari padre mwanajimbo wa kwanza kufundisha katika Seminari yake ya Ntungamo, naye ni Padre Dominic Rugemalira. Na katika seminarindogo ya Rubya, mmoja wa mapadre waalimu, Padre IgnasNdibalema alikuwa na digrii ya kwanza ya ualimu kutoka Chuo Kikuucha Makerere, Uganda, na mwingine Padre Sadoth Rweymamu alikuwa na Diploma ya ualimu kutoka Dublin,Ireland. Na Katibu Mtendaji wa Elimu wa Jimbo Padre Longino Rujwahura alikuwa na Diploma ya ualimu kutoka Ireland akiwa pia na Digrii ya Pili (Masters)katika Theologia kutoka Chuo Kikuu cha Urbaniana, Roma.

Na orodha ya Walei aliowashughulikia kupata elimu ya juu nao ni ndefu. Kwa sababu ya ufinyu wa rasilimali watu (mapadre) na rasilmali fedha, hakuweza kufanya mengi kwa mara moja, lakini dira yake ilikuwa wazi. Pole pole kadiri alivyokuwa anawezeshwa alikuwa anatekeleza. Na kweli yeye aliweka msingi ambao bado unaendelea kutegemeza kuta za elimu ya mapadre katika Jimbo lake la zamani,Rutabo/Bukoba. Alikuwa kweli mwanaharakati wa elimu kwamapadre.

+Damian Kyaruzi Askofu wa Sumbawanga


Kardinali Rugambwa - Mpenda watu na Mnyenyekevu

Padre Justinian Bamanyisa

(Padri Justinian Bamanyisa alikuwa katibu wake wa karibu sana tokea mwaka 1955, aliishi naye nyumbani na alisafiri naye kila mahali, Ulaya, Marekani na Afrika hadi alipohamia Dar es Salaam mwaka 1969. Alimwamini sana na kumpenda).


Family

Mwadhama Kardinal Rugambwa alikuwa mtu aliyezaliwa katika familia ya kitemi Parokiani Rutabo - BUKOBA, Kagera; wazazi wake Ta Domitian Rushubirwa na Ma Asteria Mukaboshezi, walimlea vizuri na tabia zake zilijionyesba hasa katika upendo na unyenyekevu, akiwashughulikia wenzake vilivyo.

Hivyo msemo wa Mtakatifu Augustino, 'UBI AMATUR NON LABORA­RATUR, SI LABORATUR, LABOR .AMATUR', ndio kusema:" PENYE UPENDO HAKUNA UCHOVU, na kama uchovu upo, UCHOVU HUPENDWA."
Upendo Wake
Umedhihirishwa na kuoneshwa akiwa mwanafunzi huko Rutabo shuleni, Rubya seminari ndogo, na hasahasa akiwa frateri huko Katigondo (Uganda). Alikuwa kiongozi shupavu na mpenda watu.. Mafrateri walimfikia wakati wa shida na furaha, akiwa tayari kutoa huduma zilizohitajika. Baganda, Banyankole, Bakiga, Batoro na Banyoro pale Seminarini hawakusita kumfikia, na hivyo aliweza kujifunza na kuelewa lugha zao na yeye kuwafundisha Kiswahili na Kihaya, ndio kumegeana kwa upendo karama. Walimu na viongozi Seminarini waliridhika na tabia zake, hasa Fr. Joseph Kiwanuka, W.F., alimsifu.

Akiwa Padre, Parokiani Kagondo, Rubya na Kashozi, daima alikuwa tayari kutoa huduma na msaada wa- kiroho na kimwili kwa watoto, vijana na wazee, aliwachangamkia na kuwapokea vizuri kwa upendo wa kibaba.

Huko Roma, katika Chuo cha Urbanianum (Propaganda College), akiwa mmojawapo wa mapadre wanafunzi toka nchi za Afrika Mashariki, Afrika ya Kati na pengine Ulaya, Asia na Amerika, aliwaunganisha Waafrika katika umoja ili kusaidiana katika Vyuo mbalimbali mjini Roma. Na miongoni mwa wanafunzi hao mapdre toka Tanzania, Uganda, Kenya, Zambia, Malawi, Rwanda na Burundi, walijisikia nyumbani pamoja na Fr. Laurean Rugambwa, katika upendo bila ubaguzi wowote.


Bamanyisa

Akiwa Askofu wa Jimbo la Kagera ya Chini (Lower Kagera), lililokabidhiwa kwa mapadre wazawa kama vikariati, aliendelea kudhihirisha karama zake na upendo wake katika uongozi wa Vikariati. Wakati huo huo akiwa mvumilivu na mpole kama mapadre wenzake hapo Rutabo walivyosimulia.

