ISSN 0865-6941 | Toleo Na. 307 | Machi 2016 | |
"Iweni Mtu Mpya"Ujumbe wa Pasaka wa Mha Askofu RwomaWapendwa katika Bwana, "Heri kwa Sikukuu ya Pasaka". Ujumbe wangu wa Pasaka wa mwaka huu 2016 umejikita katika upyaisho kwa njia ya maboresho ya maadili, uongozi, uaminifu na haki kama sehemu ya njia ya kuzuia kuota kwa majipu. Pasaka ni kipindi cha kuishi maisha mapya - maisha mazuri yaliyoboreka kutokana na neema zilizoambatana na kipindi cha Kwaresima. Ninashauri kiongozi na asiye kiongozi kupyaisha moyo wa kuwajibika, kwa namna moja au nyingine wote tu wafanyakazi na wote tu viongozi wa nafsi au watu wengine. Naamini kabisa ya kuwa kila mfanyakazi anastahili mshahara wake halali na wa haki. Marupurupu, takrima, nk, si mshahara, mfanyakazi asivifanye nyongeza ya mshahara au sababu ya mgomo wa kuendelea na kazi. Kila mfanyakazi afanye kazi yake bila kusimika nguvu ya utendaji wake katika matarajio mazito ya marupurupu nje ya mshahara au mkataba kama askari waliomuua Yesu -walivyojipatia marupurupu kwa kugawana mavazi yake. Bwana wetu Yesu Kristo anatuasa wote akisema, "…Nanyi mtakapokwisha kufanya yote mliyoagizwa, semeni, 'Sisi tu watumwa wasio na faida: tumefanya tu yaliyotupasa kufanya" (Lk 17: 10). Mtu aridhike na malipo ya haki anayopewa baada ya kufanya yaliyompasa kufanya. Tufufuke pamoja na Kristo. Tufahamu kuwa anayeshiriki meza ya Yesu awe upande wa Yesu. Mkristo asiwe kama Yuda msaliti aliyeshiriki meza ya Bwana khali akijua ya kuwa atamsaliti. Mkristo aliyefufuka na Kristo hatakubali kushiriki meza ya Bwana na meza ya shetani (1 Kor 10:21). Aliyefufuka na Kristo awe na msimamo katika dini yake, asiwe mtu wa kuyumbayumba kiimani tena, ukiyumba jamii ya waamini ikuitie nani kwa kukupatia huduma ya kiroho, padre au mchungaji au mpiga ramli? Kipindi cha baada ya Pasaka na kuendelea ni kipindi cha kuweka msimamo wako wazi. Kwa mantiki hiyo Mtanzania, kwa mfano, awe mzalendo, asiwe msaliti wa nchi yake kama Yuda aliyemsaliti Yesu kwa busu. Mashangilio ya kufufuka kwa Yesu yatoke rohoni. Mashangilio ya Kristo Mfufuka, makubwa na madogo ni mazuri. Lakini ukubwa wa mashangilio hayo usije kufanana, ukubwa wa kelele ya shilingi idondokayo sakafunia ambao si ukubwa wa thamani yake. Asemalo na kulitenda Mkristo lioneshe uwiano wa uzito wa imani yake ya ndani na nje katika Kristo Mfufuka na si vinginevyo. Viongozi walezi: wazazi, viongozi wa serikali, dini zote, na jamii kwa ujumla, tuishi kulingana na mafundisho ya maadili ya Mtanzania na ya dini. Ngoma na mavazi yake, kama vile vigodoro, michezo na mavazi yake, lugha na nyimbo, vioneshe kujali maadili na mafundisho ya dini. Mtu asikubali kufunga goli kwa mkono wa shetani na kuishia kumwagiwa sifa au mhusika kujisifu kana kwamba amefanya tendo tukufu - tendo lisilo na waa. Tuwatunze na kuwalea watoto wetu kulingana na maadili na maelekezo ya dini. Pasaka isherehekewa kwa kuwa na kiasi katika kula na kunywa, nk. Jamii ijiepushe na kukwaza kama Nuhu alivyowakwaza watoto wake kwa ulevi (Mwanzo 9:21). Watoto wetu tuwarithishe mikoba ya imani na maadili. Kila mmoja ataulizwa na Mungu amewajibikaje kulinda na kurithisha maadili. Ninaipongeza jamii kwa hatua zinazochukuliwa kutumbua majipu. Tufufuke pamoja na Kristo Mwalimu wa uaminifu, upendo na haki. Ninashauri zoezi la kutumbua majipu lipige hatua moja mbele ya kila mtu kutafuta muarobaini wa kuzuia kuota kwa majipu kwake na kwa wengine. Nyuma ya utumbuaji majipu pawepo mkakati endelevu unaolenga kutoa elimu ya kinga dhidi ya uotaji majipu kwa kuwa na katiba nzuri, sheria ndogo ndogo na nguvu ile ile na hata zaidi ya ile tunayotumia kujikinga na maambukizi ya kipindupindu. "Prevention is better than cure". Juhudi za kufanya kazi hii zisimalizwe nguvu yake kwa mabezo ya kukatisha tamaa kwa kuziita nguvu za soda. Katika kutenda mema hakuna kukata tamaa, ndiyo maana Paulo Mtume anasema, "Lakini ninyi ndugu, msikate tamaa katika kutenda mema" (2 Wathesalonike 3:13). Nawatakia furaha, amani, na baraka kutoka kwa Kristo Mfufuka na mwanzo mpya wa upyaisho wa maisha ya kiroho. Jipatie ridhiki kwa haki na kuonesha fadhila ya mapendo kwa matendo ya huruma kwa jirani masikini, tunaposherehekea Pasaka ya mwaka huu, "YANGUHA". Mtumishi wenu, +Desidrius M. Rwoma Askofu wa Jimbo Katoliki la Bukba. |