Header
rumuli

ISSN 0865-6941

Toleo Na. 306

Februari 2016

Waraka wa Kichungaji wa Mha Askofu Rwoma kwa Mwaka 2016


Wapendwa katika Bwana na Mkombozi wetu Yesu Kristo. Karibu katika mwaka mpya "Yangua". Baada ya kuangalia mwelekeo wa mfumo wa mazishi katika Jimbo letu nimeona inafaa nitoe ushauri wangu kwa nia ya kuleta maboresho katika taratibu za mazishi hasa katika kipindi cha siku chache za kabla na baada ya mazishi.

NINAISHAURI JAMII YA WAAMINI KUJALI MAHITAJI YA KIROHO YA MAREHEMU. Tusikimbilie kubadili mila na desturi kongwe bila tafakari na tathimini ya kina. Mabadiliko ninayoyaona sasa kwa asilimia kubwa yana mwelekeo wa kujali mahitaji ya kimwili ya watu wanaofika msibani kuliko mahitaji ya marehemu.

TUANGALIE MATUMIZI YA POMBE KATIKA SIKU ZA MSIBA. Wapo wanaotenga maisha ya binadamu katika sherehe tatu: ya kwanza ikiwa ni ya kuzaliwa, ya pili ndoa au wito wa utawa au upadre na ya tatu kifo. Sherehe za kuzaliwa, na ndoa hutawaliwa na furaha. Kinyume na sherehe hizo kwa asilimia kubwa sana wafiwa hawatakubali hali ya kufiwa waliyo nayo kuwa ni "sherehe ya kifo" kwa sababu moja kubwa kuwa kifo hutawaliwa na hisia za majonzi na huzuni. Hu ni ndio ukweli.

Kulingana na hali ilivyo sasa ipo haja ya kutumbua jipu. Lipo hitaji la kupiga vita ulevi wa pombe, si katika kipindi cha kufiwa tu bali siku zote. Inawezekana. Umoja ni nguvu. Siri ya mafanikio ni kutenda haraka (Lat. Secreto effecientiae est actionis sine mola: "The secret of success is action without delay").

Mila na desturi, mathalani za Wahaya, hazikupokea kifo kama sherehe ya kuadhimisha na kila mtu kwa shangwe, chakula na pombe kwa wote kama nionavyo mwelekeo wakati huu. Mabadiliko katika mila na desturi za jamii si haramu. Yatakuwa haramu kama yanapingana na amri za Mungu na katiba ya nchi.. Inasikitisha inapofika mahali msibani watu wakaingia unywaji pombe kiasi cha hata wafiwa kulewa na kushindwa kuwatambua waliofika kuzika na kuwapa mkono wa pole. Ni vizuri tukumbushane kuwa ulevi ni dhambi, ni ulafi na adui mkubwa wa afya roho na mwili wa binadamu. Ni muhimu mtu mmoja mmoja na jamii kwa jumla kutumbua jipu hili. Ukweli humweka mtu huru ingawa unauma.

Siku za maombolezo na mahali ulipo msiba (Kih. Omu biro byo'rufu na mbali balikutekera orufu) visigeuzwe kuwa mahali na siku za neema kwa wafanyabiashara ya pombe. Inasikikitisha kuona baadhi ya watu wamelewa siku chache kabla na baada ya mazishi kutokana na pombe inayotolewa bure kwa watu wanaofika kuwapa pole wafiwa. Kuhusu hili daima ninajiuliza marehemu au wafiwa wanafaidi kitu gani? Mpaka ninaandika makala haya sipati jibu chanya. Furaha yangu ni kwamba bila shuruti tayari baadhi ya parokia zimeliona hilo na kujiwekea mkakati wa kuondoa tatizo hili. Kipimo cha mfanikio ya mazishi ni kumzika marehemu kwa sala na heshima zote. Nashauri kabla na baada ya mazishi pawepo utaratibu wa Jumuiya (JNK) kumwombea marehemu na mtu kutafakari binafsi juu ya ubora wa kila mtu kukesha duniani kabla ya kifo chake.

Ngoma na tenzi za wajukuu ni kwa wajukuu. "Engoma no'kusilibya omu rufu biba bya abaijukuru." Je, hivi ndivyo hali ilivyo sasa? Muziki mzito na wa gharama kubwa siku za msiba, unaingiza kwa haraka katika jamii gharama kubwa na zisizo za lazima kwa familia ya wafiwa.

Licha ya kuwa mziki huo ni wa gharama kubwa, hata wanaoucheza si wajukuu na si kwa nia ya kuwaliwaza wafiwa kama lilivyokuwa lengo la miaka mingi ya ngoma na nyimbo za wajukuu. Kinachoendelea siku hizi mahali pengi ni burudani tu ambayo lengo lake si kufariji wala kuliwaza wafiwa.

