Header

Walei: Mama Olive Luena

Walei

Kumbukumbu ya Miaka Kumi ya Kifo cha Mwadhama Rugambwa

Na Mama Olive Luen: Mwenyekti Halmashauri ya Walei Parokia Kuu ya Mt.Yosefu na Katibu Mkuu WAWATA Taifa

Kuanzia mwaka 1972 nimekuwa mwanaporokia ya Mtakatifu Yosefu parokia mama ya jimbo Kuu la Dar Es Salaam ambapo ndipo makao makuu ya Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Katika Kipindi hicho nimewahi Kushika nyadhifa Mbalimbali katika halmashauri ya Walei katika Kanisa hilo Kutokana na nafasi hizo , kwa namna ya pekee,niliweza kupata nafasi ya kumfahamu Mwadhama Laurean kardinali Rugambwa na mara nyingi kuweza kuwa na mazungumzo naye katika utendaji wa kazi ya parokia na katika matukio muhimu yote ya kijimbo ,kitaifa na kimataifa yaliyoweza kufanyika katika parokia yetu.

Walei

Mwadhama alikuwa Mtu Mpole na mcheshi kwa namna yake.Nakumbuka siku moja tukiwa katika hafla ya parokia' yeye akiwa mgeni rasmi, alituchekesha sana kwa kutupa hadithi ya mtu mmoja Ulaya aliyeibiwa jino la bandia la dhahabu alipokuwa akicheka! Tukio jingine nalolikumbuka ni lile alipokuja nyumbani kwangu na Paroko kuangalia Video tuyoichukua wakati wa ya kubariki Grotto ya Bikira Maria pale St Joseph, tukio alilolifanya mwaka 1988, Mwaka wa Maria. Wakati huo wanangu walikuwa wadogo sana , basi Mwadhama alimwuliza mwanangu wa kiume kama atakuwa Padre naye alijibu kuwa hataki kuwa padre bali anataka kuwa Kardinali kama yeye. Sote tulicheka sana.

Nakumbuka vile vile siku aliniita na kunionyesha barua iliyokuwa imeandikwa kilatini. Aliomba niisome na nimtafsirie. kwa hakika niligwaya kwa sababu sijui kilatini zaidi ya kile cha kuimba nyimbo za Misa za kilatini. Nilichoweza kubaini ni kwamba katika hati aliyotaka nisome na nitafsri kulikuwa na jina langu. Kumbe ilikuwa ni hati ya kuniarifu kwamba Baba Mtakatifu Yohani Paulo wa Pili aliniteua kuwa Mjumbe wa Baraza la Kipapa la Walei Vatikano (Pontifical council of the Laity.) Fikiria kiwewe kilichonipata . Sitamsahau alivyonipongeza na kunipa moyo na ushauri ambao ulinsaidia sana katika kipindi chote cha utumishi wangu katika Baraza hilo la kipapa. Daima nilipokwenda kwenye vikao huko Roma alipenda nimpe taarifa mbalimbali za yale tuliyoyajadili ambayo yangeweza kuwa na manufaa kwa Kanisa la Tanzania.

Walei

Nafasi nyingine ambayo ilinipa fursa ya pekee,ni ile ya WAWATA.Katika kipindi cha kuanzia 1982 hadi alipofariki nilikuwa kiongozi wa WAWATA katika ngazi ya parokia ,jimbo hadi taifa. Nakumbuka tullipoanzisha mpango wa mafungo ya Jumamosi ya Matawi kwa WAWATA, yeye ndiye aliuzindua mpango huo ambao unaendelea kwa mafanikio makubwa hadi leo. Kutoka na uwingi wa akina mama waliojitokeza alitoa mashine ya kuhesabia ili aweke katika kumbukumbu zake kwani alisema alikuwa hajawahi kuwaona akina mama wa jimbo kuu la Dar es salaam wakijitokeza kwa wingi kiasi kile. Mara kadhaa alitupa heshima ya kufungua, au kufunga mikutano yetu ya kitaifa. Akina mama wengi hasa wale wa mikoani ambo walikuwa wakimwona kwa mara ya kwanza, waliona wamebahatika sana kana kwamba wamemwona Baba Mtakatifu mwenyewe. Msongamano wa kumsalimia na Kubusu pete yake daima ulichukua muda mrefu sana! Hii ni dalili ya heshima na upendo ambao watu walikuwa nao kwake.

Wakati wa Ugonjwa wake,mara nyingi tulienda kumwangalia pale nyumbani kwake. Siku moja Ujumbe wa WAWATA ulipofika alituuliza tulikuwa tumemletea nini .Tulijibu kuwa hatukujua tumletee nini. Tulishikwa na aibu pale alitutania kuwa "Mngeniletea karanga".Kumbe kwa mama mtoto hakui!

Habari za Kifo chake nilipata nikiwa Brussels Ubelgiji, Nilikatisha shughuli zangu huko na kurudu haraka. Namshukuru Mungu kwamba niliwahi kurudi na kufika Bukoba kuhudhuria mazishi yake kuonyesha shukrani zangu Kwake na kwa Mungu.

Naamini yuko Mbinguni akituombea!

Mama Olive: Kwa niaba ya Walei
Contact Information
Bishop's House Ntungamo,
P.O.Box Private Bag,
Bukoba, Tanzania.
Tel. & Fax. 028 - 2220746
Office: Tel. 028 - 2220194
E-mail: b.officebk@yahoo.com
Website: www.bukobadiocese.co.tz
© Bukoba Catholic Diocese 2023
Find us on
Facebook: Bukoba Catholic Diocese
Twitter:  @bcdcatholic