Alijumuika na mapadre katika ujenzi wa shule; na shule ya Rutenge, ilipangiwa jina la 'Bishop's School' kwa sababu katika kupangiana kazi hiyo aliisimamia mwenyewe. Alihimiza ujenzi we Shule za Kati, shule za Ufundi kama Seremala, Ushonaji viatu na nguo, na maarifa ya nyumbani, seminari ya Rutabo na zahanati ya Mugana (Kashanga Dispensary).

Aliwakaribisha Masista Wakanossa na Mafranciscan wa Heythuysen kusaidia kueneza ufalme wa Mungu kiroho na kimwili huko Mugana na Mwemage.

Katika nyanja za EIimu, alijishughulisha sana katika kutafuta ufadhili wa masomo (Scholarship), si kwa Mapadre, Mafrateri na Masista tu, bali hata kwa Walei, Jimboni Rutabo, Bukoba na hata Tanzania na Afrika Mashariki. Na miongoni mwa waliofaidi ufadhili huo wamewahi.kushika nyadhifa mbali mbali za uongozi Kitaifa na Kimataifa, wakiwemo hata mabalozi na wafanyakazi katika Umoja wa Mataifa.

Kama Askofu wa Jimbo la Bukoba na Kardinali, Mwadhama L. Rugambwa, aliendelea na juhudi zile zile za upendo wake kwa watu wote bila ubaguzi. Elimu, Afya, Ustawi wa jamii, vilitiliwa mkazo zaidi kwa vile, yeye, kama Kiongozi wa ngazi ya juu Kanisani na taifani, aliweza kupata na kutoa misaada. Alijenga Seminary ya Ntungamo, Rugambwa Secondary School, Hospitali ya Mugana na kuimarisha hospitali za, Rubya na Kagondo na Zahanati za Kashozi na Mwemage. Kanisa Kuu zuri la Bukoba Mjini ilijengwa na Makanisa mengine na Mashule yalijengwa au kupanuliwa.

Upendo wake na uvumilivu pamoja na unyenyekevu wake kama Askofu wa Kagera ya Chini (Lower Kagera) kwa kusafiri kwa pikipiki na hata nyuma ya lori vilizaa matunda akiwa Askofu na Kardinali.


Mapadre

Monsinyori wa Bukoba, Mwadhama Kardinal Laurian Rugambwa alijaliwa kuwa KIFUNGUA MIMBA: Ni mtoto wa kwanza wa wazazi wake, Ta Domitian na Ma Asteria; ni Padre wa kwanza Parokiani Rutabo; ni Padre mwanajimbo wa kwanza kufuata masomo Roma; ni Askofu mwananchi Mtanzania wa kwanza, ni Askofu Mkuu Mwafrika wa kwanza wa Dar es Salaam, Kardinali wa kwanza Mwafrika kupata cheo hicho; na mwisho ni wa kwanza kama Kardinali Mwafrika kukaa katika Baraza la Makardinali kuchagua Papa (Conclave). Pia alikuwa Kardinal wa kwanza Mwafrika kuwakilisha Baba Mtakatifu (kama Mjumbe) katika sherehe za miaka 100 ya Ukristu Madagaska 1961.

Ingawa aliwahi kukutana na watu mashuhuri wengi, wakiwemo Mababa Watakatifu (wengine aliwachagua, kama Paulo V, John Paulo I na John Paulo II), Makardinali, Marais na viongozi wengine wa nchi Afrika, Ulaya, Amerka na Asia na Australia, akapewa na Shahada na nishani kadhaa, Kardinali Rugambwa hakujiona kama mtu mkubwa. Alikaa mtu wa watu wote bila ubaguzi.

Wakati wa safari zake za Roma na Ulaya, daima alikumbuka kuchukuwa zawadi kwa rafiki zake; Kahawa ya TANICA, hata pilipili kwa wale waliokuwa wanatuimia, pia na UGOLO kwa Rector na Mapadre kutoka China na Nigeria waliokuwa wanafurahia SNUFF made in BK Tanzania! NSENENE na KAMWANI (kahawa ya kutafuna) vilikuwa miongoni mwa zawadi. Na kila mmoja alikuwa anauliza, 'Je, Baba, TANICA, KA-UGOLO na PILIPILI? Nsenene?' Na jina alipata la 'Nostra Eminenza' Yaani Kardinali wetu. Mpaka kustaafu kwake Bukoba na Dar es Salaam, Kardinali aliacha kumbukumbu kubwa sana za UPENDO NA UNYENYEKEVU wake mkuu kwa Majimbo hayo na Taifa letu hata Kanisa dunia kwa ujumla.

