Header

Askofu Nestor Timanywa: Mtu Mnyenyekevu

Rugambwa

MWADHAMA KARDINALI RUGAMBWA

Na Askofu Nestor Timanywa

( Askofu Nestor Timanywa alipewa Upadre na Uaskofu na Mwadhama Rugambwa na pia alikuwa mrithi wa pili wa Uaskofu wa Bukoba baada ya Askofu Nkalanga).

UTANGULIZI

Sasa miaka imepita tangu mpendwa wetu Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa atutoke. Yako mengi ya kukumbuka na kusema juu ya Baba yetu huyu. Hebu niwamegee machache.


1. UPENDO KWA UPADRE NA KWA WANAFUNZI WA UPADRE

Baba Kardinali Rugambwa aliupenda upadre na kutekeleza majumu yake katika maisha akiwa padre wa kawaida, akiwa Askofu na hatimaye akiwa Kardinali. Ni mfano wa kuigwa.

Ili kuhakikisha Wito huo Mtakatifu unaendelea kuwapo katika Kanisa na katika Jirnbo, Kardinali Rugambwa alifanya kila jitihada kuanzisha na kuendesha Seminari. Pia alikuwa daima karibu na mapadre na waseminari, wadogo kwa wakubwa. Ifuatayo ni baadhi ya mifano halisi.


Seminari ya Bunena

Alipopata Uaskofu tarehe 10 Februari 1952, tulikuwa ndio tumeanza malezi yetu katika Seminari ya Bunena. Ilikuwa Seminari ya Msingi (Preparatory Seminary) ya Jimbo likiitwa Vikariati ya Bukoba wakati ule (Bukoba Vicariate). Iliwaandaa watoto kabla ya kujiunga na Seminari Ndogo ya Rubya.

Kila alipopita Bunena akitembelea sehemu mbali mbali za Jimbo lake la 'Kagera ya chini' (Lower Kagera Vicariate), ambalo baadaye liliitwa Jimbo la Rutabo. alifika Seminarini kutusalimu, kutujulia hali na kutupa baraka. Alituhimiza tufuate nyayo zao waliotutangulia katika njia ya upadre.


Seminari ya Rutabo

Kwa kutambua kuwa Seminari ya Bunena haikutosheleza kukidhi mahitaji ya majimbo mawili, alifanya jitihada za makusudi kuanzisha Seminari kwa ajili ya Jimbo lake la Rutabo.

Mwaka 1957 alifungua Seminari ya Rutabo na kuiweka chini ya usimamizi wa Mtakatifu Yohane Bosko mlezi na msimamizi wa vijana. Aliiweka kwenye makao makuu ya Jimbo ili atoe malezi yakinifu kwa mapadre wa kesho wa jimbo lake. Alikuwa daima karibu sana na waseminari na walezi wao, akiwa Baba wa kweli.

Seminari za Rubya na Katigondo

Seminari hizi mbili: Seminari Ndogo ya Rubya na Seminari Kuu ya Katigondo, Masaka, Uganda, zilikuwa nje ya Jimbo lake. Huko ndiko alikotuma waseminari wake kwa malezi zaidi.

Alitoa ushirikiano mkubwa kwa walezi wa Seminari hizo. Pia alikuwa karibu sana na kila mmoja wa waseminari waliosoma katika Seminari hizo. Lakini ukaribu huo haukuwa wa kuwadekeza. La! Hasha! Alituambia ukweli wa msimamo unaompasa padre wa kweli.


Kujengwa kwa Seminari Kuu ya Ntungamo

Kwa kuangalia alama za nyakati, ambazo zilikuwa ni pamoja na nchi yetu kupata uhuru wake na kuongezeka kwa miito, aliamua kuanzisha Seminari Kuu ya Ntungamo Jimboni Bukoba. Pia alijenga makao yake katika ujirani na Seminari hiyo, kwenye mazingira yale yale na yenye utulivu, kwenye uwanda wa juu, nje ya kelele za mji. ili malezi ya mapadre yaboreshwe chini ya uangalizi wake wa karibu.

Baadaye Seminari ya Ntungamo imekuwa sehemu ya taasisi nne zinazoiunda Seminari Kuu moja kwa ajili ya majimbo yaliyo mengi nchini Tanzania. Taasisi hizo ni Seminari Kuu ya Segerea, Dar es Salaam; Seminari Kuu ya Kipalapala, Tabora; Seminari Kuu ya Kibosho, Moshi na Seminari Kuu ya Ntungamo, Bukoba. Amekuwa mshauri mkuu wa Seminari hizi na mjumbe wa Bodi ya Seminari hadi mwisho wa maisha yake ya hapa duniani.


2. KUJITEGEMEA KWA KANISA

Kardinali Rugambwa alifahamu sana maana na umuhimu wa kujitegernea. Hivyo, tangu mwanzo wa uongozi wake kama Askofu alishughulika sana kuliwezesha Kanisa kujitegemea.