Tudumishe utamaduni mila na desturi nzuri. "Engoma yabaijukuru no'kusilibya kwabo guba muruka gwa'baijukuru. Eikola elyo Tulibalekele. Ngoma na tenzi za kuliwaza na kufariji wafiwa ni wajibu wa wajukuu. Waachiwe hao kwasabu lengo lao ni wazi na kihistoria lina chimbuko lake.

Uzuri wa utamaduni wa ngoma na nyimbo za wajukuu ni kutumika kwa muda mfupi kila wanapofika watu maalumu wanaostahili kushirikishwa utani wao. Hali kama hii hupelekea kupatikana kwa muda wa kutosha wa sala za kumwombea marehemu.

Imarisheni utamaduni wa kuhani wafiwa. Mahitaji ya familia ya wafiwa daima ni makubwa. Sambamba na sala onesha ukarimu kwa kuhani wafiwa. Msaada wako utasaidia wafiwa kufuta deni linalotokana na gharama za kumuuguza marehemu, kumsafirisha kabla na baada ya kifo chake, au kulisha ndugu na jamaa waliofika kwa mazishi kutoka mbali.

NYIMBO ZA IBADA zinazotumika katika ibada za Mazishi na siku nyingine kama vile Jumapili, sikukuu na sherehe zioneshe kujali mchanganyiko wa waamini wanaoshiriki ibada. Zishirikishe kwa kutumia lugha hasa ya Kiswahili inayofahamika kwa wengi. Lugha ya Kilatini kama vile, Kyrie, Gloria, Sanctus, Agnus Dei, Salve Regina, Tantum ergo na kadhalika, zipewe kipaumbele katika baadhi ya sehemu za Misa Takatifu na maadhimisho mengine.

USHIRIKI WA WATU WA DINI TOFAUTI katika ibada ya mazishi na sherehe za kidini unakaribishwa. Hekima kila mara itumike katika kuwaeleza jinsi ya kushiriki ibada hiyo bila kusababisha uvunjifu wa amani.

"ENYUNGU Y'EMPISI," (Kih): "CHUNGU CHA FISI," Ni mlo wa ndugu wa marehemu ambao kutokana na kupokea wafiwa wengi tangu kufariki kwa marehemu hadi mazishi yake huwa hawapati muda wa kutulia na kula chakula. Mlo huu huwa hautolewi kwa kila aliyefika msibani. Pasipo kudumisha utamaduni huu, familia maskini zitafikia wakati ambapo zitalazimika kukopa fedha nyingi ili kupata uwezo wa kulisha na kunywesha watu wote waliofika msibani. Sasa hivi hali ni ya kadi ya njano kwa familia maskini, Je, tusubili hadi hali inakuwa ya kupokea kadi nyekundu mradi familia imefuta aibu ya kutowahudumia waliofika kwa msiba wa ndugu yao?

Tuionee huruma familia ya marehemu. Inampendeza Mungu, na ni faida kwa marehemu, siku ya mazishi inapokuwa fursa ya kumkomboa marehemu kiroho kwa kufupisha muda wake wa kukaa Toharani kwa njia ya sala.Tulenge hapo.

WAJUKUU WASICHELEWESHE IBADA YA MAZISHI. Ni jambo la hekima na ukomavu wajukuu kumaliza utani wao muda mrefu wa kutosha kabla ya kuanza kwa adhimisho la Ibada ya Misa Takatifu au Ibada ya Mazishi bila Padre. Ikiwa wajukuu wataona lazima ya kutamadunisha wafanye utani wao huo kwa heshima ya marehemu bila kuathiri muda wa kuanza na kumaliza mazishi. Kumalizika mapema kwa mazishi ni msaada mkubwa kwa waliotoka mbali. Wataweza kuwahi nyumbani kabla ya muda wa saa mbaya, saa ya "utawala wa wenye kiu ya makoromeo".

Matukio kama vile kutoa na kukimbia na mfuniko wa jeneza au jeneza lenyewe kwa madai ya kupewa "haki yao kwa kiasi cha fedha au kitu wanachotaka wao" ni kudhalilisha utamaduni, mila na desturi. Utamaduni udumishwe lakini usiadhibu wafiwa au waliofika kushiriki mazishi.

+Desidrius M. Rwoma Askofu wa Jimbo Katoliki la Bukba.

Jipatie Nakala Yako
Anuani:
Rumuli Printing Press
P. O. Box Private Bag, Bukoba
Cell:+255784-440 159 au +255768 - 761 270
Fax:2222113
E-mail: rumulipaper@hotmail.com

Contact Information
Bishop's House Ntungamo,
P.O.Box Private Bag,
Bukoba, Tanzania.
Tel. & Fax. 028 - 2220746
Office: Tel. 028 - 2220194
E-mail: b.officebk@yahoo.com
Website: www.bukobadiocese.co.tz
© Bukoba Catholic Diocese 2023
Find us on
Facebook: Bukoba Catholic Diocese
Twitter:  @bcdcatholic