Hivyo ndivyo Baba Mwadhama Kardinali Laurian Rugambwa alivyotimiza lile neno la Mt. Augustini: 'UBI AMATUR NON LABORATUR, SI LABORATUR, LABOR AMATUR.' Na kwa kumwenzi, tufuate alivyofanya: AMEWEZA na SISI TUNAWEZA kutenda vema kwa watu wote.

Fr. L. J. BamanyisaWasifu wa Hayati Kardinali Rugambwa

'Aliwapenda sana Watoto Wadogo nao Walimpenda sana'
Askofu Desiderius Rwoma - Askofu wa jimbo la Singida

Upendo kwa Watoto Wadogo

Hayati Mwadhama Kardinali Rugambwa aliwapenda sana watoto wadogo. Watoto walimpenda pia. Alikuwa na mvuto wa pekee kwa watoto. Binafsi upendo wake niliuonja nikingali mtoto mdogo, kwa kumbukumbu zangu mwaka 1955.


Mtoto

Shule yangu ya awali (Chekechea) ilikuwa karibu na nyumba yake ya Kiaskofu Parokiani Rutabo. Mara nyingi tulipokutana naye mathalani asubuhi baada ya Misa Takatifu alizoea kuwauliza wachache waliokwenda kumsalimia majina yao na ya wazazi wao na kwa kuoanisha sura wengi wetu alitufahamu hata kwa majina na kuulizia habari za wazazi wetu. Wakati wa sikukuu kama vile Pasaka na Noeli alipendelea kutupatia zawadi ya picha mbalimbali za watakatifu na mara chache Rozari na kudadisi kama tulijua kusali Rozari au la.

Kila alipokuwepo nyumbani Askofu Rugambwa alipendelea mara nyingi kusimama mbele ya baraza akiangalia kwa makini jinsi tulivyokuwa tukicheza. Mara chache ilipotokea yakawepo mabishano makali au magomvi baina yetu tulizoea kumwendea atuamue. Mara zote alitupatanisha bila adhabu nasi - nadhani kwa kuwa tulimwona kuwa "mpole, mheshimiwa na mtu wa haki" - tulipokea maelekezo yake kwa furaha.

Kwa utani alizoea kumuuliza kila mmoja wetu kama anataka kuwa Padre au hapana. Wengi tulijibu tunataka kuwa Padre. Aghalabu aliendelea kuuliza,"Unataka kuwa kama Padre gani au Sista gani?" Wengi tulisema,"Kuwa Padre kama wewe" na wasichana "Kuwa Sista kama Mameya yaani Sista mkubwa wa nyumba au Sista mwalimu wetu. Naye alizoea kumalizia akisema "Chunga sana msinidanganye".

Mimi binafsi naweza kusema niliguswa sana na Mwadhama na kupata hamu ya kuwa Padre kutoka kwake. Siku moja tukicheza mbele ya nyumba yake mpira mdogo uliingia ndani ya nyumba yake. Tuliogopa sana kumwendea aturuhusu tuingie kuuchukua. Baadhi yetu tulianza kusogea polepole tukiambaa ukuta uliokuwa karibu na chumba ulipoingia mpira wetu. Mwadhama alitambua haraka nia yetu na hofu yetu. Baada ya muda mfupi aliashiria twende tukauchukue. Nilijitosa kumwendea. Bila kusema neno alinyoosha kidole akinielekeza niufuate chumbani mwamke uvunguni mwa kitanda chake cha kulala. Nilikwenda nikitetemeka. Baada ya kuupata nilimwendea na kumshukuru. Ndipo aliposema kwangu kwa sauti ndogo, "Mwanangu, umeshupaa hadi kuingia chumba changu cha kulala, lazima uwe Padre". Sikumbuki kama niliitika ndiyo au hapana. Ila Neno lake hilo lilibaki rohoni mwangu. Nilijisikia furaha kualikwa kuwa kama yeye ambaye wengi wetu tulimwona kama mtakatifu, mtu wa cheo kikubwa ajabu na wa kuheshimiwa sana hata zaidi ya Mfalme. Nilifurahi sana nilipojikuta nimekuwa Padre nikiwa bado na kumbukumbu hai ya neno lake la kunihimiza niwe Padre. Mungu mwema na ailaze mahali pema roho yake mbinguni.

+ Desiderius M. Rwoma - Askofu wa jimbo Katoliki la Singida.Contact Information
Bishop's House Ntungamo,
P.O.Box Private Bag,
Bukoba, Tanzania.
Tel. & Fax. 028 - 2220746
Office: Tel. 028 - 2220194
E-mail: b.officebk@yahoo.com
Website: www.bukobadiocese.co.tz
© Bukoba Catholic Diocese 2023
Find us on
Facebook: Bukoba Catholic Diocese
Twitter:  @bcdcatholic