Kuhusu Nyenzo

Alianzisha roho ya kujitegemea kwa kila parokia. Alitoa miongozo ya kusaidia kila parokia na taasisi kujisimamia na kujitegemea kiuchumi, wakitumia rasilimali zilizopo. yaani waamini na watu wenye mapenzi mema, pamoja na ardhi za missioni.

Inasimuliwa kuwa zawadi alizozawadiwa katika parokia wakati wa kumpongeza kwa kupata Uaskofu aliziacha kwenye parokia husika ziwe kianzio cha parokia hiyo kujitegemea.

Pia alianzisha na kuchochea uanzishaji wa mipango ya kuendeleza watu; kwa mfano, Credit Unions, ili jumuiya ya watu ijipatie kipato cha kuendeshea maisha na kukuza maendeleo.

Kuhusu Wahudumu (Personnel)

Baba Kardinali Rugambwa alikazana sana kutafuta na kukaribisha jimboni wasaidizi: watawa, mapadre na walei, iii kuimarisha na kuboresha utume katika nyanja zake mbali mbali. Sambamba na hilo, alishughulika sana kupanua na kukuza elimu ya msingi na sekondari kwa jinsia zote. Pia aliwatuma wengi masomoni nchi za nje.


3. UNYENYEKEVU (SIMPLICITY)

Mwadhama Kardinali Rugambwa hakuwa na makuu. Aliweza kufikiwa kwa urahisi na watu wote, wakubwa kwa wadogo — hii ni pamoja na watoto. Alipokea na kutumia ushauri wa watu mbali mbali katika kuongoza Jimbo.

Kwa takriban miaka miwili alitimiza utume wake akisafiri kwa pikipiki. Lakini hakuzembea katika utume wala kufikiri kuwa aina hiyo ya chombo cha usafiri inamshusha hadhi kama Askofu.Alitambua vipaji vya watu na kuvitumia vizuri kutenda mambo makuu kwa manufaa ya Kanisa na jamii. Pia aliviendeleza kwa kuwapatia fursa za masomo ndani na nje ya nchi ill warudipo waweze kuchangia maendeleo yaliyokusudiwa.

Licha ya nyadhifa zake nyingi na nzito, Kardinali Rugambwa alikuwa na nyakati za kushiriki mapumziko (light moments) na wanajumuiya yake huko uaskofuni au katika jumuiya alizozitembelea, hata kama alikwenda huko kikazi. Kwa hali, zote alikuwa mkweli na muwazi. Katika moyo wa mshikamano na maaskofu wenzake wa Tanzania, Baba Kardinali alishiriki na kuambatana nao kikamilifu. Kwa mfano, tulipofika Dar es Salaam kwa mikutano, hata kabla ya kituo cha Maaskofu cha Kurasini kuboreshwa jinsi kilivyo sasa, Kardinali alihamia kwenye Makao Makuu ya Baraza la Maaskofu tangu mwanzo hadi mwisho wa vikao.

Tulipokwenda Roma kwa AD LIMINA VISIT au katika nchi nyingine kwa mikutano ya AMECEA, alipanga pamoja nasi, hata mahali ilipobidi kushirikiana vyumba au huduma nyinginezo. Kamwe hakutumia fursa zilizokuwapo kwa ajili ya Kardinali, kwa mfano kulala mahali pa peke yake au kusafiri kwa gari lake pekee. Alitufundisha na kuimarisha urika wa maaskofu kwa vitendo.


4. SALA NA KAZI

Mwadhama alikuwa mchapa- kazi na mwajibikaji wa hali ya juu. Alitekeleza kazi yake na kusimamia vizuri zile alizowakabidhi wasaidizi wake kwa ngazi zote. Wakati huo huo alikuwa mwaminifu kwa maisha ya sala. Alidhihirisha upendo mkubwa na ibada kwa Mama Maria. Yamkini alichota busara yake ya kichungaji kutoka kwa Bikira Maria Mama wa Shauri Jema (Mater Boni Concilii) aliyekuwa Kauli-Mbiu ya Nembo yake ya Kiaskofu.

5. HATIMA

Ni matumaini yangu kuwa msomaji wa habari hizi atafaidika, siyo tu kwa kumfahamu zaidi Baba Kardinali Laurean Rugambwa, lakini hasa kwa kuiga angalau baadhi ya fadhila na busara zake.

Ama! Kweli hapa methali inadhihirika isemayo: "Kumcha Mwenyezi Mungu ni shule ya hekima; kabla ya kuheshimika ni lazima kuwa mnyenyekevu" (Methali I 5:33).

APUMZIKE KWA AMANI
Askofu Nestor Timanywa



Contact Information
Bishop's House Ntungamo,
P.O.Box Private Bag,
Bukoba, Tanzania.
Tel. & Fax. 028 - 2220746
Office: Tel. 028 - 2220194
E-mail: b.officebk@yahoo.com
Website: www.bukobadiocese.co.tz
© Bukoba Catholic Diocese 2023
Find us on
Facebook: Bukoba Catholic Diocese
Twitter:  @bcdcatholic